28 January 2011

Sumaye akerwa uchumi kuacha kando maskini

*Asema ni hatari kwa utulivu wa nchi

Na Tumaini Makene

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Bw. Frederick Sumaye amesema kuwa takwimu za ukuaji wa uchumi ambazo hazijidhihirishi katika hali
chanya miongoni mwa wananchi wengi maskini hauna maana, kwani unaweza kuwa unakua lakini uko mikononi mwa mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu wachache wabinafsi.

Amesema kuwa watu maskini wanapoachwa pembeni huku ikisemwa 'shauri yao' kutokana na watu wenye mamlaka kuendekeza ubinafsi badala ya kutumikia umma wa Watanzania, ni hatari kwa utulivu wa nchi.

Bw. Sumaye, aliyasema hayo jana katika mahafali ya kuwaaga wanafunzi wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Pungu, akiwaasa vijana hao kujiandaa kuwa watumishi wa umma wa Watanzania maskini wanaolipia masomo yao kupitia kodi.

Huku akishangiliwa na wanafunzi, waalimu, wafanyakazi na wageni waalikwa, Bw. Sumaye alisema kuwa moyo wa upendo wa watu wanaonufaika na jasho la walipa kodi maskini wa Tanzania kuutumikia umma unazidi kupotea badala yake 'unajengeka moyo wa ubinafsi'.

"Sijui wangapi wanajua umuhimu wa mahafali haya ya leo...ukiwauliza vijana watasema majibu tofauti...wapo watakaosema wanafurahi kumaliza kuachana na mwalimu fulani, wapo watakosema kuwa wameachana na somo fulani...hivi kuna mtu hata mmoja amefikiria baada ya hapa itakuwaje.

"Ni kipindi cha kuonesha mavuno baada ya shamba, tunatumaini kuwa wahitimu wa leo wanayo mavuno ya kuonesha mara fursa itakapofika...lakini ni vyema mkajua kuwa kuhitimu kwako maana yake unategemewa kuwa kioo au msaada mkubwa kwa jamii inayokuzunguka.

"Unapaswa kutambua kuwa kuna Watanzania wana maisha magumu kiasi kwamba hawana viatu vya kusitiri miguu yao, chakula chao cha siku ni shida. Wengi wakiulizwa nani kawasaidia hapo walipofika mtasema ni serikali...lakini ukweli ni kuwa ni walipa kodi maskini, wamejitoa kuwasomesha ili msaidie kutatua matatizo yao," alisema Bw. Sumaye na kuongeza.

"Watanzania wanatakiwa watoke katika umaskini, itakuwa ni kosa tukijijali wenyewe na kuisahau jamii...siku hizi moyo wa upendo wa kutumikia umma unapungua, badala yake unajengeka moyo wa ubinafsi sana, watu maskini wanaachwa pembeni ikisemwa kuwa ni shauri yao.

"Hali hii ni hatari sana kwa utulivu wa nchi yetu...hata kelele hizi zinazopigwa juu ya ufisadi, wizi, rushwa, ushirikina, mauaji ya kutisha ni matunda ya ubinafsi, moyo usiojali wengine. Ni kweli kuwa uchumi wa nchi yetu unakua vizuri, lakini ukuaji wa uchumi uonekane katika hali chanya ya wananchi walio wengi."

Bw. Sumaye ambaye ni waziri mkuu mstaafu pekee mpaka sasa aliyewahi kutumikia vipindi viwili vya miaka mitano mfululizo wakati wa serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, alisema kuwa uchumi unaweza kukua lakini ukawa mikononi mwa mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu wachache.

Alisema kimsingi hapigi vita utajiri, wala kuwaonea wivu wenye utajiri, bali anawaonea huruma wenye maisha duni, waliojitoa maisha yao, kwa njia ya kulipa kodi, kuwasaidia baadhi ya watu, hususan wenye mamlaka hapo walipo.

Alisema Watanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya maisha magumu, umaskini uliokithiri, ujambazi, rushwa, ufisadi unaoikumba jamii nzima na kuiathiri, hasa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa.

"Ukuaji wa uchumi unaweza kuwepo kwa kundi la watu wachache au mtu mmoja...ni hatari...tiba ni kuwatumikia wananchi kwanza kabla ya nafsi zetu...tuwe na moyo wa upendo kutumikia binadamu wenzako kwanza...umuhimu wako utakuja tu ukijitoa kutumikia wenzako hasa wenye hali duni.

"Kuna msemo mmoja wa Kiingereza unasema it is nice to be important but it is more important to be nice (ni vizuri kuwa mtu muhimu lakini ni muhimu sana kuwa mtu mwema). Sipigi vita utajiri la hasha, siwaonei wivu wenye utajiri wao, nawaonea huruma wenye hali duni waliojitoa maisha yao," alisema Bw. Sumaye.

Akiwatakia kila la heri na yote mema ya maisha wahitimu kwa ajili ya kuwatumikia wananchi huko waendako, Bw. Sumaye aliipongeza serikali kwa kujitahidi kuboresha sekta ya elimu, ambayo alisema ndiyo nyezo ya kupambana katika ulimwengu usiokuwa na huruma wa maendeleo ya sayansi.

Aliongeza kuwa shule ni sawa na karakana ya maisha kwa mwanadamu, ikimsaidia kujichongea mitambo ya kuendesha maisha yake mwenyewe, ingawa itategemea anaamua kujichongea mtambo wa aina gani anapokuwa amepata fursa ya kuwa darasani kusoma.

"Naipongeza serikali kwa kutoa kipaumbele kwa elimu kwa mafanikio yaliyofikiwa...elimu ni tofauti kabisa na huduma zingine za jamii...ni uzima wa maisha yenye maana kwako na jamii inayokuzunguka...umuhimu wake hauna mjadala, nchi iliyo nyuma kielimu haiwezi kushindana...

"Ni muhimu tukajielekeza kutoa elimu bora badala ya bora elimu ili kushindana katika ulimwengu wa utandawazi, serikali ihakikishe kuwa elimu inayotolewa inakidhi viwango vinavyokubalika kimataifa. Tusitengeneze viwango vyetu wenyewe kujiridhisha.

"Imekuwa kawaida sasa kuona katika taarifa za habari watoto wetu wamerudia mtindo wa kukaa sakafuni, kwenye vumbi huku wakiandikia magotini au kwenye migongo ya wenzao. Hapo hatutengenezi elimu ya viwango vya kimataifa, bali vya kwetu sisi wenyewe...haya ni mambo ya kuaibisha kabisa elimu yetu, ni vyema serikali ikayafanyia kazi.

"Mtaalamu mmoja alisema kama unafikiri elimu ni ghali jaribu ujinga...walimu Nyerere alikuwa akimfananisha mtu aliyekwenda chuo kikuu sawa na mtu aliyepewa chakula chote cha kijiji ili aende akatafute chakula cha kutosha kijiji cha jirani kisha alete...msiwasaliti Watanzania," alisema Bw. Sumaye.

Mapema Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu, Bw. Rukonge Mweru alisema kuwa moja ya changamoto wanazokabiliana nazo ni 'uvamizi' wa mipaka ya shule, hali ambayo mbali ya kumega eneo la shule pia inatishia ufanisi katika masuala kama vile kilimo, kama ilivyokuwa enzi za nyuma na kuhatarisha usalama na mali za wanafunzi na shule.

Wanafunzi wahitimu katika risala yao walirudia kero hizo, ikiwemo hiyo ya uvamizi wa eneo la shule, tatizo la maji, vitendea kazi (kama vile vitabu, vifaa vya maabara), uchakavu wa majengo na upungufu wa dawa katika zahanati ya shule.

19 comments:

  1. mheshimiwa mstaafu ni kweli hayo maneno yanatoka moyoni mwako? hongera sana kwa kuyajua hayo baada ya kutoka madarakani. au ulikuwa unayajua hayo kabla? hongera sana. hongera sana.hongera sana.

    ReplyDelete
  2. Hivi unampa hongera ya nini huyu,anazungumzia UFISADI looo maajabu na vituko vya wanasiasa wa Bongo,huyu mzee alikuwa Waziri Mkuu enzi ya Mkapa na ndio awamu iliyoleta balaa katika nchi hii.UFISADI WA EPA UMETOKEA HUKO,RELI,RADA,NDEGE YA RAIS,BANDARI,MADINI,MABENKI NA KILA AINA YA BALAA IMETOKEA KATIKA AWAMU YAKE NA MKAPA SASA LEO ANATUAMBIA NINI? Kikwete una kazi kubwa maana hawa vigogo uliowaacha ndio wanakutupa mkono na kukuzunguka. SUMAYE TUBU KWA MUNGU NA WAOMBE RADHI WANANCHI MLILOLIFANYA WEWE NA MKAPA NDIO MATOKEO YA VURUGU ZA HAPA NCHINI KWA SASA.

    ReplyDelete
  3. Ee Bwana wee,

    Nyie kwenye enzi ya uongozi wenu mliuza raslimali za nje kama vile hakuna kesho: si tu mashirika ya uma bali pia mali asili na chochote kile - hata nyumba za serikali. Mliwapuuza waalimu, madaktari, wauguzi na hata wakulima, mkajinufaisha nyie wenyewe, mkatajirika haraka haraka, sasa unatuambia nini? Hebu Frederick taja mali ulizokuwa nazo wakati hujawa waziri na ulizokuwa nazo ulipoacha uwaziri mkuu mwaka 2005. Na kama utakuwa mkweli kama unavyojifanya tutakuuliza umezipataje?

    ReplyDelete
  4. Ni kweli uchumi umewaacha kando maskini lakini hii inatokana na misingi wewe na wenzio mliyoijenga yenye kujenga matabaka. Bwana Sumaye usidhani wananchi hawakumbuki mliyofanya, na kama sasa unatafuta cheap popularity umenoa. Hukumu yako itakuwa ile ile ya wale walioifikisha hii nchi hapa ilipo.

    ReplyDelete
  5. Huyu mzee hawezi kusema haya kwa ujasiri kama alikuwa fisadi.

    Naanza kuamini magazeti yaliyokuwa yanamwandama yalikuwa ni propaganda za siasa. Kwani hata leo magazeti ya chama fulani hayana mvuto hata wa kuyasoma. Wao kuandika habari za kupakana matope ni biashara yao. Laiti wasingepata ruzuku, wangefunga virago.

    Hongera Sumaye kwa kutoa elimu ya uraia.

    ReplyDelete
  6. Maadam kaliona hilo na kulipatia tafakari basi nawajibike kama mtanzania na mwenye nafasi kubwa kuwasilisha na kusimamia katika ngazi husika na sio kusema tu na kukaa kimywa ninamini bado anayo nafasi ya kutetea hoja yake kwa vintendo.

    ReplyDelete
  7. USEMAYO NI KWELI JASHO LETU WANALOKULA IPO SIKU LITAWAUJUMU

    ReplyDelete
  8. Hivi wewe unayesema magazeti yalikuwa yakimuandama sumaye,hivi huji enzi yeye akiwa Waziri Mkuu wa nchi ufisadi ndipo uliposhika kasi? nani kauza Reli,nani kanunua ndege ya Rais kwa bei ya ajabu,nani aliuza ATC,nani kabinafsisha mashirika ya umma kwa bei chee,nani kanunua rada kwa bei ya ajabu hata wazungu wenyewe wakashangaa,nani kauza ardhi yenye madini kwa bei chee,nani kakodisha bandari kwa bei ya kutupwa na licha ya utendaji wa hovyo mkataba ukaongezwa kabla hata wa kwanza haujaisha kinyume na mkataba unavyoonyesha ni madudu mengi yamefanywa na awamu ya kina sumaye na mkapa ambayo sasa yanaleta tabu kwa wananchi

    ReplyDelete
  9. Bila aibu wala haya ni kweli Sumaye unawaambia Watanzania haya? ama kweli wanasiasa wengi wa nchi hii ni wasanii

    ReplyDelete
  10. Kilichobaki tu Tz ni kuwaondoa kikwete, Makamba na mafia wote wa ccm !!! CCM must now go. Afrika inabadilika, madikteta tu kama waliopo CCM bado hawaoni. Angalia kinachotokea Tunisia, Misri, Libya, etc, etct !!!!! Watanzania amkeni tuichukue nchi yetu !!!!!!

    Abdallaha Juma

    ReplyDelete
  11. huyu jamaa hana lolote anajipendekeza sasa kwa wapinzani chadema napia kujitaka kujisafisha ili aonekane msafi kwanza ni fisadi number one halafu ni mnafiki mwizi ndumi la kuwili ameiba mali za serekali nyingi magari na kujilimbikizia viwanja vya serekali mikocheni na pugu sasa leo hii anasema haya hakumbuki aliko toka wewe wacha usani wako huo tushakujuwa unataka ruaisi lakini hutopata mwizi mkubwa wewe fisadi

    ReplyDelete
  12. jamani mbona mnamnyanyasa huyu mzee? au kwa sababu ni wa dini fulani?

    ReplyDelete
  13. Pumbavu mmoja wewe unayesema habari ya dini hapo juu,hivi una akili timamu kweli au mvivu wa kusoma ya waliochangia maoni? sishangai maana kuna mzungu mmoja alisema ukitaka kumpatia mtu mweusi mpe makaratasi mengi au habari nyingi asome,akaendelea kusema wengi na pengine asilimia themanini (80%) ni wavivu wa kusoma na hili jambo ni kweli wa Watanzania,wavivu wa kufikiri na wavivu wa kusoma,ndio maana hata wengine hapo kwenye kuchangia simple tu wanasema tufanye kama Tunisia na Misri lakini hawajui lolote kuhusu viongozi hao wanaokataliwa na wananchi na taarifa za viongozi hao,utakuta tu mtu kirahisi anasema tufanye kama Tunisia na Misri,kuweni serious kutafakari kitu na kutolea maoni

    ReplyDelete
  14. Hawa akina sumaye na mkapa wasamehewe tu kwa sababu ndio wametufikisha hapa. Huyu jamaa yao nae anayeimba udini anamawazo finyu. Kama mwalimu Nyerere alivyosema kwamba ukiona kiongozi wa serikali anaanza kusema udini! udini! ujue huyo kafilisika kimawazo. Ndipo walivyofilisikam hawa akina kikwete na makamba. MUNGU UWASAMEHE KWA KUWA HAWJUI WATENDALO

    ReplyDelete
  15. Kelele pekee haziwezi kumkomboa Mtanzania.Matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno.Tunaweza kuwa wasikilizaji wa mihadhara ya wezi wastaafu ambao baada ya kutuhujumu kupindukia sasa wanadai wanatuhurumia.Chaguo ni letu: kuendelea kuumia huku tukighilibiwa na "busara" za watu kama Sumaye (ambaye laiti sheria ingefuata mkondo angezungumza haya akiwa Segerea) au tukusanye nguvu zetu kama wenzetu wa Tunisia na kujikomboa.Hakuna short cut katika kuung'oa mfumo dhalimu.

    ReplyDelete
  16. Sumaye anapata wapi maneno hayo wakati ndio waliolifilisi sana Taifa letu? Wasubiri tu vijana watakapoingia mitaani kama Tunisia na Egypt.

    ReplyDelete
  17. TANZANIA TUSIWE KISIWA...NGUVU YA WATU (PEOPLE'S POWER)TU NDIO ITAWEZA KUIKOMBOA NCHI HII. HAKUNA VIKAO WALA TUME WALA MUAFAKA WA AINA YOYOTE ILE. WATANZANIA TUACHE UOGA TUTOKE BARABARANI TUDAI HAKI YETU. BILA KUONYESHA MFANO KWA KUUTOA UONGOZO MADARAKANI HATUTAKUWA NA SERIKALI INAYOOGOPA WANANCHI. (endelea chini)

    ReplyDelete
  18. SERIKALI INATAKIWA IOGOPE WANANCHI KWANI WAO NDIO WAMEIWEKA MADARAKANI. CCM INACHOFANYA NI KWAMBA HAIJALI NA WALA HAIMUANGALII MWANANCHI WA KAWAIDA. UCHUMI UMEKUWA...KWA ROSTAM AZIZ NA MAFISADI WENZAKE TU. MWANANCHI WA KAWAIDA ANAZIDI KUPOROMOKA NA KUFA. TUACHE UNAFIKI WA KUPIGA WEZI WA KUKU NA KUWAUWA WAKATI WEZI WA MABILIONI YA KODI ZETU WANAINULIWA MIKONO JUU WAKATI WA KAMPENI KUWA NDIO VIONGOZI WAZURI NA SHUPAVU.

    ReplyDelete
  19. Nimependa sana huyo aliyetoa maoni hapo juu. inanikumbusha mama yangu aliyemwagiwa sufuria lake la wali akiuza sokoni eti kwa sababu hakulia ushuru.Ushuru wanaolipa na kodi nyingine za wananchi kwa miaka nenda rudi anakuja kupewa Dowans (Rostam) kwa siku moja tu. Tuwe na hasira na hawa watu jamani!!!!!

    ReplyDelete