14 January 2011

Wakamatwa wakitoroshea mbolea Burundi

Na Sammy Kisika, Mpanda

JESHI la Polisi wilayani Mpanda, mkoani Rukwa linamshikilia Bw. Kain Buchumi (27) raia wa Burundi pamoja na Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Bw. Hamidu Sungura (34) kwa tuhuma za kukamatwa na mifuko 195 ya mbolea ya
ruzuku wakiwa na lengo la kuitorosha kwenda Burundi kwa njia ya magendo.

Watuhumiwa hao walikamatwa hapo juzi saa 6:30 mchana katika kijiji cha Isanjandugu Tarafa ya Nsimbo nyumbani kwa Katibu wa kamati ya ugawaji wa mbolea za Ruzuku wa kijiji hicho, aliyejulikana kwa jina moja tu la Bw. Sabasi.

Walikamatwa na mbolea aina ya Urea mifuko 150 na nyingine aina ya Mijingu mifuko 45 ikiwa tayari imepakiwa kwenye gari aina ya Fuso namba T590 ALL, mali ya Bw. Buchumi.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na taarifa zilizolifikia jeshi hilo pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa Bw. Buchumi anashirikiana na baadhi ya viongozi wanaogawa mbolea za ruzuku kutorosha mbolea hizo nchi jirani.

Katika tukio hilo, raia huyo wa Burundi alijaribu kutoa rushwa ya sh. 150,000 pasipo kujua kuwa waliomkamata walikuwa ni maofisa wa TAKUKURU na polisi, hali iliyosababisha kumkamata na kumuweka chini ya ulinzi kwa kosa jingine, la kujaribu kushawishi na kutoa rushwa.

Baada ya kubaini kuwa aliokuwa akitaka kuwahonga ni maofisa wa TAKUKURU na polisi alitaharuki na kutaka kukimbia, na baadaye alianza kukiri kuwa ni kweli alikuwa na mpango wa kuisafirisha mbolea hiyo kuipeleka Burundi, na hivyo kuwaomba msamaha.

Watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani jana na wamerudishwa rumande wa kukuosa dhamana.

Hivi karibuni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Bw. Emmanuel Kalobero aliunda tume ya kuchunguza mwenendo wa ugawaji wa mbolea za ruzuku ambazo zinadaiwa kuwa haziwafikii walengwa, hali inayosababisha malalamiko
kwa wakulima.

Miongoni mwa malalamiko ya wananchi wamelalamikia baadhi ya kamati ya pembejeo pamoja na mawakala wao wanadaiwa kutumia majina hewa kwa kutoa vocha na pia kuwabadilishia wananchi aina ya mbolea inayokuwa imeorodheshwa kwenye vocha, hasa mbolea aina ya Urea ambayo bei yake ni kubwa.

Mkoa wa Rukwa katika msimu uliopita ulikumbwa na kashfa ya mawakala wake na baadhi ya watendaji ambapo inadaiwa zaidi ya sh. 6.5 bilioni za fedha za pembejeo zilipotea katika mazingira kama hayo, huku wakulima wenyewe wakikosa pembejeo hizo.

2 comments:

  1. Tatizo la hii nchi ni kwamba mfumo mzima umeoza toka juu hadi chini kabisa. Kwa mfumo huu, sahau maendeleo Tanzania; hata kama kungekuwa na mipango, semina elekezi, kaulimbiu, mikakati, n.k. mizuri namna gani - hayo ni ya kwenye makaratasi tu lakini utendaji sifuri.

    Hebu fikiria mkoa mmoja tu (Rukwa), kwa mwaka mmoja tu (2010), ka-item kamoja tu (pembejeo), watendaji wachache tu (mawakala) zimepotea jumla ya T.Shs. bilioni 6.5. Hivi kwa nchi nzima (mikoa, idara, wizara, n.k zote), miaka yote (fanya kama 15 hivi), items zote (madini, misitu, uvuvi, mifugo, mikataba, manunuzi ya umama, ujenzi, n.k.), watendaji wote (kuanzia kiongozi mkuu hadi mimi/wewe) zimepotea bilions/trilions ngapi? Halafu tunasema Tz ni maskini? Hapana! Hii ni kama kujaribu kumlaani Mungu - hatutaweza!

    Napendekeza Katiba mpya ambayo tunakusudia kuiunda iweke bayana mfujaji/mwizi yeyote wa mali yoyote ya umma (hata kama ni Sh. 1) adhabu yake moja kwa moja iwe risasi moja kisogoni na hakuna cha rais au nani kuweka saini. Mahakama ikishathibitisha kosa na rufaa ikithibitisha hivyo adhabu itekelezwe mara moja. Wachina tunaoasifia leo hii kwa maendeleo wame/wanafanya hivyo kwa wezi wote wa mali ya umma. Rushwa ni mbaya.

    ReplyDelete
  2. HI INACHEKESHA NA INASKITISHA SANA

    ReplyDelete