22 February 2011

Mmiliki Dowans utata

*Achanganya wananchi, wahoji maswali lukuki
*Mbunge ataka akamatwe apigwe picha kwa nguvu
*CTI wataka mitambo yake itaifishwe haraka


Na John Daniel

MBUNGE wa Ubungo Bw. John Mnyika ameitaka serikali kutumia vyombo vyake
vya dola kumtia mbaroni Bw. Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi, aliyejitaja kuwa ndiye mmiliki wa Kampuni ya Dowans Holdings SA na kampuni tanzu ya Dowans Tanzania Limited.

Mbunge huyo amesema serikali inapaswa kuchukua hatua hiyo kwa madai kuwa mtu huyo alishakana kuhusika na kampuni hiyo wakati alipohojiwa kuhusu uhusiano wake na Dowans.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bw. Mnyika kwa vyombo vya habari jana, Bw. Al Adawi anapaswa kutiwa mbaroni kwa kuwa ametii kile alichosema katika tamko lake la Februari 16, mwaka huu la kutaka mmiliki wa mtambo huo ajitokeze.

Alisema katika tamko hilo aliitaka serikali itaifishe mitambo ya Dowans na kuiwasha kama sehemu ya kupunguza makali ya mgawo wa umeme na kuwataka wamiliki wake popote walipo duniani kujitokeza hadharani iwapo wana sababu za kuepusha mitambo yao isitaifishwe.

"Nilitarajia mmiliki wa Dowans ambaye angejitokeza angekiri hadharani kama wamedanganywa na kampuni ya Richmond na vyombo vingine katika kuhamishiwa mkataba ili kuweka msingi muhimu wa majadiliano, lakini imekuwa tofauti.

"Kutokana na hilo naomba kutoa rai kwa vyombo vya dola vimkamate vimpige picha na kumuhoji Al Adawi kwa mujibu wa sheria ya uhujumu uchumi na sheria nyinginezo kutokana na maelezo tata yaliyotolewa mpaka sasa kuhusiana na kampuni ya Dowans," alisema Bw. Mnyika katika taarifa yake.

Alidai kuwa kilichomshangaza ni kuwa siku chache baada ya tamko lake Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja, alinukuliwa na gazeti moja Februari 18 mwaka huu kuwa serikali haitataifisha mitambo hiyo kwa kuwa hiyo siyo sera ya CCM.

"Ikumbukwe kwamba katika gazeti la Mwanahalisi toleo namba 128 la Machi 2009 Al Adawi alikanusha kuwa yeye sio mmiliki wa Dowans kama alivyonukuliwa katika Mahojiano na KLHN.

Kama amekuwa akikanusha kuwa si mmiliki lakini sasa amejitokeza kuwa ndiye mmiliki kuna kila sababu ya vyombo vya dola kumuhoji zaidi," alisisitiza Bw. Mnyika

Alitaka vyombo vya dola vimuhoji Bw. Al Adawi kuhusu utata wa kampuni ya Dowans Holdings SA ambayo kumbukumbu zake kamili hazipo Costa Rica inapoelezwa kusajiliwa na kuwa na ofisi zake.

"Kwa kuwa sasa wanaotajwa kuwa wamiliki wa Dowans wameanza kujitokeza ni muhimu pia wamiliki wa kampuni ya Portek Systems and Equipment PTE Ltd ambayo inatajwa kumiliki hisa takribani 40%  kwenye Dowans wakatajwa na wakajitokeza," alisisitiza. 

Alirejea ushauri wake wa kuitaka serikali kuitaifisha mitambo ya Dowans na kuchukua hatua stahiki dhidi ya ukiukwaji wa sheria uliyojitokeza ili kuepusha kasoro zingine kujitokeza katika hatua za dharura zinazokusudiwa kuchukuliwa hivi sasa.

"Kutaifisha mitambo ya Dowans sio kutekeleza sera ya chama chochote, ni kuzingatia maslahi ya taifa na kusimamia utawala wa sheria ikiwemo sheria ya uhujumu uchumi,"alisisitiza Bw.Mnyika katika taarifa yake.

Mbali na Bw. Mnyika, baadhi ya wasomaji wa gazeti walikerwa na kitendo cha mfanyabiashara huyo kukataa kupigwa picha ili Watanzania waweze kumuona, isijekuwa aliyejitokeza ni mtu mwingine asiyehusika.

"Biashara ni matangazo kama ilivyo siasa. Wafanyabiashara na wanasiasa ni watu wanaopenda kupigwa picha na kujitangaza Watanzania, Huyu Al Adawi ni mfanyabiashara wa namna gani asiyependa kupigwa picha na kuonekana? Sisi tuna walakini na biashara yake," alisema Bw. Jerome John, mkazi wa Kigilagila.

Mkazi mwingine wa Ilala ambaye hakutaka kutaja jina lake, alionesha hasira kwa wanahabari kwa kushindwa kumlazimisha Bw. Al Adawi kumpiga picha au kutunmia mbinu za kipaparazi kunasa picha yake ili iweze kuonekana.

Katika hatua nyingine, suala la Kampuni ya Dowans limezidi kuwachanganya wabunge baada ya watumiaji wakubwa wa umeme kuhoji Kamati ya Nishati na Madini, sababu za kushindwa kuishauri serikali kutaifisha mitambo ya  kampuni hiyo haraka kunusuru taifa.

Pia kamati hiyo ya bunge imetakiwa kujibu iwapo nchi haikufanya makosa kuingia katika mkataba na Dowans wakati bunge liliazimia kusitishwa kwa mkataba wa Richmond baada ya kubaini mapungufu kadhaa.

Katika kikao kilichofanyika Ofisi ndogo za Bunge Dar es Salaam jana kati ya Kamati hiyo ya Bunge na viongozi wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI), Baraza la Biashara la Taifa (TNB) na Mfuko wa Sekta Binafsi (TPSF) wadau hao walitaka kamati hiyo kuchukua hatua za haraka kunusuru uchumi wa nchi.

Vyanzo vyetu ndani ya kikao hicho vilieleza kuwa viongozi waandamizi wa taasisi hizo walionyesha wazi kukerwa na mjadala wa Dowans wakati nchi ikiwa katika hali ngumu ya umeme na kuitaka kamati hiyo kutoa majibu ya uhakika na kuweka siasa pembeni.

"Viongozi wa CTI, Bi. Esta Mkwizu, Bw. Arnold Kilewo na wale wa TPSF walituhoji ni kwa nini tunakazania tu kuzungumzia mitambo ya Dowans badala ya kuitaka serikali kununua mitambo yake.

Lakini kubwa zaidi walitaka mitambo ya Dowans itaifishwe haraka ili itumike kuzalisha umeme wa dharura kama mali ya nchi, walishangaa kwa nini nchi inapoteza mabilioni ya fedha bila sababu," kilisema chanzo chetu ndani ya kikao hicho.

Kwa mujibu wa chanzo hicho viongozi hao wa wafanbiashara wakubwa ambao ndio watumiaji wakubwa wa umeme kwa asilimia 8,0 waliitaka kamati hiyo kueleza iwapo si kosa kwa nchi kuingia mkataba na Dowans wakati bunge iliazimia kuwa mkataba wa Richmond haukuwa halali.

Awali akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo yaliyojiri katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Januari Makamba alisema wadau hao walilalamikia ukosefu wa umeme na kwamba hali hiyo imelisababishia taifa hasara ya mabilioni ya fedha.

"Tatizo la umeme ni kubwa kiuchumi, kwa mfano Twiga Cement pekee licha ya kutumia jenereta bado wanapoteza karibu milioni 20 kwa siku.

Kama taifa tunapoteza karibu dola za Marekani 200,000 kwa siku kutokana na ukosefu wa umeme, hii ni hali mbaya sana, ndio maana tumelazimika kuzungumza kwanza na wadau kujua ukubwa wa tatizo kiuchumi," alisema Bw. Makamba.

Alisema katika kikao hicho ambacho kilikuwa bado haijafikia mwisho CTI waliweka wazi kuwa kati ya viwanda 280 vinavyomilikiwa na wanachama wake 50 wameshindwa kuendelea na uzalishaji na kusitisha kazi kwa muda kwa ukosefu wa umeme.

"Kama mnavyojua tunatakiwa kuanza vikao vyetu wiki mbili kabla ya bunge lakini tuliomba kibali maalumu kwa Spika kufanya vikao kutokana na ukubwa wa tatizo hili, leo (jana) tumekutana na wadau, kesho (leo) tutakutana na Wizara ya Nishati na Madini na kesho kutwa TANESCO.

"Pia Jumamosi tutaitisha public hearing (mdahalo wa wazi) pale Karimjee, tutaandaa vizuri ili tupate mawazo ya wadau kwa utaratibu mzuri," alisema Bw. Makamba.

Alisema Kamati hiyo itakutana na wadau wote wanaohusika na umeme wa gesi ili kutoa mapendekezo yatakayokidhi haja ya taifa kuondokana na adha ya sasa.

Alisema Kamati yake haijatoa mapendekezo yoyote kuhusu mitambo ya Dowans na kwamba kilichonukuliwa na vyombo vya habari yalikuwa maoni yake binafsi kabla ya kikao cha kamati hiyo.

"Kamati itatoa mapendezo yake kwa serikali Jumanne ijayo baada ya kumaliza kazi yake, kwa sasa tunaendelea na vikao ili kujua nini kinachotakiwa hasa kuokoa taifa letu na ukosefu wa umeme," alisema.

Alipoulizwa iwapo Kamati yake itamwita mtu aliyejitangaza kuwa mmiliki wa Dowans anayedaiwa kutua nchini juzi na kuzungumza na wahariri wa vyombo vya habari kwa sharti la kutopigwa picha alisema hawana sababu ya kufanya hivyo.

Hata hivyo alisema uamuzi wa serikali kutumia au kutotumia mtambo wa Dowans kuzalisha umeme wa dharura kwa sasa ni uamuzi tu na kwamba si jambo gumu na kufafanua kuwa kamati yake haiwezi kuishinikiza kufanya hivyo au kutofanya.

Alisema kabla ya kutoa mapendekezo yake kamati yake itafanya ziara kujionea hali halisi ya nishati hiyo katika vituo vyote vinavyozalisha umeme isipokuwa Mtera ambapo tayari wametembela.

19 comments:

  1. Sawa kaka Mnyika, Kaza buti na wabunge wengine wakusaidie katika hili bila kujali itikadi zao za kisiasa. Ukisikia utapeli wa kimataifa ndio huu. Sasa watanzania tuamke na tuwe makini katika hili. Hapa ndio patamu na pa kujua mbivu na mbichi katika sakata hili. mwananchi/ Mtanzania mwenzangu nina maswali kadhaa ambayo ningependa nikushirikishe katika kuyatafakari:-
    1. Hivi umewahi kusikia wapi mwekezaji safi katika moyo wake (Adilifu) na mwenye nia njema katika biashara zake kukataa kuonana na viongozi wa serikali, kukataa kupigwa picha, kukataa kurekodiwa katika vyombo vya habari? Kwangu mie huyu ni mwizi na ni tapeli mzoefu, mbabaishaji na ni mtu wa kutunga umiliki wake wa kampuni.
    2. Taarifa ya kamati ya bunge chini ya Uenyekiti wa Mh. Mwakyembe iliyopelekea Waziri Mkuu Lowasa kujiuzulu ilibainisha kuwa kampuni hii haijawahi kuwepo katika rekodi zozote za makampuni duniani; na hasa Costa Rica, Tanzania wala Canada. Sasa iweje leo ajitokeze kuja kuelezea umiliki na uwepo wa kampuni ya Dowans duniani na kwamba yeye ndiye mwenye hisa nyingi??
    3. Katika kikao na waandishi wa habari (wakati anafafanua ugomvi wao na mzee Mengi juu ya mafisadi nyangumi na papa), Mh. Rostam Aziz - Mbunge wa Igunga alikana kuhusika kwake na kampuni zote mbili za umeme na kwamba hahusiki hata kidogo katika umiliki huo achilia mbali kusemasema na kujitokeza hivi karibuni. Je umiliki wake wa hisa ni wa aina gani? Je uongozi wake kama mbunge hauna shaka? Je uaminifu wake katika nchi yetu uko wapi? Je anafaa kuendelea kuitwa kiongozi wa watu kama aliwaficha/ aliwakana wawekezaji hapo awali? Mbunge aliyeapa kuitetea katiba, kuwa mwaminifu katika nchi yake, kutunga sheria za nchi na kutoa ushauri kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu??
    4. Tapeli Adawi aliwahi kuhojiwa juu ya umiliki wake wa Dowans akakana. Leo anadiriki kujitokeza na kutaka kutuaminisha kuwa ni mmiliki halali wa kampuni ya Dowans. Hivi huu si ni ujinga na utapeli wa hali ya juu?

    ReplyDelete
  2. 5. Kwa kukataa tu kuonana na viongozi wa serikali, hatuoni kuwa kuna walakini hapa!! Kwanini mwekezaji halali wa kampuni aogope kuongea na viongozi? Ama atuambie ana watu wanaoshirikiana nao pale TANESCO au ni tapeli tu!! Kukataa kuonana na viongozi wa serikali si ni udhalilishaji na taifa (Nation Sovereignity)? Je ni halali mwekezaji kuweka masharti ya kutokuonana na viongozi ambao hiyo TANESCO inakuwepo kutokana na baraka ya viongozi?? Na hasa ukizingatia wingu kubwa lililopo katika nchi yetu kwa wakati huu? Yaani hata Waziri wa Nishati ambaye alikuwa anatetea kulipa deni naye ni adui wake?? Hapana hapa kuna jambo. Hivi Usalama wa taifa mko wapi na kwanini hamumshughulikii huyu jamaa ambaye anadhalilisha viongozi wetu?? Zoka upo au unajua kuwadhibiti wapinzani tu? Unbearable!!
    6. Katika hotuba yake siku ya maadhimisho ya CCM, Mh. Rais Kikwete alisema hawafahamu wamiliki wa Dowans na kwamba haungi mkono kuwalipa Dowans. Imani yangu inaniambia kuwa Kikwete ni "baba" yetu (Nyumba ya Tanzania) na akisema deni, lisilipwe maana yake ni kuwa hatalipwa. Nilifikiri Adawi angesema anahitaji busara ya Rais ili alipwe badala yake anasema hataki kuonana na viongozi. Huu ni ubabe wa aina yake ndugu zangu watanzania na haupaswi kuachiwa kiuzembe namna hiyo. Kikwete unavumilia tu, Diplomacy?? No, No, No! Kila kitu kina ukomo wake kaka yangu Kikwete; Acha uzoba!!
    7. Kuna baadhi ya wachangiaji katika matoleo yaliyopita wanashauri mwekezaji akae na TANESCO ili waone jinsi ya kupunguza au kusamehe deni. Hili ni jambo jema kabisa; lakini kwanini Taifa linyanyaswe na kudharauliwa hivyo? Mtu hataki kuonana na viongozi wetu (Hata kama walipatikana kwa kuchakachua), anawadhalilisha na kuwabeza. Hii sio haki na haihitaji kunyamaziwa hata kidogo. National Sovereignity has its space in here, we need to be a bit more serious than this otherwise we are welcoming Neo Neo Neo Colonialism in our country!!. Jambo la busara hapa ni kuitaifisha mitambo, kumtia adabu huyu mdharau viongozi wetu na tapeli wa kimataifa anayejitokeza siku za mwisho baada ya jambo hili kushika kasi.
    8. Sakata hili limedumu kwa zaidi ya miaka mitano. Siku zote limewasumbua watanzania; viongozi na wanataaluma ndani na nje ya nchi. Hivi haiwezekani kuwa Rostam na wengine wamehusika kumshawishi huyu Adawi kujitokeza kuwa mmiliki halali ili malipo haya yaende kwake na wagawane na wamiliki uchwara?? Tukumbuke kuwa wote walikana kuhusika na kampuni hii; na kumbukumbu tunazo kupitia vyombo vya habari. Ikumbukwe pia matapeli huwa ni wajanja na wana mbinu mbalimbali za kutafuta fedha. Hivyo, sishangai kujitokeza kwa Adawi kuja kudai malipo hayo na ikizingatiwa udhaifu wa kisheria tulionao/ tuliouonyesha hadi sasa. Inawezekana kabisa kuwa hata viongozi wetu wamehusika kumwita huyu FISADI wa kimataifa maana watapata share yao. Ni wakati wa viongozi wetu kuonyesha misuli yao kisheria. Kikwete usikubali kudhalilishwa. Huu ni mchezo mchafu na haufai hata kidogo. Mkamateni na ashughulikiwe. Yapo mengi naweza kuyasema lakini naomba maswali yangu yaishie hapo kwe leo. "Hakuna Mjomba atakayetoka nje kuja kuwasaidia watanzania, kama yupo naomba mniambie/ mnitajie....." Mwl. Nyerere!!. Ewe mwananchi, tafakari na chukua hatua ndugu yangu Mtanzania.

    ReplyDelete
  3. Huyu mmiliki wa dowans ni mwizi inatakiwa akamatwe.

    Hongera mnyika wewe ni noma hata Bana alikukubali kwenye mdahalo!!!!!!!!!!!!!!111

    ReplyDelete
  4. mh inabidi uchunguzi ufanyike maana, itabidi tupate majibu ya kila tatizo kabla ya kiongozi kuleta hoja kwa wananchi. jamani tukumbushane zile ahadi zetu za mabilioni, mimi nataka nione mv bukoba mpya tu.

    ReplyDelete
  5. .

    Huu ni mpango uliosukwa na Rostam ili ajinasue na wagawane hizo hela ! Watanzania HATUDANGANYIKI NG'O !

    Paul

    .

    ReplyDelete
  6. .


    Mhhhh Hapa unapata "live" picha za aina ya "wawekezaji" wa serikali tapeli ya Kikwete. Asilimia 90 ya mikataba yote nchini imesainiwa Kitapeli kama huu wa Rostam na CCM !! Tanzania amkeni, yaliyotokea Misri, Tunisia na sasa Libya hayako mbali !!! CCM lazima iondoke !!

    Paul
    .

    ReplyDelete
  7. Paul kweli umenena. Hii ni mbinu ya ROSTAM AZIZ kutaka kujichotea kilaini fetha zetu kwa kumtumia tapeli wa kiarabu. Rostam na huyu tapewe wakamatwe, wapigwe jela --- Wanatuchezea akili, hawana Adabu kabisa !

    ReplyDelete
  8. huyo mnyika asitake kuleta siasa za Chadema ndani ya suala la umeme viongozi kama yeye wanaoweka jazba mbele kuliko busara ndio watakaosababisha matatizo makubwa zaidi kwa taifa. Siasa za utaifishaji ndizo zilisababisha wawekezaji wengi kuikimbia Tanzania na kwenda kuwekeza Kenya. Dowans wamenunua mitambo kutoka Richmond, Tanesco wameingia mkataba na Dowans wa kuzalisha umeme jambo ambalo walilitekeleza kwa ufanisi mkubwa. Viongozi wetu wa kisiasa kama Mnyika wakavunja mkataba kwa jazba kisa mitambo imenunuliwa Richmond¡, kosa la Dowans ni nini? Tung'oe kwanza borit i kenye macho yetu ndipo tuone kibanzi kwenye macho ya wenzetu. Tunahitaji umeme sio siasa wala maoni ya wasomi Tanesco iachwe ifanye kazi bila kuingiliwa na wanasiasa uchwara kama Mnyika
    i

    ReplyDelete
  9. JAMANI MNYIKA HAYALETA SERA ZA CHADEMA,MEME NI CCM SAFI,ANATAKA MAMBO YA HUYU TAPELI WA ROSTAM YAWE BAYAHA.
    HAPA HATA MTOTO MDOGO ATAJUA TU KUNA MBINU CHAFU ZA ROSTAM AMBAZO NI ZA CCM.ROSTAM NI CCM NA WAMEKAA KIMYA,HAWAWEZI KUMHUKUMU ROSTAM NI MFADHILI WAO MKUBWA HASA KWENYE UCHAGUZI MKUU.NI KIGUGUMIZI KITUPU SASA,HUYO MWARABU KALETWA KUZIBA PUMZI ZA SISI WAJINGA,KUMBE KUNA WENYE AKL WAMESHTUKIA MTEGO.
    HUYO TAPELI NA MWENYEJI WAKE ROSTAM WAKAMATWE.ULIONA WAPI TAJIRI ANAKATAA HATA PICHA.NI TAPELI. MNYIKA HIYO MITAMBO IKO JIMBONI KWAKO,KOMAA NA HAO MATAPELI,USIKUBALI.SASA HIVI HATA WAJINGA TUNA AKL,TUMEONA TUNAVYOCHEZEWA,WAKUBWA HAWAONGEI MAANA WANAFAIDI VYA ROSTAM VINGI TU,MFADHILI WAO.WAKO KIMYA!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  10. HIVI HUYO ANAYEJIFANYA NDO MMILIKI JINALAKE LILIKUWEPO KWENYE YALE MAJINA YALIYOTANGAZWA NA WAZIRI KWA MARA YA KWANZA YA WAMILIKI WA DOWANS AU TUNAONYESHWA MAZINGAHOMBE.

    ReplyDelete
  11. Naomba majina ya wamiliki wa waliotajwa na mh. Ngeleja tafadhali tuoanishe na huyu asiyetaka kupigwa picha kama limo!

    ReplyDelete
  12. Na nyie waandishi, uoga gani huo? Watu wakikaa uchi mnawapiga picha na kuwaandika mambo ya aibu bila ruhusa zao, inakuwaje huyo "Dowans" mnashindwa kumpiga picha? Mnaomba kumpiga picha mtu ambae uwepo wake tu ni news? Hiki ni kichekesho. Ingekuwa nchi za wengine kungekuwa na mapicha lukuki kwenye magazeti, tv na kila mahali, hiyo haiombwi, toka airport palepale unagonga tu. Acheni uoga bwana!

    ReplyDelete
  13. Ukweli ni kuwa fidia inayotakiwa kulipwa na TANESCO ni karibu sawa na bei ya kununulia mitambo kama hiyo. Busara itumie kama wanaweza kulipa fidia hiyo kwanini mitambo kama hiyo isinunuliwe? Kuna watu wajanja wanaotumia uelewa mdogo wa viongozi wetu na kuwanyonya watanzania. Hakuna haja ya kulipa fedha hizo kwani ni mchezo unaochezwa na watu wachache kuibia nchi.

    ReplyDelete
  14. KWAKO SAIDI MWEMA,
    Kwa mujibu wa record zilizowakilishwa na Richmond kwa serikali ni kwamba kampuni ya Richmond iliandikishwa rasmi Houston Texas,mwanasheria mkuu wa Texas GREGG ABBOT aliithibitishia tume ya mwakyembe kuwa kampuni hiyo haijawai kusajiliwa TEXAS kwahiyo documents zilizowakilishwa na Richmond ambaye ndiye mzazi wa DOWANS zilikuwa FEKI na kwa mujibu wa sheria za nchi kuwakilisha documents feki ni kosa LA JINAI kwahiyo inabidi ALDAWI akamatwe kwa kuwakilisha feki documents ili kujipatia tenda/nafasi ya kufanya biashara na serikali. kwahiyo kwa kuwa kila siku umekuwa ukisisiza kuwa nchi hii uongozwa kwa mujibu wa sheria sasa inabidi uchukue hatua kwani ili tuone kweli maneno yako unamaanisha.

    ReplyDelete
  15. Nampongeza Ndugu Mnyika kama tungekuwa na wabunge ambao wapo wazi wa aina yake nadhani majanga matatizo menge yanayojitokeza yangepungua. Wengi wa viongozi wetu wanaogopana hivyo kukalia uovu. Ndugu I unayesema Mnyika analeta sera za CHADEMA kwa mawazo yako ni kweli maana za CCM ni kuficha uonvu na kukumbatia uhalifu hata kama uko wazi na ndio chanzo cha matatizo yote hata haya ya DOWANS, SIDHANI NI KWELI KWAMBA RAIS ASIJUE KWAMBA KAMPUNI HIYO NI NANI WAKATI IPO NCHINI MWAKE NA INALALAMIKIWA KILA SIMU, mini minaamini anazo habari zote kwani sio mjinga asitake kujua kinachosumbua wananch wake. Tatizo ni kwamba serikali yetu imefanya utumbo ulio kithiri hadi wananchi kufikia kuwa na mashaka nayo. Waswahili wanasema " UKILA NA KIPOFU USIMSHIKE MKONO" Sasa imefikia kwamba sisi wananchi tumeshikwa mkono na si mkono tu hadi kuvutwa nyuma. Wabunge wengine mliochaguliwa na wananchi tunawaomba mtusaidie maana ninye ndio wawakilishi wetu.

    Aminani

    ReplyDelete
  16. Sasa nadhani watanzania mmeona jinsi gani tunavyoweza kudanganywa kwa kofia ,vitenge, sukari,t-shirt na hawa ccm akina Rostam huko Igunga baadaye kuwapa kura. Rostam na viongozi wa ccm hawawezi kuongea lolote juu ya Al Adwi ni mwenzao na wana share hata Kikwete ambaye alipiganiwa na Rostam kuwa madarakani. Jambo moja tu Kikwete na serikal yake waondoke ndiyo tutpata nafuu ya maisha. Watanzani njia ni ileile walofanya MIsri, Tunisia, na sasa Libya, tumwondoe Kikwete. Msidanganywe ataweka tume ni uongo mtupu, maana hata tume iliyosema Dowans matapeli wala haipo haikusikilzwa.Watanzania jitokezeni kesho mitaani nchi nzima Kikwete aondoke ili tupate umeme na mengineyo.

    ReplyDelete
  17. Kwa hii style ya kutokutaka apigwe picha sidhani kama huyu jamaa (anayejitaja Al Adawi na mmiliki wa Dowans) ni original Al Adawi.

    Yaani kuanzia uwanja wa ndege anapoingia mpaka anaondoka hakuna aiyempiga picha! Hata camera za ulinzi za airport na ikulu hazijamnasa tuone sura yake inafananaje?

    ReplyDelete
  18. Hivi kweli vyombo vya habari vyote vimenunuliwa na Dowans kiasi cha kutokumpiga picha mmliki wake?
    Na vyombo vya dola hawaoni kuwa huyu jamaa ana kesi ya kutudanganya?

    ReplyDelete
  19. Wamekula kwa vijiko weeee, wakaona kuwa hawashibi mhh sasa wameamua kujilisha kwa kutumia MAKOLEO matokeo yake mdomo umekuwa mdogo! vimemwagika nje nasi tumeona HONGERA mH. rAhIsI kIWetE kwa kutupatia MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA. HONGERENI SANA CCM maana sera zenu za kuiba mali ya nchi zinafanikiwa kwa kiwango cha juu.

    ReplyDelete