Na Dunstan Bahai
USHINDI wa Mwanakombo Chicago, aliyegombea udiwani wa viti maalumu kupitia CCM na kushika nafasi ya pili, unadaiwa kuchakachuliwa na Katibu wa
CCM, mkoa wa Dar es Salaam, Kilumbe Ng’enda, kwa kile kinachodaiwa kuwa na maslahi binafsi.
Katika uchaguzi huo wa kura za maoni uliofanyika mwaka jana katika Jimbo la Temeke, Bi. Mwanakombo alipata kura 505 dhidi ya wagombea 18 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, huku Mariam Mtevu, akishika nafasi ya kwanza kwa kupata kura 609.
Baada ya kushinda katika uchaguzi huo, vikao vya kujadili na kupendekeza majina ya wagombea ngazi ya wilaya na mkoa, vilimpendekeza Mwanakombo kuwa mshindi halali wa nafasi hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, ulibaini kuwa kumekuwa na mapendekezo ya vikao hivyo ambapo Katibu wa CCM, Wilaya ya Temeke, Bw. Saad Kusilawe,alimwandikia Bi. Mwanakombo, barua ya uthibitisho kuwa ameteuliwa na CCM kuwa diwani wa viti maalumu.
Barua hiyo ilieleza kuwa “Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam katika kikao chake cha tarehe 9/08/2010, pamoja na mambo mengine, ilikuteua wewe kuwa Diwani wa Viti Maalum kutoka Jimbo la Temeke. Hongera sana.
“Uteuzi huu ni kwa ajili ya kukamilisha taratibu nyingine za Kiserikali kama vile ujazaji wa fomu wakati ukisubiri uteuzi wa Tume ya Uchaguzi.
“Ninakutakia kila la kheri katika kufanikisha majukumu yako,” ilieleza barua hiyo ambayo nakala yake ilipelekwa kwa Katibu wa CCM mkoa, Katibu wa UWT Mkoa na Katibu wa UVCCM wa wilaya hiyo.
Hata hivyo, uchunguzi wa kina uliofanywa na Majira, umegundua kuwa Bi. Mwanakombo, hakuridhika na hatua hiyo ya kuchakachuliwa jina lake na badala yake aliamua kumwandika Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba barua ya malalamiko akidai kuhujumiwa na Katibu wa CCM wa mkoa huo Kilumbe Ng’enda.
Katika barua hiyo, Mwanakombo anamtuhumu Bw. Ng’enda, kuwa alipewa “kitu kidogo” kwa lengo la kufanikisha azma hiyo ya kuchakachua jina lake na kumpa mtu mwingine.
Madai mengine ya Bi. Mwanakombo ni pamoja na Ng’enda kutumia ugomvi wa Bi. Mwanakombo na mumewe kumuengua katika nafasi hiyo.
Hata hivyo, Katibu Ng’enda alikanusha vikali tuhuma hizo akidai hakuna kitu kama hicho.
“Nataka kukueleza ukweli kwamba hakuna kitu kama hicho… sijahongwa fedha wala gari. Gari analosema Mwanakombo, limenunuliwa kihalali na mdogo wangu Abeid Shaban Ng’enda na vielelezo vipo.
“Ila mdogo wangu hakuwa na fedha za kutosha za kununulia gari hilo, hivyo aliniomba nizungumze na Chicago ili aweze kumkubalia alipe kwa awamu jambo ambalo Chicago alilikubali,” alisema Ng’enda.
Akifafanua zaidi, Ng’enda alisema kwamba tayari mdogo wake huyo ambaye anafanya shughuli zake binafsi huko Sinza, amelipa kiasi kikubwa cha fedha anazodaiwa na kwamba sasa kimebaki kiasi kidogo ambacho anatarajia kukilipa mwezi ujao.
“Hilo gari analo na hivi ninavyozungumza na wewe, anakaribia kumalizia kulipa deni hilo ambalo bado kidogo sana,” alisema bila kufafanua kiasi cha deni lililobaki.
Akizungumzia kuhusu Bi. Mwanakombo, kuondolewa jina lake, Ng’enda, alisema mgombea huyo hakuonewa bali alienguliwa kihalali na kwamba haoni sababu ya msingi ya kulalamikia uamuzi huo.
“Kuwa mshindi wa pili au wa kwanza, hakumfanyi mgombea kwamba ndio keshapita…unaweza kushinda katika kura za maoni, lakini vikao vya juu vikakuona hutoshi kuwa kiongozi, hivyo vikakuengua, hiyo ndio hali halisi ya kuenguliwa kwake.
”Kwa ufupi naomba ukanikariri kwamba nimesema huyu Mwanakombo, pamoja na kushinda katika kura za maoni, hatoshi kuwa kiongozi. Kuna sababu nyingi za kuenguliwa kwake hata nilivyoitwa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, niliwajibu hivyo kwamba hatoshi,” alisema Ng’enda bila kufafanua zaidi sababu za kutotosha kwake kuwa diwani.
Kwa upande wake Chicago, hakupenda kuzungumzia suala hilo.
Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Bw. John Guninita alisema hafahamu chochote kwani halijafika mezani kwake, licha ya kwamba vikao vyenye mamlaka ya kumuengua mlalamikaji huyo ni vya Kamati ya Utekelezaji ya UWT, Sekretarieti, Kamati ya Siasa na Halamashauri Kuu ya CCM, vyote vya mkoa.
No comments:
Post a Comment