Na Zahoro Mlanzi
HALI ndani ya Klabu ya Yanga, inaonekana kutengemaa baada ya uongozi wa klabu hiyo kuwapoza wachezaji wao waliokuwa wamegoma kwa kuwapa posho za sikukuu ya Krismasi.Wachezaji hao walimgomea Kocha wao, Kostadin Papic
kufanya mazoezi mpaka fedha zao za usajili zinazodaiwa kufikia sh. milioni 70, watakapolipwa.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu, alisema wamemalizana na wachezaji hao kwa kuingia makubaliano maalum ikiwa ni pamoja na kuanza kuwapa posho za sikukuu ya Krismasi.
"Kweli jana (juzi) jioni Kamati ya Utendaji ilikutana na wachezaji wote kujadili malalamiko yao, kimsingi tulifikia muafaka kwa kuanza kuwalipa posho kwa ajili ya sikukuu ya Krismasi," alisema na kuongeza;
"Baada ya kuwapa fedha hizo walikubali kuendelea na programu za kawaida za mazoezi na baada ya sikukuu kupita, ndipo zile fedha wanazodai zitaanza kutolewa."
Mgomo huo ulianza Ijumaa saa tisa Alasiri kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ambapo wachezaji hao walifika kama kawaida uwanjani, lakini baada ya Papic kupuliza filimbi ya kuwaita uwanjani, waligoma kuingia.
Papic alipojaribu kuuliza kulikoni, ndipo walipomwambia kwamba, wamechoka na ahadi zisizotimizwa kutoka kwa viongozi wao kuhusu fedha za usajili.
No comments:
Post a Comment