20 January 2012

Mapya yaibuka mgogoro CUF

*Wakili ataka Maalim Seif akamatwe, afungwe jela
*Awasilisha ombi la kuitwa mahakamani na wenzake

*Ni wale walioshiriki kikao cha kumtimua mteja wake
*Hamad asema CUF haina tofauti na kioo kilichopasuka


Rachel Balama na Grace Ndossa

MBUNGE wa Wawi, Zanzibar, kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Hamad Rashid Mohammed
, kupitia wakili wake, Bw. Agustine Kisarika, ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iwaite wajumbe wote waliohudhuria kikao kilichotoa uamuzi wa kumfukuza uanachama mteja wake ili waeleze kwa nini wasifungwe jela kwa uamuzi waliotoa.
Miongoni mwa vigogo wa chama hicho ambao wanaguswa na ombi la Bw. Kisarika katika Mahakama hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad.
Ombi hilo liliwasilishwa katika Mahakama hiyo chini ya hati ya dharura. Ombi la pili ambalo limetolewa na Bw. Kisarika kwa niaba ya mteja wake ni kuitaka Mahakama ione kuwa, mkutano uliomvua uanachama ni batili.
Akitoa hoja za kisheria jana mbele ya Jaji Augustino Shangwa anayesikiliza shauri hilo, Bw. Kisarika, aliiomba Mahakama hiyo iharakishe kusikiliza kesi hiyo kwa sababu mteja wake amefungua kesi chini ya hati ya dharura.
Kwa kuwa kesi hii imefunguliwa kwa hati ya dharura, naiomba Mahakama iharakishe kusikiliza kesi na kutoa uamuzi mapema kwani mteja wangu (Bw. Mohammed) anatakiwa kuhudhuria shughuli za bunge,¡± alisema, Bw. Kisarika.
Akijibu hoja za wakili huyo, Jaji Shangwa, alisema kesi hiyo haiwezi kuendeshwa haraka kwani bunge haliwezi kufanya chochote kuhusu mgogoro huo zaidi ya kusubiri uamuzi wa mahakama.
Wakili wa CUF, Bw. Twaha Silima, aliiambia Mahakama kuwa, chama hicho kilipokea hati ya kuitwa mahakamani Januari 13 mwaka huu, saa saba mchana, hivyo ilibidi waifanyie kazi Jumatatu ya Januari 16 mwaka huu.
Mheshimiwa Jaji, mimi kama wakili wa CUF nilipokea hati Januari 17 mwaka huu, Wakili mwenzangu Bw. Job Kerario, aliipata Januari 18 mwaka huu, hivyo tunaomba mahakama itupe muda wa kuwasilisha hoja kwa njia ya maandishi na tupangiwe muda ambao utatosheleza kuwasilisha majibu,¡± alisema.
Jaji Shangwa alikubaliana na maombi hayo na kupanga kusikilizwa Januari 27 mwaka huu, ambapo CUF iwe imewasilisha majibu yao na Bw. Mohammed, atajibu hoja hizo Februari 6 mwaka huu.
Wakati huo huo, Mahakama hiyo imepanga kuanza kusikiliza kesi hiyo Februari 13 mwaka huu. Pande zote katika mgogoro huo zilikubaliana uamuzi wa kesi hiyo utolewe kabla ya Machi 13 mwaka huu.
Kabla ya Jaji Shangwa hajaahirisha, kesi hiyo alishauri wanachama wa pande zote, wasisumbuke kufika mahakamani wakati kesi hiyo itakapokuwa inaendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Bw. Mohammed alisema CUF imepasuka na kukosa mwelekeo.
Kioo kikipata vumbi kinafutwa lakini kikipasuka kinatupwa hivyo Watanzania wasubiri dira mpya baada ya mahakama kutoa uamuzi, alisema Bw. Mohammed.

3 comments:

  1. kwa maneno unayosema hamadi toka ufukuzwa thamani yako imeshuka sana na inadhihirisha ukweli wa kuwa wewe ni another MAPALALA.
    Nakushauri achana na C.U.F mission yako na wenzio imeshidikana unazidi kujidharirisha wenzio hata hawakujibu wanakuona kama kinyago vile.wengi walikwenda CUF kwa lengo la kukiua majina tunayo lkn waangalie leo hii wako wapi.Fikiri kabla ya kutenda Hamad!WAWI hawakutaki nani atakutaka zaidi ya pupet wenzio mnaotumiana kuua upinzinia nchini kwa kigezo cha Democracy.GO TO HELL HAMADI

    ReplyDelete
  2. Kwa mtazamo wa wachambuzi wa kisiasa, Hamad Rashid aidha hakufanya utafiti yakinifu wa 'mradi' wake wa kisiasa au alidharau ushauri wa wataalamu kabla kubonyeza kifungo cha uzinduzi wa 'mradi' huo.

    Wataalamu wa saikologia pia wanaashiria huu ndio mwanzo wa mwisho wa safari yake ya kisiasa Zanzibar na bila ya kupata baraka Dar, huenda akaathirika kisaikologia kutokana na kukosa kile alichokipania cha kutwaa nafasi ya juu katika uongozi huko visiwani.

    Wataalamu wa kibiashara wangemshauri Bwana Hamad kuachana na siasa za Visiwani na kutumia vijipesa alivyonavo kuendesha biashara na ujasirimali, eneo ambalo linaweza kumrejeshea hadhi yake siku za usoni.

    Siasa za Tanzania zina utata. Bila ya kuwa mwangalifu unaweza kupoteza nafasi adhimu kwa tamaa ya muda mfupi. Rasilimali ya siasa za Tanzania sio FEDHA bali ni WATU. Imedhihirika Hamad Rashid hana 'political base' Visiwani ndio maana alibaki Dar kupiga debe HOJA zake badala ya kuwepo katika jimbo lake.

    Katika juhudi zake za kutapata, tunategemea kumuona Bwana Hamad kuisakama sana CUF na viongozi wake wa juu hatua ambayo kimsingi itamwangamiza mwenyewe...

    ReplyDelete
  3. Kama wanampenda na kumuamini kweli Hamadi wampokee na kumrejesha CCM na wampe cheo alicgokipoteza kutokana na huenda kumshauri kufanya aliyoyafanya na
    wala msimdharau na kumpiga teka kama vile mlivomfanyia Bi Magimbi.CUF ina haki kuyafanya yenye maslahi na chama na wala hakuna haki ya kuinhiliwa. Mbona CCM iliwahi kuwafukuza wengi wakiwemo Maalim Seif na huyo Hamadi mwenyewe na hatujamsikia yeyote kutaka CCM kuburuzwa mahakamani? Wacheni nyie

    ReplyDelete