15 February 2011

Mbowe atangaza baraza dogo

*Lina mawaziri 29 kutoka CHADEMA pekee
*Wapinzani wengine kufikiriwa baadaye


Na Kulwa Mzee, Dodoma

KIONGOZI wa Kambi ya Upinzania bungeni, Bw. Freeman Mbowe ameteua
Baraza la Mawaziri Kivuli lenye wabunge 29 kutoka CHADEMA ili kutekeleza dhamira ya chama hicho kuwa na baraza dogo.

Bw. Mbowe alitangaza baraza lake la mawaziri jana bungeni na kusema kwamba pamoja na serikali kuwa mawaziri ya manaibu 50, ameteua hao wachache ili waishi kwa vitendo kutokana na kilio chao cha kuwa na baraza dogo la mawaziri.

Alisema kwa kuwa CHADEMA ndiyo iliyotimiza yatokanayo na kanuni ya 14 fasili ya (4) ya kuchagua Kiongozi wa Kambi ya Upinzania Bungeni, hivyo ameamua kwa sasa kuunda baraza la mawaziri kivuli kutoka CHADEMA peke yake wakati mazungumzo na wapinzani wengine yakiendelea.

Mbali na yeye atakayeongoza Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Mbowe amemteua Bi. Raya Khamis, (Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu wa Bunge) na Bi. Esther Matiko (Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji). Manaibu waziri katika wizara hiyo ni Bw. Silinde Ernest (TAMISEMI-Utawala) na Bw. Vicent Nyerere (Elimu).

Mawaziri kivuli Ofisi ya Rais ni Bw. Said Arfi (Utawala bora), Mchungaji Israel Natse (Mahusiano na Uratibu), Bi. Suzan Lyimo(Menejimenti ya Utumishi wa Umma).

Bi. Pauline Gekul anakuwa Waziri Kivuli Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Bi. Grace Kiwelu (Mazingira) na Bw. Zitto Kabwe kateuliwa kuwa Waziri Kivuli Wizara ya Fedha na Naibu wake ni Bi. Christina Mughwai.

Wizara ya Mambo ya Ndani aliteuliwa Bw. Godbles Lema, Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Tundu Lissu; Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Ezekia Wenje, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bw. Joseph Selasini na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Silvester Kasulumbayi.

Wengine ni Profesa Kulikoyela Kahigi anayeshika Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Halima Mdee, Maliasili na Utalii, Bw. Peter Msigwa, Wizara ya Nishati na Madini, Bw. John Mnyika,Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Salvatory Machemuli, Wizara ya Uchukuzi, Mhonga Ruhwanya, Wizara ya Viwanda na Biashara, Bi. Lucy Owenya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Christowaja Mtinda na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Mbasa Gervas.

Wizara ya Kazi na Ajira, Bi. Regia Mtema, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Naomi Kaihula, Wizara ya Habari, Vijana na Michezo, Bw. Joseph Mbilinyi, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Mustapha Akunaay, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Opulukwa Meshack na Wizara ya Maji, Bw. Highness Kiwia.

Bw. Mbowe alisema pamoja na kutambua kuwa kanuni za bunge zimebadilishwa na kuwa wabunge wote wa upinzani wako chini yake, ameamua kuwateua wabunge wa CHADEMA pekee kwa kuwa bado mawasiliano hayajakamilika na vyama vingine na kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na baraza hilo kwa sasa.

"Ni matumaini yangu kuwa hapo siku za usoni na baada ya kuelewana na kuridhiana na wenzetu, nitaweza kuunda baraza litakaloshirikisha vyama vingine kutoka kambi rasmi ya upinzani bungeni," alisema.

Bw. Mbowe alitoa rai kwa serikali kwamba watendaji watoe ushirikiano kwa wasemaji ili waweze kutekeleza majukumu yao kuimarisha demokrasia.

"Uzoefu unaonesha kuwa wasemaji wa upinzani wamekuwa wakionekana wanoko, vizabizabina na wasio na uzalendo pindi wanapohoji na kukosoa, muono huu uondoke kwani lengo letu sote kujenga nchi iwe na uchumi imara na demokrasia ya kweli kwa ajili ya maendeleo ya watu," alisema.

Aliwapongeza wabunge wa upinzani waliochaguliwa kuongoza kamati za bunge za udhibiti wa fedha za umma na kuwahakikishia ushirikiano wake na baraza lake.

Alipomaliza kutangaza baraza hilo, Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda alisema alichofanya Bw. Mbowe ni kwa mujibu wa kanuni za bunge, na kuwataka wabunge kukubaliana na Kiongozi wa Upinzani na ahadi yake kuwa bado anayo nafasi ya kulibadili na kushirikisha wapinzani wengine kadri atakavyoona inafaa.

Wakati baraza hilo likitangazwa, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod alikuwa bungeni kwenye eneo la wageni akisikiliza.

Akimtambulisha Dkt. Slaa, Spika Makinda alisema alikuwa mbunge shupavu na mchapakazi, akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu ya Serikali za Mitaa na kumalizia kuwa 'tutammisi sana kwenye kamati hiyo'.

18 comments:

  1. Chdema ubinafsi utakuwekenipabaya acheni uchu wa madaraka kwa kweli tunakudegemeeni kutuletea maendeleo lakini dalili ya mvua ni..............

    sijui tutafikia wapi kwa hali hii kambi ya upinzani inaelekea wapi sasa heeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee. haya tutaonaaaa..........

    ReplyDelete
  2. Bora kambi ya upinzani hata iwe na mbunge mmoja kuliko kuwa na wabunge wengi halafu wengi wao ni mamluki, Chadema mko sahihi msije mkaingiza mamluki wakabeba na wengine kuwarudisha CCM, komaeni hivyo Chadema tuko nyuma yenu. Upinzani lazima uwe wa kweli sio wa kinafiki eti ilimradi wapinzani tu ndio wajumuishwe kwenye kambi ya upinzani.

    ReplyDelete
  3. Hivyo hivyo CHADEMA mpaka kieleweke. CUF, TLP, NCCR imejaa Mamluki, Ndumilakuwili. Kaza buti Mungu ni mwema tutafika tuuuu!

    ReplyDelete
  4. eng Mwakapango,E.P.AFebruary 15, 2011 at 8:44 AM

    watanzania tunawatakia kila la kheri wabunge mliochaguliwa kwenye baraza la mawaziri kivuli. nyinyi ni watch dogs ambapo mtakutana na mambo mengi ikiwa ni pamoja na misuguano na chama tawala na sisi watanzania tunataka vitu mbadala na kama vina mantiki Rais aliyeko madarakani avichukue. Rais Dr Jakaya Mlisho Kikwete aliahidi kusoma ilani za uchaguzi 2010 ya vyama vyote na kuchukua mazuri hata kama hayako kwenye sera za CCM na huo ndiyo uungwana. nimelipenda baraza la mawaziri ni zuri sana nawaheshimu vijana wapiganaji wenzangu akina Tundu lisu sasa wafanyeni kazi kama mawaziri ili wakonge nyoyo za watanzania. unajua wanaowapa kura si wanachama wa vyama vyenu kwani kitakwimu wanachama wa vyama siasa hawazidi milioni sita. kuna watanzania waajabu sana nadhani upeo wao mdogo mtu kama Maria Hewa jamani CCM watu hawa wanazidi kuwapotezea kura yeye anawashangaa watu wa Mwanza kuwapa CHADEMA. namtaarifu kuwa isingekuwa uchakachuaji hata nafasi yake ubunge wa mezani asingepata ashukuru wachakachuaji. CHADEMA SONGA MBELE muwathibiti mafisadi ndani ya Serikali nchi ni yetu wote.

    ReplyDelete
  5. wewe unayesema CHADEMA wajiunge na wenzao,unanjua maana ya mwezako?? Mwezako ni yule mnayekubaliana katika mambo ya msingi katika mikakati yenu.Kwa mfano hivi chadema CUF ni kipi hasa kinachowaunganisha hata useme wajiunge nao,waipinge au waikosoe serikali ipi ambayo CUF ni mshiriki??.hUNA HATA HAJA YA KUZUNGUMZIA UBINAFSI WAKATI HUU,kwa maana kama ushirikiano wa hao unaowaita wapinzani ungeanzia hata kabla ya uchaguzi.sasa wanachotaka ni vyeo tu.kwani hao unaosema wakikosa vyeo ambavyo mmesema Chadema wanangangania hawawezi kuwa wapinzani??HONGERA MBOWE,HONGERA CHADEMA. Lazima waso wapinzani wa dhati watose.kwani wengine ni mamluki wa ccm na tunawafahamu msishirikiane nao.

    ReplyDelete
  6. kwani uwaziri kivuli una manufaa gani? wanapata priorities & facilities kama mawaziri kamili? au basi tu kuwa maarufu? Umaarufu nao una maslahi gani? mi naona ni kupoteza wakati kwa jambo lisilo na maana! hapendwi mtu hapa, pesa tu! hamjatizama komedi wameonyesha jamaa aliyeukosa uwaziri alivyommbomoa mganga wake!

    ReplyDelete
  7. KOMEDI NAO HAMNA CHOCHOTE NA HATUONGOZWI NA KOMEDI KUFANYA MAAMUZI TUNAONGOZO NA HOJA NA MALENGO YA KUFANYA KILE KITAKACHOTUFIKISHA KWENYE MALENGO KUSUDIWA,,KWANZA HAO COMEDI NI CCM...UPO???

    ReplyDelete
  8. HAKI YA NCHI IMEFIKIA MAHALI PABAYA. NI VILIO KILA MAHALI KILA KUNAPOKUCHWA. BIDHAA ZIMEPANDA KIASI CHA KUTISHA. NI KWELI ZIMEJAA MADUKANI NA SOKONI, LAKINI HAZIKAMATIKI. SHILLINGI IMESHUKA SANA THAMANI, NA UFISADI UMEKUWA JUU SANA BILA HATUA ZOZOTE KUCHUKULIWA DHIDI YA WAHUSIKA. CHADEMA, KAMA NGUZO KUU YA UPINZANI BUNGENI, INA WAJIBU MKUBWA NA MZITO KATIKA KUYASHUGHULIKIA HAYA ILI KUWAPA WATANZANIA UNAFUU WA MAISHA. NI MATUMAINI YANGU KWAMBA SASA SI WAKATI WA CHADEMA KUPIGA TENA SIASA. KWA WINGI AU UCHACHE HUOHUO MLIO NAO BUNGENI, MKIEGEMEA ZAIDI KATIKA KUINUA HALI YA KIMAISHA YA MTANZANIA PASIPO KUTAFUTA UMAARUFU, TUNATARAJIA NYIE KUWA MAKOMANDOO WA KUTUPIGANIA WATANZANIA TULIOCHOSHWA NA UGUMU WA MAISHA. JIVIKENI SILAHA ZOTE KUTUKOMBOA NA UCHUMI HUU USIO NA MFUMO WALA MUELEKEO. HONGERENI KWA KUFIKA HAPO MLIPOFIKA.
    NICHUKUE PIA NAFASI HII KUMPA BIG UP MHESHIMIWA MAKINDA. MWANZONI NILIANZA KUFADHAIKA NA MWENENDO WAKO BUNGENI, LAKINI KWA WIKI HII, NAANZA KUONA MATUMAINI YA KUUONA TENA ULE UJASIRI WAKO WA KAWAIDA. NA WEWE NIKUPE HONGERA.

    ReplyDelete
  9. Wanaotaka CHADEMA wajiunge na wenzao, wawaambie CUF, NCCR-mageuzi, TLP,nk wahamie CHADEMA ili wafikiriwe uwaziri kivuli

    ReplyDelete
  10. UKWELI HUWEZI KUSHILIKIANA NA MTU AMAYE MGUU NDANI MGUU NJE.SASA KAMA CHADEMA WATAWEZAJE KUSHILIKIANA NA VYAMA VINGINE WAKATI NISEHEMU YA CCM?HAITAWEZEKANA HATA KIDOGO NAWASHUKURU SANA CHADEMA KWA HUO UJASIRI WENU NI LAZIMA TUFE KIUME KAMA YESU ALIVYO KUFA MSALABANI.

    ReplyDelete
  11. Hongera Freeman kuwaumbua hao mamuluki wanaojiita wapinzani. sasa chapa kazi ili serikali iwe makini 2015 CHADEMA DAIMA

    ReplyDelete
  12. Hongereni Chadema, ni sawa tu mlivyofanya,kwani huwezi kuweka panya ndani ya gunia la mahindi.

    ReplyDelete
  13. Tena Mbowe, kusema kuwa eti CHADEMA itafikiria kuwashirikisha wengine, iwe mwisho hapa hapa kwenye magazeti. Utawshirikisha nani? Wale walioandika barua eti kutaka neno "rasmi" lifutwe kwenye kanuni walizoziweka wenyewe wakati kwa manuafaa yao? HAPANA! CHADEMA mnastahili hiki mlichokifanya, msigeuke jiwe la chumvi bure! Sasa ni utekelezaji, na si kurudi nyuma kufikiria mamluki waliofunga ndoa na CCM. NA wengine wakaingizwa kwenye mtego huo bila kujua. ALUUTA KONTNUUUUAAAA! Tuko nyuma yenu wapambanaji!

    ReplyDelete
  14. NYIE WOTE MNAOSEMA CHADEMA WAKO SAWA NYIE AKILI ZENU HAZIKO SAWA NI WAJINGA MNAUA DEMOKRASIA NA HAMNA NIA NJEMA NA CHADEMA NYIE NDIO MAMLUKI WA CCM MNATAKA CHADEMA IFE TARATIBU KAMA ILIVYOKUWA NCCR MAGEUZI NA TLP HAYA TUONE

    ReplyDelete
  15. Pole mtoa maoni hapo juu, tena pole sana. Una ndoto za ndaria kuota kuwa CHADEMA kitakufa. NCCR na TLP wakikusikia kuwatangazia tanzia ya kifo, hutapona wewe! Mrema ni mwenyekiti wa Kamati muhimu sana bungeni, Kafulila naye ndiye huyo rafiki kipenzi wa CUF. Sasa wamekufa wapi?. Acha uchuro wee. Kilichokwishakufa na kinasubiri mazishi ni CCM. Wao ndiyo wanaotapatapa kubadili kanuni kila kukicha ili kupunguza kazi na nguvu ya CHADEMA. Lakini wapi, Mbowe ndiyo huyo-o kawala chenga! Upo????

    ReplyDelete
  16. Mhhh! Yangu macho, na huu ndio mwisho wa taarifa ya habari tukutane tena hapo mwaka 2015 wakati CCM itakapoingia tena Ikulu kwa kosa dogo tu la kutokuona mbali!

    Tunaendelea na taarifa ya habari! Mwaka 2015 Novembar 30.

    Wapinzani wameshindwa kuunganisha nguvu zao kumsimamisha mgombea mmoja wa urais kutokana na tofauti kibao walizonazo hivyo basi kusababisha ccm kuunda serikali kwa kuwa kina asilimia 49 ya ushindi. Wapinzani hao hata waliposhauriwa kuunganisha nguvu zao baada ya matokeo kwani Chadema wana asilimia 27, CUF asilimia 15, n vyama vingine vidogo asilimia 9 hivyo kufanya jumla ya ushindi wao wa pamoja ni asilimia 51, lakini kutokana na kutokuelewana kulikopo tangu zamani vyama hivyo vimeshindwa kukaa pamoja na kuunda serikali. Hali hiyo imemlazimu Mwenyekiti wa kamati huru ya uchaguzi kuitangaza CCM kuwa ndio chama kitakachounda serikali pamoja na kushindwa kupata nusu ya kura zote kutokana na mabadiliko ya katiba yaliyopitishwa mwaka 2012.

    Na huu ndio mwisho wa taarifa ya habari.

    ReplyDelete
  17. CHADEMA msitishike na watabiri hawa. Cha msingi anzeni mapema kujiimarisha tangu mashina, vijiji hadi mijini. Kazi kubwa iko vijijini ambako wananchi bado wananfikiri CCM ya Nyerere ndiyo hii ya JK, Rostam, Lowassa, Makamba, & Co.

    ReplyDelete
  18. Hongera chadema kuachana na mamuluki hawa,

    Mbowe watanzania tunakupa onyo usijaribu hata kidogo kuingiza hawa mamuluki kwenye kambi yako!!!! NSSR MAGEUZI,TLP wameungana na CUF ambao ni ccm2 hivyo si wapinzani wa kweli.

    MUNGU IBARIKI CHADEMA AMBALO NI TUMAINI LA WANYONGE NDIO CHAMA IMARA CHEMA VIONGOZI NA WANACHAMA WALIOTAYARI KUFA KWA AJILI YA NCHI YAO!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete