LONDON,England
MIAMBA ya soka inayofukuzana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England, Arsenal na Chelsea, inakutana leo katika mechi ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Emirates, London.Miamba hiyo inakutana kila mmoja akiwa katika mazingira
tofauti, Arsenal watakuwa kwenye uwanjani wao wa nyumbani wakiwafukuzia vinara wa ligi hiyo Manchester United, huku Chelsea ambayo imekuwa ikifanya vibaya mechi zilizopita, ikitaka kuondokana na hali hiyo ili iweze kufufua matumaini yake ya kutetea ubingwa huo.
Kabla ya mechi za jana, Manchester United inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 34, baada ya kucheza mechi 16, ikifuatiwa na Arsenal na Manchester City, ambazo zilikuwa na pointi 32 kila moja katika mechi 17.
Chelsea wao walikuwa katika nafasi ya nne wakiwa na pointi 31 walizozivuna kwa kucheza mechi 17.
Hata hivyo, mechi hiyo inadaiwa itakuwa ni ya vuta nikuvute kutokana historia iliyopo baina ya timu hizo mbili zinapokutana.
Mbali na historia, pia mtanange huo unatarajiwa kuwa na msisimko kutokana na timu hizo wachezaji wao wa kutumainiwa kurejea uwanjani.
Kwa upande wa Arsenal ambayo mwishoni mwa wiki, iliahirishwa mechi yao dhidi ya Stoke City, hali hiyo iliwafanya wachezaji wake, Lukasz Fabianski na Abou Diaby kupata muda wa ziada wa kujiweka fiti, ingawa kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger amethibitisha kuwa, mchezaji Thomas Vermaelen atakuwa nje ya uwanja hadi mwishoni mwa Januari mwakani.
Chelsea wao wanatarajia mchezaji wao, Frank Lampard kushuka uwanjani kuikabili Arsenal baada ya kukosekana katika timu hiyo tangu mwishoni mwa Agosti mwaka huu.
Hata hivyo, timu hiyo itawakosa wachezaji wake Alex, Yossi Benayoun na Yuri Zhirkov ambao wote ni majeruhi, ingawa inatarajia kupata msaada kutoka kwa Jose Bosingwa ambaye amepona matatizo ya nyama za paja yaliyokuwa yakimkabili.
Historia inaonesha kuwa, Chelsea ndiyo inayoongoza kuondoka na ushindi dhidi ya Arsenal, baada ya kupoteza mechi mbili kati ya mechi 18, walizokutana katika michuano mbalimbali na kuibuka wababe mara tano katika mechi zilizopita.
Blues wanaongoza kwa kupachika mabao dhidi ya wapinzani wao baada ya kufunga mabao 11, katika mechi nne walizokutana na Gunners, huku ikiwa imeruhusu bao moja.Mbali na rekodi hiyo, ndiyo timu ya kwanza kushinda mechi nne mfululizo za ligi dhidi ya Arsenal tangu Liverpool ilipofanya hivyo kati ya mwaka 1996 hadi mwaka 1998.
No comments:
Post a Comment