29 November 2010

Kandoro ataka BMU chafu zivunjwe.

Na Faida Muyomba, Sengerema.

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Abass Kandoro, ameziagiza halmashauri zote za wilaya mkoani humo kuhakikisha Kamati za Ulinzi na Rasilimali za Uvuvi (BMU) zinazonuka vitendo vya
rushwa na kuendeleza uvuvi haramu katika ziwa Victoria zinavunjwa mara moja.

Mkuu huyo wa mkoa wa Mwanza, alitoa kauli hiyo katika kijiji cha Kahunda, wilayani Sengerema juzi mara baada ya kuweka jiwe la msingi la kituo cha kupokelea samaki kitachogharimu sh. 531,962,726.88.

Kituo hicho kimejengwa chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya (EU) na kitakapokamilika kitakuwa miongoni mwa vituo sita vilivyojengwa nchini kwa ufadhili.

Alisema kuwa kituo hicho kimetumia fedha nyingi ili kutengeneza mazingira bora kwa uvuvi endelevu hapa nchini, hivyo itakuwa kazi bure endapo kitatumika katika shughuli za uvuvi haramu kinyume na matarajio yaliyowekwa.

Alizitaka halmashauri zote za wilaya mkoani humo, kuhakikisha zinakomesha vitendo vya uvuvi haramu katika maeneo yao kwa lengo la kulinda hifadhi ya samaki ndani ya ziwa hilo ili kulinda soko na pato la taifa.
 
Mapema katika taarifa yake kwa mkuu wa mkoa, Mratibu wa Mpango wa Usimamizi wa Uvuvi katika Ziwa Victoria [IFMP) Bw. Lameck Mongo, alisema lengo la kujengwa kwa kituo hicho ni kuboresha na kuendeleza wavuvi katika mialo yao.

Alisema mbali na lengo hilo pia kitawasaidia kupata ubora na usalama wa samaki wanaokidhi viwango vya kimataifa katika soko la ndani na nje ya nchi na
alivitaja vituo vingine kuwa ni Katunguru, Kigangama (Magu), Bwai (Musoma), Sota (Rorya), Ikumba Itare(Chato) na Marehe (Bukoba).
 
Katika vituo hivyo sita jumla ya sh. bilioni 3.3 zitatumika hatua inayodaiwa kuwa itachangia kukuza Pato la Taifa.

1 comment:

  1. Bryceson Mathias, Dodoma.

    Mhariri,

    Neno BMU katika habari 'Kandoro ataka BMU chafu zivunjwe'si sahihi, Neno sahihi ni PMU maana yakeni Procurement Management Unit; BMU inaleta tafsiri tofauti. Mwandishi wa majira Dodoma.

    ReplyDelete