13 March 2013

Mauaji ya waandishi yawagusa wadau

Na Rehema Maigala

WADAU wa habari nchini, wamekubaliana kuunda kamati ya watu 16 ambayo itakutana na wakuu wa vyombo vya  usalama nchini ili kuzungumzia undani wa suala la usalama wa waandishi wa habari nchini.


Kamati hiyo inatarajiwa kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Said Mwema, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Bw. Othuman Rashid pamoja na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dkt. Edward Hoseah.

Katika kikao hicho, wadau hao walizungumzia vitendo ambavyo wanafanyiwa waandishi wa habari nchini kwa kushambuliwa, kuumizwa, pamoja na kuuawa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari
nchini (MOAT), Reginald Mengi, alisema lengo la kikao hicho
ni kujadili hali ya kuzorota kwa mazingira ya usalama wa
waandishi wa habari, wanaharakati, kutoa matamko na
kuunda kamati ya watu 16.

Akisoma tamko la kwanza, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Business Times Limited (BTL), Bw. Aga Mbuguni alisema, wao wanaamini kuvamiwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Bw. Absalom Kibanda, kumetokana na msimamo imara wa kalamu yake.

“Shambulio lililofanywa dhidi ya Kibanda halikutokana na kitu kingine chochote zaidi ya kazi yake ya uandishi wa habari hivyo wadau wa habari wamelichukua jambo hili kama shambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini, kuwajengea hofu wahariri, waandishi na wanaharakati wote ili wasitekeleze wajibu wao kwa umma,” alisema Bw. Mbuguni.

Tamko la pili lililosomwa na Bw. Tumaini Mwailenge kutoka Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISATAN).

Katika tamko lake, Bw. Mwailenge alisema wadau wa vyombo
vya habari wanaona tukio hilo ni mfululizo wa mashambulizi wanayofanyiwa waandishi na wahariri ambapo kutokana na
hali hiyo usalama wao upo mashakani.

Alisema awali alianza kushambuliwa Mhariri wa Gazeti laMwanaHalisi, Bw. Saed kubenea na Bw. Ndimara Tegambwage, kutekwa kwa Dkt. Steven Ulimboka na kuuawa kwa mwandishi wa Kituo cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosina ambapo hivi sasa, shambulizi limehamia kwa Bw. Kibanda.

Katika tamko la tatu, lilisomwa na Mhariri Mkuu wa Gazeti la Nipashe, Bw. Jesse Kwayu, ambaye alisema wadau wa habari wamesikitishwa na baadhi ya maofisa, watumishi wa vyombo
vya usalama kutumiwa kutekeleza vitendo vya uhalifu ambavyo vinatishia usalama wa waandishi na wananchi.

Alitolea mfano usumbufu alioupata mwandishi, Bw. Erick Kabendera na familia yakeambapo wazazi wake walihojiwa
na watu waliojiita watumishi wa umma ili kutekeleza matakwa
ya kuzorotesha kazi zinazofanywa na waandishi nchini.

Akisoma tamko la nne, Bw. Hussein Bashe ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya New Habari, aliitaka Serikali iunde tume huru ya wapepelezi kuchunguza undani wa masuala hayo.

Alisema kasi ya uchunguzi wa vyombo vya usalama nchini bado  hairidhishi ambapo baadhi ya watendaji ndani ya vyombo hivyo wanahusishwa na kadhia hizo.

Naye Bw. Kubenea, alitoa tamko la mwisho na kudai kuwa, wadau wa habari wamekubaliana kuunda kamati ya watu 16 ambayo itakutana na wakuu wa vyombo vya usalama nchini.

Wajumbe wa kamati hiyo ni Bw. Mengi, Bw. Henry Muhanika ambaye ni Katibu (MOAT), Bw. Bashe, Bw. Tido Mhando ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Kampuni Mwananchi Communication Limited pamoja na Bw. Mbuguni.

Wengine ni Bw. Abdallah Mrisho (Meneja Mkuu Global Publisher), Bw. Ansbert Ngurumo (Mhariri Mtendaji Free Media), Bw. Kwayu na Bw. Mikidadi Mahmood (Mkurugenzi Uhuru Publishers).

Wajumbe wengine Bi. Godfrida Jola kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bw. Japhet Sanga (Tanzania Media Fund-TMF), Bw. Neville Meena (Katibu TEF), Pili Mtambalike (Baraza la Habari nchini-MCT), Bw. Mwailenge,
Bw. Deodatus Balile (Mhariri Mtendaji Gazeti la Jamhuri na
Bw. Samson Kamalamo (Gazeti la Changamoto).

Kamati hiyo itafanya kazi kwa wiki mbili ili kujua uzorotaji
wa mazingira ya usalama kwa waandishi wa habari nchini.

No comments:

Post a Comment