Na Addolph Bruno
KIUNGO mpya wa Majimaji, Ulimboka Mwakingwe amewataka wachezaji na vongozi wa klabu hiyo kushirikiana ili waweze kufanya vizuri mzunguko wa pili Ligi Kuu Tanzania Bara.Ulimboka ambaye ameichezea Simba kwa muda mrefu ni
miongoni mwa wachezaji wanne, waliosajiliwa na Majimaji katika dirisha dogo la usajili ili kuimarisha kikosi hicho.
Akizungumza kwa simu jana akiwa Morogoro anakoishi, mchezaji huyo alisema ligi ya msimu huu ni ngumu lakini kutokana na uzoefu wake anaona ushirikiano wa wachezaji na viongozi ni ushindi tosha.
"Nilibahatika kushuhudia baadhi ya mechi za mzunguko wa kwanza niliona kuna kazi ngumu msimu huu, nilichokigundua kila timu imejiandaa vizuri hivyo naomba ushirikiano tu wa wachezaji na viongozi," alisema.
Alisema anatarajia kuondoka kesho kwenda Ruvuma kujiunga na timu hiyo tayari kwa kuanza mazoezi na baadaye kwenda Msumbiji kwa ajili ya kambi itakayoanza Desemba 28, mwaka huu.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa klabu hiyo Ahamed Dzumba alisema timu hiyo inatarajia kucheza mechi tatu za kirafiki kujiandaa na mzunguko wa pili, dhidi ya timu ya Combine ya Songea na michezo mingine itacheza na Nampula wakiwa Msumbiji.
No comments:
Post a Comment