Na Pendo Mtibuche, Dodoma.
SERIKALI imesema kuwa ili Chuo cha Elimu ya Bishara (CBE) kiweze kufanikiwa ni lazima kijikite zaidi katika kufanya tafiti makini zitakazowasaidia Watanzania kupata biashara za kisasa kwa lengo la
kukuza Pato la Taifa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Bi. Joyce Mapunjo wakati wa mahafali ya 45 ya chuo hicho, kampasi ya Dodoma.
Bi. Mapunjo alisema kuwa katika dunia ya leo kitu kinachokubalika na kuheshimika katika utoaji wa hoja au maamuzi ni fikra zinazotokana na utafiti makini, iwe katika siasa, uchumi, utamaduni na hata vitu vingine.
Alisema kuwa baada ya kulibaini hilo, wizara itaendelea kushirikiana na uongozi wa chuo kwa lengo la kuimarisha uwezo wa wahadhiri kufanya utafiti ulio makini, hasa kwa kusaidia kuwajengea uwezo wa kiujuzi wahadhiri kupitia mafunzo na upatikanaji wa vitendea kazi vya kisasa.
Vile vile alisema kuwa katika ulimwengu wa sasa nchi zinazowekeza katika utafiti na uendelezaji bidhaa na huduma ndizo zinatazamiwa ziwe waanzilishi wa mawazo yenye mwelekeo wa kiubunifu iwe ndani ya wizara na hata ndani ya serikali.
Akizungumzia suala la miundombinu ndani ya chuo hicho, Katibu Mkuu huyo alisema kuwa taasisi hiyo ambayo imeonyesha wazi kuelekea kuzidiwa na idadi kubwa ya wanafunzi na hali hiyo kuonekana kuleta usumbufu suala ambalo alisema kuwa yeye kama katibu mkuu ataendelea kuwasiliana na hazina ili kutoa udhamini kwa chuo hicho na kukiwezesha kupata mkopo kutoka kwenye taasisi za fedha.
“Nafahamu vema kwamba majengo ya kampasi hii yalifanyiwa ukarabati kwa mara ya mwisho mwaka 1993-1994 na hali ya majengo yote ni mbaya, mifumo ya majisafi, majitaka na umeme imechoka sana na inahitaji kubadilishwa.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho, kampasi ya Dodoma, Dkt. Wycliffe Lugoe akitoa maelezo ya chuo hicho alisema kuwa chuo hicho kwa sasa kimekuwa na ongezeko kubwa la wanachuo katika kampasi zake tatu za Dar es Saalam, Dodoma na Mwanza, kitu kinachosikitisha kuwa kuna mwamko mkubwa wa wananchi kuhitaji elimu ya juu.
Dkt. Lugoe alisema moja ya changamoto zinazokikabili chuo hicho ni kukosa maktaba kubwa na ya kisasa, mabweni ya kutosha kwa ajili ya wanachuo, uhaba wa madarasa pamoja na upungufu mkubwa wa wafanyakazi.
Katika mahafali hayo wahitimu walikuwa 1,165, kati yao 542 wa ngazi ya astashahada, 380 ngazi ya stashahada, 216 stashahada ya juu na 27 stashahada ya uzamili.
No comments:
Post a Comment