01 March 2011

Upelelezi dhidi ya kina Lukaza wahusisha Interpol

Na Benjamin Masese

KESI ya ya wizi wa mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu Tanzania (BoT) inayowakabili, Bw. Johnson Lukaza na
ndugu yake Mwesiga Lukaza iliendelea jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kwa upande wa mashtaka kueleza jinsi walivyofanya upelelezi.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya mwaka 2004/2005 walikula njama za kughushi nyaraka mbalimbali na kujipatia sh. bilioni 6 kwa njia ya udanganyifu kwa kutumia kampuni ya Changanyikeni Residential Complex Ltd ya Tanzania wakidai wanakusanya madeni ya kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan.

Akitoa ushahidi huo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Salim Kisai alisema jopo la upelelezi lilianza kufanya kutafuta zilipo ofisi za Marubeni na kuzipata nchini Kenya, kwa kushirikiana na Polisi wa Kimataifa wa Interpol.

Alisema kuwa katika harakati za upelelezi huo walikutana na Meneja wa Tawi la Marubeni na kupitia nyaraka mbalimbali zinahusiana na BoT.

Bw. Kisai alisema kuwa baadhi ya nyaraka zilionekana kusainiwa na viongozi wa tawi la Marubeni la Kenya, lakini uongozi uliokuwepo ulimkana kiongozi aliyesaini malipo hayo pia kutotambua mihuri iliyokuwa imegongwa katika nyaraka hizo.

Hata hivyo alisema mihuri iliyotumika kugonga nyaraka hizo ilikuwa tofauti na nyaraka za BoT.

Vile vile alisema kuwa upelelezi uliendelea hadi nchini Japani palipo na makao makuu ya Marubeni na kufanya mazungumzo na mkurugenzi wa kampuni hiyo ya uwekezaji wa magari aina ya Nissan na kupata nyaraka mbalimbali zinazohusiana na kesi.

Mawakili wanaowatetea kina Lukaza walimtaka Bw. Kisai kuonesha nyaraka alizozipata Japani, naye akadai kwamba alishindwa kuondoka nazo kutokana na utaratibu wao kuwa tofauti na wa Tanzania.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa tena Machi 28, mwaka huu ili kuendelea na ushahidi.

1 comment:

  1. THESE PEOPLE SHOULD BE LOCKED AWAY FOR A LONG TIME. AND IF NOT SO THEN TANZANIAN PEOPLE SHOULD TAKE TO THE STREETS - THE EGYPTIAN WAY!!!!!!

    ReplyDelete