14 February 2011

Walimu wa MEMKWA Kishapu wagoma

Na Suleiman Abeid, Kishapu
 
ZAIDI ya watoto wapatao 3,000 wilayani Kishapu mkoani Shinyanga waliopaswa kusoma kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi kwa
walioikosa (MEMKWA) wapo katika hatari ya kukosa elimu hiyo baada ya walimu kugoma kufundisha kutokana na kutokulipwa posho zao kwa kipindi kirefu.
 
Kwa mujibu wa habari zilizotolewa na baadhi ya walimu waliokuwa wakiwafundisha watoto hao wilayani Kishapu hatua ya kugoma kwao inatokana na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kushindwa kuwalipa zaidi ya sh. milioni 21 wanazodai kama posho ya kufundishia kwa zaidi ya miezi 10 ambazo hawajalipwa.
 
Mmoja wa walimu hao  aliyekuwa akiwafundisha watoto hao alisema wamefikia uamuzi wa
kugoma kufundisha masomo ya MEMKWA baada ya mkurugenzi kushindwa kuwalipa posho zao
kiasi cha sh. 21,600,000 ambapo kila mwalimu hupaswa kulipwa sh. 20,000 kwa mwezi.
 
Alisema mkurugenzi hakulipa posho hizo kwa miezi kumi tangu Januari 2010 mpaka Novemba, 2010 ambapo sasa wameamua kuacha kuendelea kujitolea na baadhi ya wenzake ambao si walimu wa kuajiriwa wameamua kujishughulisha na biashara nyingine ili kuweza kupata fedha za kuendeshea maisha yao.
 
Serikali ilikuwa na nia nzuri ya kuanzisha utaratibu wa kuwasaidia hawa watoto  ambao walichelewa kuandikishwa kuanza masomo ya elimu ya msingi, ndiyo maana ilibuni utaratibu huu wa MEMKWA, walimu wengi hufundisha kwa kujitolea huku wakilipwa fedha kidogo.
 
Lakini sasa tunavunjika moyo baada ya halmashauri kushindwa kabisa kutulipa posho
hizo kidogo tunazostahili,kila tunapoomba tunaelezwa halmashauri haina posho,tumeona bora tuachane na kazi hii, sisi tulioajiriwa tutaendelea na kazi zetu za kusomesha watoto wale wa kawaida, wale waliokuwa wakijitolea wameacha kufundisha, alisema.
 
Mgomo wa walimu hao utasababisha watoto wenye umri wa kuanzia miaka 10 hadi 18 waliokuwa wakisoma kupitia mpango huo wa MEMKWA kushindwa kuendelea na masomo yao na hivyo kuongeza idadi ya watu wasiojua kusoma, kuhesabu na kuandika katika Wilaya ya Kishapu.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Bw. Nyamuhanga alisema amesikia tatizo hilo lakini na amemwagiza Ofisa Elimu wa Wilaya ya Kishapu alifanyie kazi kwakuwa yeye ndiye anayepaswa kulishughulikia kwa kushirikiana na Ofisa Elimu ya Watu wazima wa Wilaya.
 
Ni kweli nimesikia walimu hao wameacha kufundisha, lakini mimi ni muidhinishaji tu wa malipo, fedha hizi hutolewa na serikali na siyo halmashauri, sasa ofisa elimu ya watu wazima kwa kushirikiana na yule wa Elimu wa Wilaya (DEO) fedha inapotumwa ndiyo huandaa malipo hayo, na mimi naidhinisha tu watu walipwe, alisema Bw. Nyamuhanga.
 

No comments:

Post a Comment