26 November 2010

Tume kuchunguza mikopo ya wanafunzi.

Na Pendo Mtibuche, Dodoma

RAIS Jakaya Kikwete amewatoa hofu wanafunzi wa elimu ya juu kuwa serikali inaendelea na jitihada za kuongeza fedha katika mfuko wa bodi ya mikopo ambao kwa mwaka huu ulipewa
sh. bilioni 237 kwa ajili ya kudhamini wanafunzi wengi zaidi tofauti na mwaka jana.

Kauli hiyo aliitoa jana lipofungua rasmi Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambacho kitakuwa kikubwa zaidi kuliko kingine chochote nchini, huku akiahidi kuunda tume maalumu kuchunguza mfumo wa utoaji mikopo.

Rais Kikwete alisema kuwa ataunda tume maalumu ya kuchunguza mfumo mzima wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na utendaji wa Bodi ya Mikopo kwa nia ya kuboresha mfumo huo na kuleta ufanisi zaidi.

“Tutautazama upya mfumo mzima wa utoaji wa mikopo ikiwepo na utendaji kazi wa Bodi ya Mikopo kwa nia ya kuuboresha na kuleta ufanisi zaidi. Nitaunda tume maalumu ambayo nakusudia kuhakikisha inaanza kazi ifikapo Januari mwakani,” alisema.

Aidha, Rais Kikwete alisema kuwa ataiagiza tume hiyo kupata mawazo ya wamiliki wa vyuo vikuu, wahadhiri na wanafunzi ili kupata ushauri uliokamilika.

Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Chimwaga kwenye chuo hicho, na kuhudhuriwa na mamia ya wanafunzi, wahadhiri, viongozi na watu wengine mbalimbali.

“Kuhusu mikopo ya elimu ya juu, napenda kuwahakikishia wazazi na wanafunzi kuwa tutaendelea kuongeza fedha katika mfuko huo ili wanafunzi wengi wanufaike. Tumefanya hivyo katika miaka mitano iliyopita na tutafanya hivyo siku za usoni.”

“Serikali imeongeza fedha za mikopo ya wanafunzi kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005/06 hadi kufikia shilingi bilioni 237 mwaka 2010/11. Wanafunzi waliopatiwa mikopo imeongezeka kutoka 16,345 hadi 69,921. Haya ni mafanikio makubwa na naahidi kuwa tutafanya vizuri zaidi ili tuwafikie wanafunzi wengi zaidi.”

Wakati huo huo, Rais Kikwete aaliupongeza uongozi wa UDOM kwa kutimiza ndoto yake na pia ameutaka kukitunza chuo hicho ambacho ni moja ya vyuo vizuri zaidi katika Afrika.

UDOM ilizaliwa kutokana na wazo binafsi la Rais Kikwete katika kutafsiri maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi wa CCM mwaka 2005 iliyotaka kupanuliwa kwa fursa katika elimu ya juu.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na Mkuu wa chuo hicho, Bw. Benjamin Mkapa, Rais wa Tanzania wa awamu ya tatu; Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Garib Bilal, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kwanza wa Baraza la Chuo, na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Idris Kikura. Dkt. Bilal pia alikuwa mhadhiri wa fizikia na msimamizi wa wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PHD) katika chuo hicho.

2 comments:

  1. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 26, 2010 at 12:51 PM

    Nasisitiza kuwa Rais Kikwete na CCM yake ni watu waliojaa sanaa.Kuna haja gani ya kuwa na Tume inayoshughulikia mikopo wakati kuna Bodi kabisa iliyoundwa kwa mujibu wa sheria kwa ajili hiyo? Basi hapa pana harufu ya ajira mpya tu...si lolote,si chochote! Kinachotakiwa ni Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Chini ya Mh.Mkono iwezeshwe ipasavyo ili kufanya kazi zake.Kwani Bodi imeshindwa? Sasa Tume itawezaje? Usanii mtupu.Hawa watu bwana ...sijui nihamie wapi mie!

    ReplyDelete
  2. Suala la kikwete kuunda tume ya kuichunguza bodi ya mikopo inaonyesha jinsi gani rais huyu mteule wa tume ya uchaguzi(NEC) alivyokosa zana ya uwajibikaji bora,kuna haja gani ya kuunda tume na wakati bodi hii ya mikopo imeanzishwa kishwria,kama wameshindwa kuiendesha basi wapelekwe mbele ya vyombo vya dora wakawajibishwe na sio kuunda tume itakayolinda uozo wa bodi hiyo,kwani hata tume ya mwakyembe ilifanya kazi lakini selikari iliwalinda mafisadi wale walioitafuna inji.SISI wanaharakati WACHACHE wa UDOM hatumuungi mkono jamaa huyu hata kidogo,labda SUA au UDSM.
    WANAHARAKATI UDOM wanaopingana na sera za sisiemu.

    ReplyDelete