16 July 2012

Asasi yataka maelezo hatima ya mwanafunzi akijifungua



Na Anneth Kagenda

SERIKALI imetakiwa kuweka bayana kama kuna sera inayoruhusu   mwanafunzi kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Maendeleo Trust Fund ya wilayani Kyera mkoani Mbeya Bw. Amos Mwakabambo, wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi yake kuhusu tatizo la mimba mashuleni
.

Alisema suala hilo halipo wazi na ni moja ya changamoto zinazoikabili Serikali. Alisema utafiti uliofanywa na asasi yake umebaini wanafunzi wengi wanapata mimba, lakini hakuna sera inayowalinda.

"Tulifanya utafiti kwa miezi mitatu katika shule zaidi ya 10  kuanzia darasa la tatu hadi la saba na kuzungumza na wanafunzi ili kujua matatizo wanayokumbana nayo," alisema.

Alisema walengwa kwenye utafiti walisema wanakaa mbali na shule, wazazi kurudi usiku na vikwazo vingine.

Alisema kutokana na sababu hizo na zingine ni wazi kuwa  wazazi wanahusika na tatizo la mimba. Alitaka sera ieleze bayana kuwa mwanafunzi anayepata mimba anaruhusiwa kurudi shuleni baada ya kujifungua.

Alisema katika utafiti huo wanafunzi 14 waligundulika wakiwa wajawazito. Pia alisema wanalenga kutoa elimu kuhusu mtoto wa kike , kwa wale ambao wameishaacha masomo baada ya kupata mimba. Alisema wanapatiwa elimu ya ujasiriamali na afya ya uzazi.


No comments:

Post a Comment