Na Gladness Mboma
MWANAFUNZI wa Darasa la nne katika Shule ya Msingi Ukombozi Manzese, Alini Hamza amekufa juzi baada ya kuangukiwa na ukuta na kisha
kusombwa na maji kutokana na mvua iliyonyesha juzi Dar es Salaam.
Akizungumza na Majira Ofisa Mtendaji wa Kata ya Manzese, Bw. Bryson Mwango alisema jana Dar es Salaam kuwa kifo cha mtoto huyo kilitokea juzi majira ya saa saba mchana wakati mvua ilipokuwa ikinyesha.
Bw. Mwango alisema kuwa maji yaliizingira nyumba aliyokuwa anaishi marehemu na wakati alipokuwa akitoka nje na mama yake ukuta ulimwangukia na kisha kusombwa na maji.
"Baada ya ukuta kumwangukia mtoto huyo alisombwa na maji na amezikwa leo (jana) asubuhi katika makaburi ya Mnazi Mmoja Manzese," alisema.
Bw. Mwango alisema kuwa katika maafa hayo mama wa marehemu alijeruhiwa.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa Serikali ya Mtaa wa Mwembeni Manzese, Bw. Nestory Kobela aliwataka wananchi wa mabondeni kuwa waangalifu na familia zao wakati wa mvua.
Bw. Kobelo alisema kuwa kama wakiona mvua zimezidi wahame kwa muda katika nyumba zao ili kuepusha maafa, huku akiwataka kuimarisha ujenzi wa nyumba zao.
Katika hatua nyingine, Mwandishi Veronica Modest anaripoti kutoka Musoma kuwa nyumba 17 ikiwemo Zahanati na Kanisa la Menonite katika Kijiji cha Kirumi Wilaya ya Musoma Vijijini zimeezuliwa kwa upepo ulioambatana na mvua.
Diwani wa Kata ya Bukabwa, Wilaya ya Musoma Vijijini mkoa wa Mara, Bw. Muhoya Muriro alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 12, mwaka huu saa 9:30 alasili na kusababisha nyumba 17 ikiwemo kanisa na zahanatikuenzuliwa mapaa na nyingine kubomoka.
"Upepo mkali ulivuma kwa muda wa dakika tano hivi na ndipo tulipoona mabati yanapeperushwa na upepo na tulipotaka kujua yanatoka wapi, ndipo tukaona kanisa la menonaiti na zahanati vimeezuliwa mapaa,รข€ alisema Bw. Muriro.
Diwani alisema kuwa katika janga hilo mifugo nayo ilikufa, wakiwemo bata 13, kuku 10 na mbwa mmoja.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mjini, Kapteni Mstaafu
Godfrey Ngatuni mbali na kuwataka wananchi kupanda miti kwa wiki, aliwaomba wawasaidie wenzao waliofikwa na matatizo hayo wakati serikali ikisubiri tathimini kamili za mali zote zilizoharibika.
No comments:
Post a Comment