06 December 2010

Vita ya umeya CCM kuinufaisha CHADEMA

Na Charles Mwakipesile, Mbeya

VITA ya uteuzi wa mgombea wa CCM kuwania nafasi ya umeya Jiji la Mbeya tayari imeibua makundi ndani ya chama hicho na hivyo kuibua wasiwasi kuwa huenda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinanufaika na mpasuko huo na kuibuka
mshindi.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa mkoani hapo wamebashiri kuwa chama hicho pinzani kinaweza kuibuka na ushindi katika nafasi hiyo kutokana na mvutano mkubwa kati ya wagombea wawili wa CCM, aliyekuwa meya kipindi kilichopita, Bw. Athanas Kapunga na Diwani wa Kata ya Isanga, Shekhe Dul Mohamed.

Mvutano huo unadaiwa ulianza mapema na kusababisha  wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Mbeya kuamua kuwapa wagombea hao alama B kila mmoja.

Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM ndani ya mkoa ambaye hakutaka kutaja jina, alisema kuwa maana halisi ya kutolewa kwa alama hizo ni kuwa wana sifa sawa za kuteuliwa kushika nafasi hiyo nyeti, hatua inayoongeza mvutano baina yao.

Uchunguzi uliofanywa na Majira miongoni mwa madiwani wa vyama vyote kwa nyakati tofauti, umebaini kuwa kutokana na mpasuko huo lolote laweza kutokea kwa kuwa wagombea   hao wamekwishanza kampeni kwa madiwani wa upinzani ili kuwasaidia.

Wakati CCM inajivunia kwa kuwa na madiwani wapiga kura  29, CHADEMA ambayo inaungwa mkono na vyama vingine vya upinzani, inategemea kuunganisha nguvu na kufikia madiwani 20, huku ikiwa imesimamisha mfanyabiashara wa jijini hapa, Bw. Boyd Mwabulanga, hali ambayo inafanya mchakato huyo kuwa mgumu wa kihistoria.

Hata hivyo wasiwasi ulioibuka ni iwapo CCM itateua  mgombea asiye chagua la madiwani wengi wa chama hicho  na hivyo kusababisha kupata adhabu iliyopewa katika uchaguzi wa mbunge wa jimbo hilo ambapo wana-CCM wa Jiji la Mbeya waliamua kumpatia kura za kihistoria mgombea wa CHADEMA, Bw. Joseph Mbilinyi.

Nafasi inayotegemewa na CHADEMA ni kupata kura za madiwani ambao wataonesha wazi kutoridhika na uteuzi wa mmojawapo wa wagombea.

Kundi linalompiga vita meya anayetetea nafasi yake limeonakana dhahiri kuwa ni lile linajiita la mabadiliko ambalo limekuwa likitamba kuwa kama lilivyofanya kwa mbunge ndivyo litakavyofanya kwa diwani huyo ambaye amekuwa katika nafasi ya umeya kwa zaidi ya miaka 10.

1 comment:

  1. Upendeleo wa kutaka kuchaguana ndio unawamaliza ccm na mtakwisha kwa kuendekeza hilo hamtaki kujifunza kutokana na makosa, chagueni mtu asiyeuzika muone itakavyokuwa CHADEMA OYEEEE

    ReplyDelete