Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wanaosumbuliwa na ugonjwa moyo wameshauriwa kujitokeza ili wapimwe na kisha watafutiwe wafadhili wa kwa ajili ya kwenda kutibia nje ya nchi.
Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam juzi jioni na Mwenyekiti wa Klabu ya Lions ya Dar es Salaam (host), Bw. Frank Goyayi, wakati akizungumza na wagonjwa waliotoka India kwa ajili ya matibabu.
Wagonjwa 14 wengi wao wakiwa watoto walipelekwa India kwa ajili ya upasuaji wa moyo ambapo walirejea nchini wakiwa wenye afya njema baada ya kupata tiba.
Waliwasili juzi jioni katika Uwanja wa Ndege Kimataifa wa Jilius Nyerere na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Klabu ya Lions ya Dar es Salaam.
Bw. Goyayi alisema klabu hiyo inatoa mwito kwa wote wanaoona wana matatizo hayo kujitokeza ili wasaidiwe.
“ Regency Medical Center imekuwa ikiwachunguza moyo watu wenye matatizo na wanaogundulika kuwa na matatizo tunawatafutia wafadhili kwenda kutibiwa nje,” alisema Bw. Goyayi
Naye Mratibu wa magonjwa ya moyo katika klabu hiyo, Dk. Rajni Kanabar alisema wagonjwa waliorudi juzi jioni walitibiwa katika Hospitali ya Fortis Escorts iliyoko New Delhi, India.
Aliwashukuru wasamaria wema waliojitolea kusaidia wagonjwa hao akiwemo mfanyabiashara maarufu Mustafa Sabodo aliyetoa dola 20,000 na Wizara ya Afya ya Zanzibar kwa kufadhili watoto 15.
Alimshukuru pia Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Bw. Reginald Mengi ambaye amekuwa mfadhili wa muda mrefu kwa wagonjwa wa moyo wanaokwenda India kutibiwa, bila kusahau Mbunge wa Hanang (CCM), Dkt. Mary Nagu.
Wagonjwa hao walifanyiwa upasuaji kwa gharama ya dola 2,000 kila mmoja, kiwango ambacho alisema ni kidogo kulinganisha na hospitali zingine duniani.
No comments:
Post a Comment