01 March 2011

Atakayeuza sukari zaidi 1,700/- kukiona

*Waziri ashangaa bei ya bidhaa hiyo Kagera
*Asema ni heri mkoa huo usiwe na kiwanda


Na Livinus Feruzi, Bukoba

WAKATI Rais Jakaya Kikwete ameagiza kuwa mfanyabiashara atakayeuza sukari zaidi ya
sh 1,700/- achukuliwe hatua kwa kuwa anadhulumu, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Balozi Khamisi Kagasheki, amesema Mkoa wa Kagera hauna haja ya kuwa na kiwanda cha sukari kama bei ya bidhaa hiyo inazidi kupanda ikilinganishwa na mikoa mingine.

Balozi Kagasheki alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano wa kuwashukuru wananchi wa kata ya Kagondo kwa kumchagua kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Alisema haiingii akilini kuona bei ya sukari mkoa wa Kagera inapanda kuliko mikoa mingine wakati inazalishwa mkoani humo.

Alisema Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda alishazungumzia suala hilo  bungeni kuwa Serikali Kuu kupitia kwa Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kufuatilia suala. Kwa sasa bei ya sukari inauzwa kati ya sh. 1,800 hadi 2,000.

Balozi Kagasheki alisema faida ya kujengwa kiwanda karibu na wananchi ni kuwasaidia kupata bidhaa kwa bei nafuu.

Alisema licha ya serikali kuruhusu soko huria, itafikia hatua  itaweka mkono wake ili bei isiendelee kupanda.

Jana, akihutubia wananchi, Rais Kikwete alikiri kuwa bei ya sukari nchini imekuwa ikipanda kwa kasi kubwa na katika baadhi ya maeneo nchini bei ya sukari ilifika zaidi ya sh 2,200 kwa kilo.

"Nilimuomba Waziri Mkuu kufuatilia kwa karibu tatizo hilo na amefanya hivyo. Alikutana na wadau wote wakiwemo wazalishaji na wasambazaji wa sukari nchini. Kilichobainika ni kuwa bei ya sukari ilipanda sana kwa sababu ya kuwepo upungufu wa sukari katika soko.

"Upungufu wa sukari katika soko ulikuwa umesababishwa na sukari iliyokuwepo katika maghala ya viwanda vya sukari na ya wafanyabiashara wakubwa wa sukari kutofikishwa kwa wingi madukani kwa hofu ambazo hazikuwa na msingi, yakiwamo mahusiano mabaya kati ya wazalishaji na wafanyabiashara wakubwa wa sukari.

"Wenye viwanda wakawa wanatoa kiasi kidogo kuliko wafanyabiashara walichokuwa wanaagiza. Kwa upande wao wafanyabiashara wakubwa nao wakawa wanasambaza kiasi kidogo kidogo kwa madai kuwa  wasijekuishiwa kabisa na bidhaa hiyo," alisema.

Rais Kikwete alisema Waziri Mkuu aliagiza sukari yote iliyoko katika maghala itoke mara moja na kufikishwa katika soko ili watu waipate tena kwa bei nafuu na kuwa hata kwa maeneo yaliyo mbali na viwanda vya sukari bei haiwezi kuzidi sh. 1,700 kwa kilo.

"Atakayeuza kwa bei kubwa zaidi ya hiyo anadhulumu, taarifa zitolewe ili hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kufutiwa leseni ya biashara," alisema.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kwa ajili ya kuziba pengo la miezi ya Mei na Juni kibali kimetolewa cha kuagiza tani 50,000 za sukari kutoka nje ya nchi.

"Tunatarajia kupata tani 12,500 kutoka nchi za Afrika Mashariki na tani 37,500 zitatoka nje ya Afrika ya Mashariki.

4 comments:

  1. Kagasheki, ulikuwa wapi kuyaona hayo na unayasema baada ya tamko la Serikali?

    ReplyDelete
  2. Kagasheki hivi KAGERA SUGAR iko umbali gani toka BUKOBA? Kwa nini usiende kupata undani kuliko kushangaa jukwaani?

    ReplyDelete
  3. Uchumi wa soko huria unategemea sana "demand and supply", sasa serikali imevuruga uchumi na haiweki mazingira mazuri ya upatikanaji wa sukari, kuwalizimisha watu bei ni kufanya hali iwe mbaya zaidi. Iwapo shilingi yetu itaendelea kuanguaka kwa kasi kama ilivyo sasa hakuna atayeagiza sukari au mali ghafi na vipuri katika uzalishaji wa sukari kwa dola inayopanda kila kukicha halafu aiuze sukari kwa bei poa! Hilo analosema rais si biashara ni siasa yakuwapumbaza watanzania!

    ReplyDelete
  4. Nini maana ya nguvu ya soko ambayo tumeikumbatia. Na pale nchi ikiendeshwa kifisadi utaona hata biashara zinaendeshwa hivyo hivyo. Suala la sukari kupanda bei si kwa bahati mbaya. Wanajua, sukari ni ishu kwa watanzania, then what they do, is to create a scacity scare, reduce supply and then politisize it. Bang!!!!!, si unaona sasa serikali inaagiza sukari kwa dharura (Unajua inapokuwa ni dharura maana yake ni nini????, lakini at the same time sukari ya Malawi kule mpakani Mbeya ni shilling mia sita (600) un beleavable. Kwa hiyo ukiiruhusu mpango wa kifisadi hautafanikiwa inawekwa marufuku kwa sukari hiyo kuhudumia mikoa ya karibu na Malawi. Ukikamatwa na TRA au serikali huko mbeya, mali yako inataifishwa na mahakamani juu (No msalie Mtume) wafanya biashara wanajua, wakikamatwa huwa wanaachia mali yao kwa madereva wasiojua kwa sababu gari hunganganiwa! na ili kukomesha kabisa hata gari lilobeba linawajibika kulipa mafaini mengi ambayo huwa alimanusra nalo kuuzwa/kunadiwa. haijalishi ni kiasi gani cha sukari ali mradi ni ya Malawi. Waulizeni watu wa Mbeya. Hii ni Tanzania yetu, msishangae sana kwa sababu maandalizi ya kukusanya fedha za kampeni ya 2015 imeshaanza. Hawangojei hadi kuchwe.

    ReplyDelete