28 January 2011

Watalaamu wa ndani wapewe upendeleo-Mwakyembe

Na Agnes Mwaijega

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa mwito kwa taasisi za serikali na sekta binafsi nchini kutoa fursa za upendeleo kwa
wataalamu wa kampuni za ndani katika sekta ya ujenzi.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli katika sherehe ya maadhimisho ya miaka 25 ya Chama Cha Wahandisi nchini (ACET), Dkt. Mwakyembe alisema katika upendeleo huo watalaamu wa kampuni za nje wawe wasaidizi.

Aliwataka wataalamu wa sekta hiyo kuzingatia maadili na viwango vinavyostahili katika utendaji wao.

Alisema ACET ni mdau mkubwa wa serikali na atahakikisha wanaitumia katika shughuli zake za ujenzi. 

Aliongeza kuwa kwa sababu taifa linahitaji kuwa na maendeleo makubwa katika sekta hii, serikali itahakikisha inawatumia wataalamu wa ndani kwa sababu wao wanaielewa vizuri nchi yetu na matatizo yanayoikabili na namna ya kuyashughulikia.

"Ni ukweli uliowazi na usiopingika kwamba hakuna taifa lolote duniani katika nchi zilizoendelea linalotegemea wataalamu wa nje kwa maendeleo yake," alisema Dkt. Mwakyembe.

Pia alisema kuwatumia wataalamu wa ndani kutapunguza gharama kubwa zinazotumika kuwalipa wa nje na itasaidia kukuza sekta zingine za uchumi.

"Hakuna sababu ya miradi inayogharamiwa na serikali kwa kutumia kodi za wananchi kukabidhiwa kwa kampuni za nje," alisema.

Alisisitiza kuwa ili kampuni za ndani ziweze kuleta ushindani lazima ziwe na mikakati ya kujiendeleza ili iweze kukua.

Dkt. Mwakyembe alisema idadi ya wahandisi washauri nchini ni ndogo na ndiyo maana maendeleo yetu katika baadhi ya maeneo siyo endelevu.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Dkt. Mwakyembe alisema serikali itahakikisha inajenga vyuo vingine na kuvipanua vilivyopo ili viweze kutoa wataalamu wengi zaidi.

1 comment:

  1. Tatizo la kuwatumia wahandisi wazawa ni la muda mrefu kwani serikali imeshindwa kuandaa mikakati maalumu ya kufanya hivyo. Mwakyembe anaahidi kuwa serikali itahakikisha inajenga vyuo vingi ili kukabiliana na tatizo hili. Nadhani tatizo si idadi ya wahandisi bali ni mpango endelevu wa kuwatumia. Acet inapaswa kutoa mapendekezo kuhusu namna ambavyo serikali inaweza kusaidia kukuza makampuni ya wahandisi wazawa ili yaweze kufanya kazi nyingi na kuepukana na kutegemea wageni ambao si lazima kwamba ni wazuri zaidi ya wazawa.

    ReplyDelete