ROME, Italia
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), limemfungia kucheza mechi nne kiungo wa AC Milan, Gennaro Gattuso baada ya kumtia hatiani
kukwaruzana na kocha msaidizi wa Tottenham Spurs, Joe Jordan wiki iliyopita katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
Kabla ya adhabu hiyo mchezaji huyo tayari alishafungiwa mechi ya marudiano, baada ya kutolewa nje ya uwanja wakati wa mechi hiyo.
Kufungiwa kwa mchezaji huyo, ina maana kwamba Gattuso hatakuwemo uwanjani wakati wa mechi za Klabu Bingwa Ulaya, hadi mechi ya fainali endapo AC Milan itafanikiwa kufika hatua hiyo na klabu hiyo ililieleza Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), kwamba mchezaji huyo hatachukua hatua zozote kuhusu adhabu hiyo na wala haitakata rufani.
Gattuso alionekana kuchanganyikiwa, wakati timu yake ilipofungwa bao 1-0 na Tottenham kwenye Uwanja wa San Siro, ambalo liliwekwa kimiani na Peter Crouch baada ya wachezaji hao wawili kugongana.
Mchezaji huyo pia alikwaruzana na Jordan, nje ya mstari wa uwanja kabla ya kumkaba shingo mchezaji huyo wa zamani wa timu ya AC Milan na baada ya mchezo huo, Muitaliano huyo alimvaa tena Jordan kabla ya kumpiga singi kocha huyo mwenye umri wa miaka 59.
Hata hivyo wiki iliyopita Gattuso, aliomba radhi kwa kitendo chake hicho lakini akasema alikuwa akichokozwa na kocha huyo, muda wote wakati wa mchezo huo.
No comments:
Post a Comment