25 November 2010

Kikwete awaridhisha wananchi.

Na Reuben Kagaruki.

WATANZANIA wa kada mbambali wametoa maoni yanayotofautiana kuhusu uteuzi wa Baraza la Mawaziri kwa maelezo kwamba hakuna jambo jipya, ingawa wengine wamepongeza hasa
uteuzi wa Profesa Anna Tibaijuka na Dkt. John Magufuli kurejeshwa katika wizara aliyowahi kuimudu vizuri.

Wakizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema Rais Kikwete hakuwa na sababu ya kuchukua muda mrefu kuunda baraza hilo, wakati halina mawaziri wenye sifa ambazo wananchi walidhani anahaha kuwapata.

Mwenyekiti wa APPT-Maendeleo, Bw. Peter Mziray, alisema; "Sijaona kitu kipya sana, Rais Kikwete amezungukwa na watu wale wale...hakuna kitu kipya cha kutegemea."

Alisema uchaguzi mkuu ulikuwa na changamoto nyingi ambazo Watanzania walitarajia zingemwongoza rais kuchagua Baraza la Mawaziri wanalolitaka.

Hata hivyo alipongeza uteuzi wa Dkt. Magufuli kuongoza Wizara ya Ujenzi, akisema ni mtu mchapakazi na mfuatiliaji mzuri.

Kwa upande wa Profesa Tibaijuka ambaye ameteuliwa kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Mziray alisema;

"Tibaijuka ni mchapa kazi labda akwamishwe na urasimu wa serikali...ni chaguo zuri tutaangalia kama atafanikiwa."

Akizungumzia Dkt. Shukuru Kawambwa kuhamishiwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Mziray alisema;

"Huyo amekuwa na desturi ya kuhamahama, amegeuka kama mtalii kwenye mawizara, sijui anamtayarisha ili awe rais! Lakini utendaji wake haujaonekana."

Kwa upande wa Bw. Stephen Wasira kuhamishiwa Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Mziray alisema; "Mtu kama huyo alitakiwa akae pembeni, amekuwa waziri tangu tukiwa watoto, lakini hakuna alichokifanya."

Alisema kitendo cha kumpeleka katika wizara ambayo haikutani na watu ni njia mojawapo ya kumwondoa. Alipongeza uteuzi wa Dkt. David Mathayo David kuongoza Wizara ya Mifugo na Uvuvi, hasa kwa kuzingatia kuwa taaluma yake inahusika na mifugo.

Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Bw. Tundu Lissu, akitoa maoni yake kuhusu baraza hilo, alisema; "Mambo ni yale yale, kwa hiyo tutakutana nao bungeni."

Alisema pamoja na Rais Kikwete kubadilisha mawaziri wa kuongoza wizara, lakini watendaji bado ni wale wale ambao wamekuwa wakiharibu kwa miaka zaidi ya 20.

"Profesa Tibaijuka anakwenda kusimamia watu wale wale ambao wamekuwa wakiharibu kwa miaka 20, kwa hapa tutegemee nini?...tutakutana nao kule kule (bungeni)," alisema.

Alisema kwa mtazamo wake bado hajaona mawaziri ambao wataweza kuchapa kazi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bw. Niclous Mgaya alisema katika baraza hili la mawaziri wafanyakazi wamefarijika kuona Profesa Juma Kapuya anaondolewa katika Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana kwa kile alichodai kwamba alikuwa kikwazo cha madai mengi ya watumishi.

Alionekana kuwa na imani na uteuzi wa Bi. Gaudensia Kabaka.

"Ni mtu ambaye hana kashifa yoyote anaweza kufanya vizuri, tutaangalia atafanyaje kazi kwa misingi ya kisheria na kuitisha vikao vya majadiliano na sisi," alisema.

Kwa upande wa uteuzi wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Hawa Ghasia, Bw. Mgaya;

"Ni masikitiko kama amerudi, lakini tutaendelea kufanya naye kazi, ugomvi wetu na yeye ni kutopenda kuitisha vikao vya majadiliano ili kutatua mgogoro ya wafanyakazi."

Alisisitiza kuwa kama atafanya kazi inavyotakiwa watatangaza kuwa na imani naye.

Akizungumzia uteuzi wa Bw. Samuel Sitta kuongoza Wizara ya Afrika Mashariki, Bw. Mgaya alisema; "anastahili kuongoza wizara hiyo kwa kuwa ni mtu mwenye uzoefu."

Kwa ujumla alisema baraza hilo limejumuisha vijana na wazee, hivyo ni vema wananchi wakaanza kuamini vijana. "Tuwape muda tuone watafanya nini," alisema.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) na mbunge wa Vunjo, Bw. Augustino Mrema alipongeza uteuzi wa Bw. Magufuli na Profesa Tibaijuka huku akichekelea wizara aliyopewa Bw. Sitta kwa madai kuwa inamstahili ili akamfungwe mdomo.

"Baraza ni zuri amejitaidi ingawa sio dogo," alisema. Askofu wa Africa Inland Church, Charles Salala, aliungana na wananchi wengine kupongeza uteuzi wa Bw. Magufuli, Profesa Tibaijuka na Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye atakuwa Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi.

Alisema uteuzi wa Bw. Magufuli na Dkt. Mwakyembe ni wazi kwamba umelenga kutekeleza ahadi ya rais za ujenzi wa viwanja vya ndege alivyoahidi kujenga wakati wa kampeni katika maeneo mbalimbali ya nchi.

"Hiki ndicho kipindi chake cha mwisho inawezekana ndiyo maana amewateua kuongoza wizara hiyo (ujenzi)," alisema Askofu salala.

6 comments:

  1. Nawashangaa wanaokosoa kwa ajili tu ya kukosoa, hao wanaosema baraza hili halina jipya kwa sababu walioteuliwa ni walewale. Kwani Baraza si linatokana na wabunge tuliowachagua? Na tuliowachagua si ndio walewale? Au tulietegemea rais atoe mawaziri wote kutoka nafasi 10 za uteuzi alizopewa na Katiba? Lakini hata hao wangetoka wapi kama si miongoni mwetu? Si wangekuwa ni walewale? Au wanamaanisha angeteua wapinzani? Nao si ndio walewale, waliohama kutoka CCM baada ya kukosa utezi au ambao hawana uzoefu kabisa wa uongozi sawa na hao wapya walioteuliwa mara hii wanaolalamikiwa pia? Au tulitaka Rais awape uraia wageni mahsusi wawe wateule wake wa ubunge na hatimaye uwaziri ili tupate mawaziri wasio walewale? Wanasiasa wawache kuwachanghanya wananchi kwa vijisababu vya kitoto kama hivi. Tunaweza tukajutia mapema kwa nini tumewapa kura zetu! Tunaweza hata kuanza kuviuliza vyama vyao vinani hata wakatuteulia wagombea kama wao. Mbona hata uteuzi wa wagombea kwenye vyama vyao, wakiwamo wa viti maalum, ni walewale? Ni unafiki kuhubiri maji huku ukinywa mvinyo!

    ReplyDelete
  2. Jumanne Maghembe nenda kapambane vema na wakulima maana wizara ya elimu ilikushinda; katika utawala wako kiwango cha ufaulu kilishuka sana na haukufanya chochote kuboresha hali za walimu; na hata suala la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu haukulisimamia ipasavyo ndiyo maana migomo ya wanafunzi ilishamiri. Kuwa makini sana kwenye kilimo kwasababu huko nako ukiharibu utatuua kwa njaa.

    ReplyDelete
  3. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 25, 2010 at 10:09 AM

    'Viva la Amistad entre los publeos de CHADEMAn Tanzania'.

    ReplyDelete
  4. HIVI KUNA UWEZEKANO WA KUAZIMA MTU KUTOKA NJE YA NCHI AKAGOMBEA URAIS? MIMI NAONA KICHEFU CHEFU KWA KWELI. WATANZANIA MTAKAA MNATEGEA NEEMA NA HAMTAIONA KAMWE!!!!!!!!!! ANDIKENI MAUMIVU,KWANI KIKWETE LEO NI MPYA? ACHENI UNAFIKI,MAWAZIRI HAMJAWAHI KUWAONA? ACHENI USHAMBA JAMANI,HAKUNA LOLOTE LA MAANA UNALOLITEGEMEA ZAIDI YA WAO KUJINUFAISHA NA FAMILIA ZAO.WAKATI WEWE UNANUNUA MCHICHA NA NYANYA ZA SHILINGI 200 MWENZAKO ANAPOKEA MSHAHARA WA MILION 200 NA GARI YA KIFAHALI.FANAYENI KAZI USHABIKI WA KISISA HATUJUI NDO MAANA TUTAKUWA MASIKINI MPAKA YESU ATAKAPORUDI.

    ReplyDelete
  5. Wizara 29, GDP ya Tz below USD 25 billion, hapa kidogo JK ume overlook!

    Kwa nini usijenge kikosi kibunifu cha wachapa kazi kama wizara chini ya 15, ndani yake manaibu mawaziri proffesionals kushughulikia matatizo na maendeleo mbali mbali ya nchi.

    Pia, ungelipamba baraza lako kwa kuwaingiza qualified opposition MPs kwa lengo la kuwa wewe ni Raisi wa raia wote, wakiwemo wasiokuchagua.

    Hata hivo unastahili CREDIT kuweza ku double Tz per capita GDP within 5 years!

    Be focused, economy inaweza ikawa legacy nzuri ya utawala wako!

    ReplyDelete
  6. Nimefurahi Chirigati katoka. Watu wa namna yake ni hatari kwa amani ya Taifa. Tukumbuke usemi wake kuhusu kura za maoni Nzega. Au kuwafukuza Ubunge Wabunge wa Chadema!!!!!

    ReplyDelete