24 February 2011

NHIF yatoa msaada wa mil 9 Gongolamboto

Na Agnes Mwaijega

MFUKO Bima ya Afya nchini (NHIF) umetoa msaada wa dawa zenye thamani ya sh. milioni 9.1 na mashuka 600 kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa
milipuko ya mabomu iliyotokea Gongolamboto Februari 16 mwaka huu.

Msaada huo ulitolewa Dar ea Salaam jana katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), hospitali za Muhimbili, Amana na Temeke.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Naibu Mkurugenzi wa NHIF Bw. Hamis Mdee alisema wameguswa kuwachangia waathirika wa mabomu hayo kwa sababu tukio hilo ni la kitaifa na linawagusa Watanzania wote.

Alisema Mfuko huo una jukumu la kuisaidia jamii kila inapopata matatizo kama yaliyotokea Gongolamboto.

"Sisi kama sehemu ya Watanzania tumeguswa sana na tatizo liliotokea na tunatoa pole kwa waathirika wote," alisema.

Pia aliwataka wanachama wa mfuko ambao waliathirika wa milipuko hiyo na kupoteza vitambulisho vyao watoe taarifa katika ofisi za NHIF ili waweze kupata vingine.

Mkurugenzi wa Fedha katika Taasisi ya Mifupa (MOI), Dkt. Philemon Felix alisema NHIF imeonesha mfano mzuri ambao unapaswa kuigwa na mifuko mingine ya hifadhi ya jamii.

No comments:

Post a Comment