Na Zahoro Mlanzi.
BARAZA la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limezindua na kukabidhi Kombe jipya la mashindano ya CECAFA Tusker Chalenji yanayotarajiwa
kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Jumamosi.
Mbali ya hilo, wadhamini wa mashindano hayo Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), imezipa changamoto timu za taifa za Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars' na Zanzibar 'Zanzibar Heroes', kuhakikisha mojawapo inatwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Akizungumza kabla ya kukabidhiwa kombe hilo Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Idd Kipingu ambaye pia alikuwa mgeni rasmi, alisema anaishukuru SBL kwa kutenga mamilioni ya fedha kwa ajili ya mashindano hayo.
"Tunaishukuru SBL kwa udhamini wao, kwani hizo fedha walizotenga wangeweza kufanyia mambo mengine lakini kwa kufanya hivyo wanajua umuhimu wa michezo kwani huleta amani na kujenga umoja miongoni mwa nchi washiriki," alisema Kipingu.
Alisema kutokana na mashindano hayo, ana imani katika fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil, timu mojawapo ya ukanda huu itashiriki, hivyo ni muda muafaka kuanza maandalizi kuanzia sasa.
Akitolea mfano nchi ya Botswana, ambayo kwa sasa inahitaji pointi mbili ifuzu fainali za Mataifa ya Afrika, imefikia hatua hiyo kutokana na mipango madhubuti ya kuendeleza soka la vijana.
Naye Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alisema timu ya Sudan ilitarajiwa kuwasili nchi jana mchana na Zanzibar Heroes, itaingia leo ambapo mpaka kufikia Ijumaa ana imani timu zote zitakuwa zimefika.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Mauzo wa SBL, Caroline Ndungu, alisema atajisikai furaha kuona timu wenyeji ambazo ni Kili Stars na Zanziba Heroes, zikilibakisha kombe katika ardhi ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment