16 August 2012

Msondo Ngoma yaihofia Mlimani Park


Na Mwandishi Wetu

BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini Msondo Music 'Msondo Ngoma', imesema italazimika kutumia jenereta katika mapambano wake dhidi ya DDC Mlimani Park 'Sikinde Ngoma ya Ukae', ili kuepuka hujuma.

Mpambano huo wa kumtafuta nani kali kati ya bendi hizo kongwe nchini, umepangwa kufanyika katika sikukuu ya Idd el Fitr, katika viwanja vya Leaders Klabu.

Akizungumza Dar es Salaam jana Meneja wa bendi hiyo, Said Kibiriti alisema wameamua kutumia jenereta ili kuepuka hujuma zinazoweza kufanywa na wapenzi wa Mlimani Park ya kukata umeme kama ilivyotokea Desemba 25 mwaka jana katika mpambano kama huo.

“Katika pambano letu lililopita katika sikukuu ya Krismasi mwaka jana lililofanyika TCC Club Chang’ombe, wapinzani wetu walitukatia umeme kwa makusudi,” alisema.

Alisema kutokana na tukio hilo ndiyo maana wameamua watatumia genereta kubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mtanange huo.

Amewataka wapenzi wa Msondo kuondoa shaka kwa kuwa jenereta hilo ni kubwa na lenye uwezo wa kuwasha sehemu kubwa, hivy hata kiwango cha muziki utakaopigwa utakuwa wa hali ya juu.

Kwenye pambano la mwaka jana, Msondo ilitumia umeme wa kawaida ambao ulikuwa ukikatika mara kwa mara, kitu ambacho kilidaiwa kuwa ni hujuma kutoka kwa wapenzi wa Sikinde ambao wao walikuwa wanatumia umeme wa jenereta.

Pambano hilo ambalo linadhaminiwa na Konyagi, limeanza kuvuta hisia za mashabiki wa muziki wa dansi nchini kutokana na upinzani uliokuwepo katika bendi hizo.

No comments:

Post a Comment