Na Grace Michael
WANANCHI wa Kata za Kitunda, Msongola, Kivule na Chanika ambao wanatumia barabara ya kutoka Mombasa kupitia Moshi baa, Dar es Salaam wameelekeza kilio chao kwa Waziri wa Miundombinu, Dkt. John Magufuli wakimuomba kuangalia kilichokwamisha
ujenzi wa barabara hiyo inayotakiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mbali na kuangalia kilichokwamisha pia wamemuomba kuitembelea barabara hiyo ambayo iko chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kuona namna wananchi wanavyopata kero ya usafiri kutokana na ubovu ilionao.
Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema kuwa barabara hiyo imekuwa ikitengewa bajeti ya ujenzi lakini ujenzi huo umekwama kutokana na madai ya wenye vibanda vilivyopo pembeni mwa barabara hiyo kutolipwa fidia.
"Wananchi tunaotumia barabara hii tunaseka sana hasa wakati wa mvua ambao sasa tunalazimika kutembea umbali mrefu kwa kuwa magari yote hushindwa kupita barabara hii na cha kushangaza bajeti ya ujenzi wa barabara hii ipo na Rais Kikwete katika kampeni zake alitueleza kuwa fedha zipo, hivyo tunamuomba Dkt. Magufuli aangalie palipokwama ili barabara hii ianze kujengwa," alisema mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Bi. Hawa.
Wananchi hao pia hawakusita kusema kuwa hawana shaka na utendaji wa Dkt. Magufuli na katika hilo wanaamini kuwa kilio chao kitashughulikiwa na hatimaye nao kuondokana na kero hiyo ambayo imewakabili kwa kipindi kirefu.
Ujenzi wa barabara hiyo umekwamishwa na madai ya fidia za waliojenga kando kando ya barabara hiyo ambapo Manispaa ya Ilala na TANROADS wanatupia mpira kuhusu suala hilo na kwa upande wa Manispaa ilisema kuwa haina uwezo wa kulipa fidia hizo na kinachotakiwa ni Serikali Kuu kuingilia kati huku TANROADS wakidai kuwa bajeti iliyopo ni ya ujenzi wa barabara tu na si fidia.
Kutokana na mkanganyiko huo, wananchi wamebaki wakighubikwa na kero hiyo huku kukiwa hakuna ufumbuzi wa aina yoyote hali iliyowalazimu kumuomba Dkt. Magufuli kuitembelea barabara hiyo na kuona namna ya kuwasaidia katika kutatua kero hiyo.
No comments:
Post a Comment