30 November 2012

BAKWATA waanza kutoa ushahidi kesi ya Ponda



Na Rehema Mohamed

KESI ya kuvamia uwanja wa Markas inayomkabili Shekhe
Ponda Issa Ponda na wenzake 49, imeanza kuunguruma jana.

Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Bw. Suleiman Golila, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kitusu kuwa, kiwanja namba 311/3/4 kitalu D, kilichopo Chang'ombe Markas ni mali ya Kampuni ya Agritanza Ltd.

Bw. Golila ambaye ni shahidi wa kwanza upande wa mashtaka, aliyasema hayo mbele ya Hakimu Victoria Nongwa, wakati
akitoa ushahidi wake.

Huku akiongozwa na wakili wa Serikali Bw. Tumaini Kweka, Bw. Golila alisema BAKWATA iliipa kampuni hiyo eneo hilo baada ya kufikia makubaliano yaliyopitishwa na kikao cha Maulamaa.

Alisema katika makubaliano hayo, kampuni hiyo iliiipa BAKWATA eneo la ekali 40, lililopo Kisarawe mkoani Pwani ambapo eneo la Markas lina ukubwa wa ekari nne.

Aliongeza kuwa, awali eneo linalokadiliwa kuwa na ukubwa
wa ekeli 27, lilikuwa chini ya umiliki wa Serikali.

“Serikali ya Misri na Tanzania, walikubaliana kuwasidia Waislamu waliopo nchini kwa ajili ya kujenga Chuo cha Kiislamu cha Elimu ya Juu hapa Tanzania,” alisema.

Aliongeza kuwa, kutokana na makubaliano hayo Serikali ya Tanzania ilitoa eneo la Chang'ombe Markas ambapo Serikali ya Misri ikasema Wizara yake ya Wakfu ndiyo itakayosimamia
suala zima la utekelezaji wa ujenzi wa chuo hicho.

Katika Makubaliano hayo, Serikali ya Misri iliitaka Serikali ya Tanzania kutafuta chombo ambacho kitasimamia shughuli hizo
nchini hivyo kuteuliwa BAKWATA.

“Sehemu ya mkataba huo kati ya Serikali ya Misri na Tanzania, ulisema baada ya kukamilika ujenzi huo, eneo hilo na mali zote zitakazokuwepo zitakuwa chini ya BAKWATA,” alisema.

Baada ya Serikali kukabidhi eneo hilo kwa BAKWATA, nao walimega sehemu ya eneo na kulitoa kwa Taasisi ya Kiislamu ya DYCC ambayo ilijenga shule, eneo lingine kupewa mfanyabiashara  Bw. Yusuf Manji na kubakia eneo la ekali nne.

Bw. Golila alisema kuwa, umegwaji huo uliwahi kulalamikiwa na baadhi ya Waislamu kuwa haukufuata taratibu hivyo Mufti aliunda tume ya kuchunguza tuhuma hizo ambapo mwisho wa siku baadhi ya viongozi waliohusika walivuliwa uongozi.

Alisema katika uchunguzi huo, iligundulika eneo la ekali nne zilizobaki hazitoshi kujenga chuo kama ilivyoadhimiwa awali
hiyo BAKWATA walilazimika kutafuta eneo mbadala.

Aliongeza kuwa, kampuni hiyo ilikuwa na eneo la ekari 20, lililopo Kisarawe hivyo BAKWATA walikubaliana kubadilishana maeneo hayo lakini kabla ya makubaliano kilikaa kikao cha Maulamaa.

“Kikao hiki ambacho kina mamlaka ya juu kwa BAKWATA, kilifikia makubaliano ya kutoa eneo hilo kwa kampuni hii na
wao watupe eneo la ekeli 40 ili tutekeleze azma ya kujenga
Chuo Kikuu cha Kiislamu,” alisema Bw. Golila.

Shahidi huyo alitoa nakala ya muhtasari wa Kikao cha Maulamaa kilichokaa na kupitisha makubaliano hayo lakini nakala hiyo ilikataliwa kupokelewa na Mahakama kama kielelezo kwa
kuwa ilikuwa kopi si orijino. Kesi hiyo imeahirishwa hadi
Desemba 13 mwaka huu.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa Oktoba 12 mwaka huu, maeneo ya Chang'ombe Markas, Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa, waliingia kwa jinai na walivamia ardhi ambayo ni mali ya kampuni hiyo kwa nia ya kujimilikisha.

Wanadaiwa kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu, walijimilikisha kiwanja hicho kwa lazima katika hali ya uvunjifu wa amani na
kuiba vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani ya sh.
milioni 59, mali ya kampuni hiyo.

Shtaka la tano, linamkabili mshitakiwa wa kwanza, Shekhe Ponda ambaye anadaiwa kati ya Oktoba 10-16 mwaka huu, katika eneo la Chang'ombe Markas, aliwashawishi wafuasi wake kutenda makosa.

1 comment:

  1. Bakwata wanatakiwa kutoa maelezo sahihi je huo mradi uliazimiwa miaka mingapi iliyopita, na kwanini haujatelezwa, je umegaji huo uliokwisha fanyika unamanufaa gani kwa walengwa?.Ponda naye anatakiwa kujua kuwa nchi inatawaliwa na sheria angefanya SUBIRA na kutafuta haki kwenye Mamlaka zilizopo.

    ReplyDelete