Na Mwandishi Wetu
MSANII wa kimataifa raia wa Jamaica, Windel Beneto Edwards 'Gyptian', amewasili nchini na kuwaomba wanachuo na wapenzi wa muziki kujitokeza kwa wingi kesho katika tamasha la
'Str8Muzik Festival Inter-College Special 2010' ambapo atatumbuiza.
Tamasha hilo, chini ya udhamini wa Kampuni ya Sigara ya Tanzania (TCC), kupitia sigara ya SM litafanyika katika viwanja vya Posta Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
Gyptian alitua nchini juzi usiku na kupokewa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na Meneja Msaidizi wa SM, Isamba Kasaka.
Alisema amefarijika kufika Tanzania, katika tamasha la Str8Muzik Festival Inter-College Special 2010, ambalo linakutanisha wanachuo kutoka vyuo na taasisi mbalimbali za elimu ya juu kwa lengo la kubadilishana mawazo na kuburudika.
“Mimi nimeshafika na wasanii wengine wakubwa wapo njiani, sasa cha msingi ni watu wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya tamasha hilo,” alisema Gyptian ambaye anatamba na nyimbo zenye miondoko ya reggae.
Mwanamuziki huyo alisema hii ni mara yake ya tatu kufika Afrika, kwani alishawahi kutumbuiza Kenya na Senegal.
Wimbo wake wa kwanza ‘Serious Times’ ulipata tuzo katika kipengele cha Nyimbo Muhimu mwaka 2005. Miongoni mwa nyimbo nyingine ambazo zimemweka Gyptian, juu katika ramani ya muziki duniani ni ‘Is There a Place’, ‘Beautiful Lady’, ‘Mama’ na ‘Don’t Cry’.
Wasanii wengine wa kimataifa wanaotarajiwa kuwasili leo kwa ajili ya tamasha hilo ni Elephant Man, Mims na T-Pain.
Tamasha la Dar lilitanguliwa na matamasha mengine Mjini Morogoro Novemba 13 na Dodoma 20, mwaka huu ambapo wasanii mbalimbali walitumbuiza.
No comments:
Post a Comment