24 February 2011

Mwathirika wa makombora akataa msaada

GLadness Mboma na Peter Mwenda

MKAZI wa Mzambarauni Ukonga, Bw. Selemani Musa ambaye nyumba yake imeteketezwa kwa mabomu amekataa kupokea msaada wa chakula na
hema kwa madai kwamba vifaa hivyo viwasaidie waathirika wenzake.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mwembemadafu, Bi. Eva Mtanga alisema kuwa Bw. Musa ambaye pia ni mmiliki wa daladala zifanyazo safari za Gongolamboto kwenda Posta alikataa msaada huo baada ya kamati ya maafa kumpelekea msaada wa dharura.

"Sisi tulikwenda nyumbani kwake tukiwa tumebeba vyakula na mahema baada ya kuona athari ya kuteketea nyumba yake na mali yote iliyokuwemo ndani, lakini hatukumkuta, tulipata namba ya simu kutoka kwa jirani tukampigia, alitujibu kwamba msaada huo wapelekewe waathirika wenzake wenye shida zaidi kwani familia yake ameisambaza kwa ndugu zake," alisema Bi. Mtanga.

Waandishi walipofika katika nyumba hiyo walishuhudia nyumba hiyo ikiwa imeteketea kwa bomu na vitu vyote vilivyokuwemo ndani kuungua moto.

Bw. Musa amekuwa mfano wa kuigwa kwa watu wasio waaminifu waliozua mtindo wa kusingizia nyufa za nyumba zao zimemetokana na mabomu na hivyo kuwapa wakati mgumu watendaji wa mitaa.

Bi. Mtanga aliongeza kuwa mbali na mtindo huo kumezuka tabia ya baadhi ya watu kwenda katika nyumba zilizoathirika kwa mabomu hayo wakitaka kuzinunua ili waweze kufidiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Leonadis Gama amewaomba watu wanaotaka kutoa misaada waanze saa 6 na 7 mchana ili muda uliobaki kamati yake ifanye kazi nyingine.

No comments:

Post a Comment