MILAN, Italia
MSHAMBULIAJI wa timu ya Inter Milan, Samuel Eto'o ameomba radhi kwa kitendo chake cha kumtandika kichwa mchezaji mwenzake, wakati wa mechi ya Ligi ya Seria A iliyofanyika
Jumapili iliyopita.
Eto'o aliamua kumtandika kichwa mchezaji wa timu ya Chievo, Bostjan Cesar akipinga kufanyiwa madhambi na mchezaji huyo, kitendo ambacho matokeo yake nahodha huyo wa timu ya taifa ya Cameroon amefungiwa mechi tatu.
"Napenda kuomba radhi kwa kila ambaye alishutushwa na kitendo changu cha kushikwa na hasira," alisema Eto'o.
"Msamaha wangu ni kwa wahusika wakuu wa mchezo, waamuzi, mashabiki na kila mwenye mapenzi na soka," aliongeza na akasema kuwa pia anapenda kuomba radhi kwa kocha wake, Rafael Benitez na wachezaji wenzake ambao hatakuwa nao katika mechi tatu.
Maofisa hao wa ligi ya Italia walilazimika kutumia mkanda wa video kumuadhibu, Eto'o baada ya mwamuzi kulikosa tukio hilo wakati wa mechi hiyo ambayo, Inter Milan ilifungwa mabao 2-1.
Taarifa kutoka Serie A ilieleza kuwa kitendo cha Eto'o, kumpiga mwenzake kichwa ni cha kusikitisha na kinajumuishwa na kufanya vurugu.
Mchezaji huyo ambaye pia amelimwa faini ya euro 30,000 ambazo ni sawa na pauni 25,600 ataonekana tena uwanjani Jumatano wiki ijayo, katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Ulaya wakati timu hiyo itakapokutana na FC Twente.
Hata hivyo kufungiwa kwake inadaiwa ni pigo kubwa kwa kocha wa Inter Milan, Rafael Benitez ambaye tayari anakabiliwa na kuwa majeruhi wengi akiwemo, Diego Milito.
Mabingwa hao wa Ulaya, pia wanakabiliwa na kushuka kiwango na kwa sasa wapo nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo ya Serie A, wakiwa nyuma kwa pointi tisa dhidi ya watani wao wa jadi kwenye mji huo, AC Milan.
Na kwa kocha huyo wa zamani wa Liverpool, Benitez pia anadaiwa katika vyombo vya habari nchini humo kuwa huenda akafukuzwa, endapo watapoteza mechi yao dhidi ya Twente.
No comments:
Post a Comment