Na Peter Mwenda
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeonya tabia ya wenye makampuni ya simu na wananchi kuvunja kanuni ya utunzaji wa siri za mawasiliano binafsi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi kuchapishwa katika
vyombo vya habari.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria ya mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Na. 3 ya mwaka 2010 na Kanuni za Mawasiliano za kulinda wateja za mwaka 2005.
“Mtu yeyote ambaye ni mfanyakazi wa kampuni yenye leseni ya kutoa huduma za mawasiliano au mwakilishi wake ana wajibu wa kutunza siri za mawasiliano binafsi na taarifa zozote za siri za wateja kwa mujibu wa sheria hii,†alisema Mkurugenzi Mkuu.Profesa Mkoma alisema mtu yeyote haruhusiwi kutoa taarifa binafsi za mteja yeyote alizopokea au kusikia kwa mujibu wa sheria hii isipokuwa mtu huyo ameruhusiwa kwa mujibu wa sheria.
Alisema kifungu cha 123 (1) kinasema mtu yeyote ambaye bila sababu za msingi atasababisha kuingilia au kuzuia kupokewa kwa mawasiliano yeyote ya kielektroniki anafanya kosa na akipatikana atatakiwa kulipa faini ya Sh. mil. tano au kwenda jela kwa muda usiopungua miaka miwili au adhabu zote kwa pamoja.
Alisema vitendo hivyo vinafanywa na mtu mwenye ujuzi na uelewa wa jinsi ya kupata taarifa hizo, na wenye ruhusa ya kufanya hivyo katika mtandao wa kampuni husika ya kutoa huduma ya mawasiliano kwenye mtandao kwa lengo la kuingilia mawasiliano binafsi ya watu.
"TCRA inayakumbusha makampuni ya simu kuweka uzuiaji na kuhakikisha siri za mazungumzo binafsi ya wateja zinahifadhiwa na hazitolewi kwa yeyote isipokuwa kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha yanafanya uchunguzi kugundua walioiningilia mazungumzo binafsi ya wateja.
Alisema kutafuta taarifa za mawasiliano ya siri kutoka kwa watoa huduma na kuzitumia binafsi pasipo kufuata utaratibu ulioruhusiwa kisheria kama zilivyochapishwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari hivi karibuni ni makosa.
Alisema TCRA inafanya uchunguzi wa uvunjwaji huo wa kutoa taarifa binafsi za wateja kinyume na sheria na wahusika wakibainika mamlaka itachukua hatua.
No comments:
Post a Comment