Na Jumbe Ismailly, Singida
BODI ya Barabara ya Mkoa wa Singida imezikumbusha halmashauri za wilaya ya manispaa mkoani hapa wajibu wao wa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya maegesho ya magari makubwa ili kupunguza msongamano kwenye maeneo ya
barabara hizo.
Wajumbe hao bodi hiyo walitoa kauli hiyo kwenye kikao chao cha 33 kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
Wajumbe hao walisema kuwa kuna baadhi ya maeneo ya miji midogo iliyopo katika halmashauri za mkoa huo hakuna utaratibu madhubuti wa kuegesha magari makubwa, zaidi ya kuyaacha barabarani, jambo ambalo wamesema linaweza kuchangia ajali zisizokuwa za lazima.
Kwa mujibu wa wajumbe hao, Bw. John Lwanji mbunge wa Manyoni Magharibi, na wabunge wa Viti Maalumu, Bi. Diana Chilolo na Bi. Christina Mughwai wameyataja baadhi ya maeneo yanayolalamikiwa kutokana na msongamano huo wa magari makubwa ni pamoja na Ikungi, Manyoni Mjini na Misigiri ambapo malori hupaki barabarani au karibu sana na barabara hizo zilizoboreshwa kwa kiwango cha lami.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Mhandisi Yusta Kangole alisema ofisi yake imekwishaainisha maeneo maalumu ya kuegesha magari makubwa, na kwamba kilichobakia ni usimamizi wa viongozi kwenye maeneo husika.
Awali akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bw. Parseko Kone alisema kuanzia sasa viongozi na watendaji wa ngazi zote wataanza kuwajibishwa kwa kushindwa kusimamia matumizi sahihi ya barabara kwenye maeneo yao.
Akifunga kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Mohamed Misanga alimhimiza Meneja wa TANROADS kuhakikisha mizani tembezi inapatikana haraka kwa lengo la kukabiliana na magari makubwa yanayovunja sheria za nchi.
No comments:
Post a Comment