11 February 2011

Majambazi yaua mfanyabiashara Arusha

Na Omari Moyo, Arusha

MAJAMBAZI wenye silaha wamemuua kwa risasi mfanyabaishara wa duka la jumla na kupora kiasi kikubwa cha fedha za mauzo ambazo
hazikujulikana mara moja.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Akilimali Mpwawa amemtaja marehemu kuwa ni, Felister Kayanga (25) mkazi wa Sokoni 1, katika mjini Arusha.

Alisema tukio hilo lilitokea saa 2:15 usiku wa kuamkia jana,  ambapo majambazi hao walivamia dukani kwa mfanyabiashara huyo na kumtaka kutoa fedha za mauzo na alipokaidi walimpiga risasi kifuani na kufa papo hapo.

Kamanda Mpwapwa alisema kwamba mwili wa merehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa, Mount Meru na upelelezi kuhusiana na tukio unaendelea na mpaka sasa  hakuna mtu yoyote anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.

Hata hivyo Kamanda Mpwapwa amewasihi wafanyabaishara kufunga biashara zao unapoingia usiku, kwani hali hiyo inaweza kuchangia kutoa ushawishi kwa majambazi.

Wakati huo huo, jeshi la polisi mkoani Arusha limekamata magari mawili yanayosadikiwa ni ya wizi yakiwa yamefichwa kwenye nyumba ya rubani mmoja.

Magari hayo yalikamatwa eneo la Sombetini, Arusha ni aina ya Toyota Corona na Corrola, yenye namba za usajili T 170 AUL ambalo linadaiwa kuporwa eneo la Sakina Februari 4, mwaka huu ambalo linadaiwa kubadilishwa namba na kuwa T 829 AZB na Toyota Corona lililokuwa na namba za usajili T 225 ABC ambalo liliporwa Februari 9, mwaka huu  eneo la Sakina, kubadilishwa namba za usajili na kuwa T 316 BEE.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha,  mtoto wa Rubani huyo ni miongoni mwa watuhumiwa waoshikiliwa kwa tuhuma za wizi wa magari hayo.

No comments:

Post a Comment