24 December 2010

Krismasi Gizani

Na Peter Mwenda

SIKU moja kabla ya sikukuu ya Krismasi Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza mgawo mwingine wa umeme katika mikoa yote iliyoungwa katika gridi ya taifa kutokana na upungufu wa umeme.Meneja Mawasiliano wa
Tanesco, Bi. Badra Masoud aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa upungufu huo wa umeme umejitokeza baada ya kampuni ya Pan Africa inayoliuzia shirika hilo gesi, kuzima moja ya visima vyake vinavyotoa nishati hiyo.

"Ukosefu huo wa gesi umesababisha mitambo kushindwa  kuzalisha umeme wa kutosha na kusababisha kupungua kwa megawati 40 za umeme katika gridi ya taifa," alisema Bi. Masoud.

Alisema upungufu huo umesababisha shirika hilo kufanya mgawo wa mikoa yote inayopata umeme katika gridi ya taifa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12 jioni katika baadhi ya maeneo na saa 12 jioni hadi saa 5 asubuhi kwingineko.

Bi. Masoud alisema ratiba ya mgawo huo itatangazwa kwenye vyombo vya habari na kueleza kuwa katizo la umeme halitawahusu wakazi waliokuwa wakitumia transfoma ya Kipawa.

"Transfoma ya Kipawa imekwishatengemaa kuanzia leo (jana) hali ya umeme katika maeneo yaliyoathirika kutokana na kuharibika kwa transfoma itarejea kama kawaida na wateja wa maeneo hayo hawatakumbwa na mgawo huo tuliotangaza," alisema Bi. Badra.

Maeneo ambayo yaliathirika na kuharibika kwa transfoma la Kipawa na sasa hawataguswa na mgawo huo ni Tandika, Temeke, Mbagala,Chang'ombe, Uwanja wa Taifa, Kitunda,Kivule, Gongo la Mboto na Kisarawe mkoa wa Pwani.

Alisema shirika pia linawaomba radhi wateja wake wa mkoa wa Dar es Salaam kutokana na maeneo mengi ya jiji kutoka umeme Jumanne iliyopita kuanzia asubuhi hadi usiku.

alisema kukosekana huko kwa umeme kulitokana na kampuni ya Pan Africa kuzima mitambo yote ya kuzalisha gesi kutokana na sababu za kiufundi.

3 comments:

  1. Serikali isiyokuwa halali huwa haina baraka za Mungu!

    Hakuna hatua yoyote inayopigwa kwenda mbele. Serikali inatumia nguvu na ubunifu wake wote kuwapiga wapinzani na wabunge.

    Serikali haina dira yeyote isipokuwa kung'ang'ania madaraka na kuchakachua chaguzi mbalimbali

    ReplyDelete
  2. Umeme ni swala la msingi la kushughulikiwa na serikali na sio kushughulikia wasio wanamtandao kama Tido walivyomchakachua. Makaa ya mawe mengi nchi hii lakini hayatumiki, mfano kiwila coal mine wafanyakazi hawana mishahara kisa, mkaa hauna soko, wakati mgodi unauwezo wa kuzarisha umeme mwingi. Watanzania mkiendelea na usanii iko siku mtabinafsisha nchi yenu

    ReplyDelete
  3. HAYA NDO YA JK ETI RAIS MPENDA WATU KUMBE RAIS "RAHISI", MSANII MKUBWA HUYU TENA KIBARAKA WA MANYANG'AU; MAFISADI ANAOWAFUGA. YEYE NDO KISA CHA MATESO YOTE WA-TZ WANAYOPITIA. EEH MUNGU TUEPUSHE NA UPOFU WA HUYU MTU ANATUPELEKA SHIMONI, KWANI DHAMBI ZAKE NI ZA WATZ WOTE? TUREHEMU MUNGU MWEMA, TUNAANGAMIA.

    ReplyDelete