01 March 2011

Man United, Chelsea patamu leo

London, England

MIAMBA ya soka nchini England, timu za Manchester United na Chelsea, leo zinatarajia kumaliza ubishi zitakapomenyana katika mchezo wa kwanza wa
Ligi Kuu, utakaopigwa Uwanja wa Stamford Bridge baada ya awali kuahirishwa kutokana na barafu.

Awali mchezo huo ulipangwa kupigwa Desemba 19, mwaka jana lakini kutokana na baridi iliyoambatana na barafu mchezo huo ukaahirishwa hadi leo usiku.

Kwa mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa Agosti, mwaka jana ambapo Man Utd iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Katika michezo mitano ya ligi hiyo hivi karibuni, Chelsea inaongoza kwa kuifunga Man United ambapo imeshinda mara tatu, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.

Ushindi wa United wa mabao 4-0 dhidi ya Wigan, mwishoni mwa wiki umeifanya United kufikisha pointi 60 wakiwa pointi nne zaidi ya Arsenal walio katika nafasi ya pili.

Katika ligi hiyo, Manchester United inaogoza ikiwa ikifuatiwa na Arsenal yenye pointi 56, huku Chelsea ikishika nafasi ya tano baada ya kujikusanyia pointi 47.

Endapo itaibuka na ushindi dhidi mabingwa watetezi Chelsea, kunaweza kuifanya United kuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kutwaa ubingwa na kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutwaa kombe hilo mara nyingi (19).

Liverpool imetwaa ubingwa wa Uingereza mara 18 ambao ni sawa na Manchester United.

Winga aliye katika kiwango cha juu Nani, ambaye amefunga mabao 10 na kusaidia mengine 14 msimu huu, hatacheza kutokana na kuumia katika mechi dhidi ya Wigan.

Naye Kocha Mkuu wa Man Utd, Sir Alex Ferguson alisema ni vigumu kuzungumzia mchezo huo lakini hafikirii kama ataupoteza kutokana na kiwango cha timu yake.

No comments:

Post a Comment