01 March 2011

Yanga yaipiga kumbo Simba

*Yakaa tena kileleni

Na Nickson Mkilanya, Morogoro

MBIO za kupokezana vijiti za Ligi Kuu Tanzania Bara ziliendelea tena jana, ambapo Yanga ilikamata tena usukani wa ligi hiyo, baada ya
kuifunga Ruvu Shooting bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri.

Simba juzi ilikalia kiti hicho kwa muda, baada ya kuuchukua kutoka kwa Azam FC ambayo sasa imesukumwa hadi nafasi ya tatu.

Kwa ushindi huo Yanga, sasa ndiyo inayoongoza ligi hiyo kwa kufikisha pointi 38, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 37 na nafasi ya tatu ikikaliwa na Azam FC ambayo ina pointi 35.

Katika mechi ya jana, Yanga ilisubiri hadi dakika ya 77 ndiyo ikapata bao lake kupitia kwa Jerison Tegete, aliyefunga kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na Kiggi Makasy.

Mechi ya jana ilianza kwa timu zote kucheza kwa nguvu na kutafuta mabao haraka haraka, ambapo Yanga kupitia Davies Mwape na Tegete kuikosesha timu hiyo mabao ya wazi.

Ruvu Shooting ambayo jana ilicheza kwa tahadhari kubwa, nayo ilikosa mabao ya wazi kupitia kwa Revocatus Maliwa, Ayoub Kitala na Hassan Dilunga.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo wachezaji wa Ruvu Shooting walijitahidi kutaka kufunga mabao, lakini hata hivyo washambuliaji wake hawakuwa makini kila walipolifikia lango la wapinzani wao.

Dakika ya 58, Martin Mlolele aliikosesha Ruvu bao la wazi baada ya kupiga kichwa hafifu akiwa na kipa wa Yanga Yaw Berko.

Katika kipindi hicho kila timu ilifanya mabadiliko ambapo, Yanga iliwatoa Mwape na Ernest Boakye na kuwaingiza Ibrahim Job na Idd Mbaga.

Ruvu nayo ilimtoa Hamis Yakuti na Mangasin Mangasin.

Hata hivyo mabadiliko hayo yaliinufaisha zaidi Yanga, ambayo ilipata bao lake kupitia kwa Tegete dakika ya 77.

1 comment: