07 December 2010

Tanzania yapaa baada ya mdororo

Na Peter Mwenda

SHIRIKA la Fedha la Umoja wa Mataifa (IMF) limesema Tanzania imefanya vizuri katika uchumi wake ambao ulishuka katika mdororo wa uchumi wa dunia lakini kwa sasa umeanza kupanda.Mwakilishi Mkuu wa IMF nchini, Bw. John Wakeman Linn alisema Tanzania
imeanza kuboresha huduma za kifedha kupitia benki na kufanya marekebisho ya sheria za Fedha za Umma zilizopitishwa na bunge Julai mwaka 2010.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa serikali na wahisani, Bw. Wakeman Linn aliitaka Tanzania kuweka sera madhubuti za kukabiliana na mdororo wa uchumi endapo utatokea tena duniani.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Profesa Benno Ndullu alisema shilingi ya Tanzania imeanza kupanda kulinganisha na kipindi ambacho kulikuwa na mdororo wa uchumi ulioathiri uchumi wa dunia nzima.

Alisema asilimia 25 ya Watanzania wanatumia simu za mkononi na wanamudu kununua muda wa hewani na fedha inaendelea kupanda kwa sababu kila sh. 100 ya Mtanzania anayotumia sh. 44 zinatumika kwa chakula.

Profesa Ndullu alisema kiasi hicho kimeshuka baada ya mikakati ya kufufua uchumi inayofanywa na serikali.

Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustapha Mkullo alisema mkataba kati ya Tanzania na IMF kuhusu uratibu wa mwenendo wa uchumi umeonesha mafanikio na kuahidi kuinua uchumi kwa kasi na kuongeza udhibiti.

2 comments:

  1. pETRO eUSEBIUS mSELEWADecember 7, 2010 at 1:02 PM

    Kwa kauli hii,siwaamini tena wazungu...kazi yao kutupamba tu huku wakijua wazi kuwa hali yetu ni taabani.Hawa wanatucheka tu...hawana lolote! Watu wabaya sana hawa....wanajua kuwa Serikali ya CCM inaundwa na akina-Mr.Misifa,basi.

    ReplyDelete
  2. Hizi ripoti za IMF na World bank zinatudanganya tu wanatuambia kila siku kuwa uchumi umekuwa wakati kila siku shilingi ya Tanzania inaporomoka thamani yake,maisha ya watanzania yanazidi kuwa magumu na bajeti ya serikali inazidi kutegemea michango ya wahisani

    ReplyDelete