*Baada ya kuichapa Sudan 2-0, Rwanda yang'ara
Na Zahoro Mlanzi.
BAADA ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Taifa ya Sudan, Kocha Mkuu wa Zanzibar 'Zanzibar Heroes', Hall Stewart ametamba kuendeleza wimbi la ushindi katika michezo
yao inayofuata.
Ushindi huo waliupata jana katika mfululizo wa michezo ya mashindano ya Kombe la Tusker Chalenji yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mbali na Zanzibar Heroes kuchomoza na ushindi huo, Rwanda nayo iliichapa Ivory Coast kwa mabao 2-1 kwenye uwanja huohuo na Burundi nayo iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Somalia katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Karume, jijini.
Akizungumza mara baada ya kumazika kwa mchezo huo ulioanza saa nane mchana, Stewart alisema ana wachezaji wa kutosha kuhakikisha katika mchezo wao unaofuata dhidi ya Ivory Coast utakaopigwa Desemba Mosi, wanaibuka na ushindi.
"Unajua kikubwa kinachoitatiza Zanzibar ni kukosa mechi za kimataifa, lakini ninawahakikishia wazanzibar timu hii itafika mbali na ninakiomba Chama cha Mpira wa Miguu Zanziba (ZFA) kuendelea na mchakato wao wa kuwa mwanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu," alisema Stewart.
Katika mchezo huo, mabao ya Zanzibar Heroes yalifungwa na Ali Ahmad 'Shiboli' aliyeifungia timu yake mabao yote katika dakika za 11 na 65 ambapo katika mchezo huo ameonesha kiwango kizuri kutokana na kila wakati kuwasumbua mabeki wa Sudan.
Shiboli ambaye kwa sasa amesajiliwa na mabingwa wa Tanzania bara, Simba kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, dakika ya 53 nusura aifungie bao timu yake baada ya kupiga shuti lililookolewa kwa miguu na kipa Amir Suliman.
Mchezo uliofuata ulikuwa kati ya Rwanda na Ivory Coast ambapo Rwanda ilishinda mabao 2-1, mabao ya Rwanda yalifungwa na Dady Birori kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Haruna Niyonzima na la pili dakika ya 79 na Peter Kagabo na la kufutia machozi lilifungwa na Kone Zoumana kwa kisigino.
No comments:
Post a Comment