Na Ramadhan Libenanga,Morogoro
Kesi inayomkabili
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda,
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Morogoro, jana imeahirishwa baada ya
wakili wake, Bw. Juma Nassoro, kuwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu katika
kipindi cha mwezi mmoja.
Shekhe Ponda
alifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo wakili Bw.
Yahaya Njama ambaye akimwakilisha mahakamani hapo, aliiambia mahakama hiyo
kuwa, Bw. Nassoro anasumbuliwa na macho.
"Mheshimiwa
Hakimu(Richard Kabate),nimekuja hapa mahakamani kumwakilisha wakili wa
mshtakiwa (Nassoro), ambaye anasumbuliwa na macho hivyo yupo safarini nchini India kwa
matibabu ya mwezi mmoja," alisema Bw.Njama.Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Mfawidhi wa
mahakama hiyo,Bw .Kabate alisema kutokana na udhuru ya Bw. Nassoro, aliahirisha
kesi hiyo hadi Novemba 7, mwaka huu.
Wakili wa Serikali, Bw. Bernard
Kongola,aliuomba upande wa mshtakiw a kuhakikisha Bw. Nassoro anafika mahakamani
siku hiyo ili kesi hiyo ianze kusikilizwa na kupunguza gharama za Serikali kuendesha
kesi kutokana na kumsafirisha mshtakiwa kila inaposomwa katika mahakama hiyo.
Shekhe
Ponda anakabiliwa na mashtaka matatu ambapo Agosti 10 mwaka huu, eneo la Uwanja
wa Ndege, Manispaa ya Morogoro, anadaiwa kuwaambia Waislamu wasikubali uundwaji
wa Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti akidai zimeundwa na Baraza Kuu la
Waislamu nchini (BAKWATA), ambao ni vibaraka wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
Serikali.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwaagiza waumini hao
kuwa, kama watu hao watajitokeza kwao na
kujitambulisha ni Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti, wafunge milango na
madirisha wawapige.Ilielezwa kuwa, kauli hiyo ni kinyume cha
agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, iliyotolewa na Hakimu Victoria Nongwa, Mei 9 mwaka huu, iliyomtaka
ahubiri amani kwa mwaka mmoja.
Shtaka la pili, ilidaiwa Agosti 10 mwaka huu,
eneo la Uwanja wa Ndege, Manispaa ya Morogoro, Shekhe Ponda aliwaambia Waislamu
Serikali ilipeleka jeshi mkoani Mtwara kushughulikia vurugu zilizotokana na
gesi ili kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya
wananchi ni Waislamu.
Shekhe Ponda anadaiwa kuwaambia wafuasi wake
kuwa Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa mwarabu
asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao
kwa sababu asilimia 90 ya wananchi wa huko ni Wakristo.
Shtaka la tatu ambalo linafanana
na lile la pili, nalo linadaiwa kutendwa Agosti 10 mwaka huu, ikidaiwa Shekhe
Ponda aliumiza imani za watu wengine kinyume na kifungu cha sheria namba 390 na
kanuni ya adhabu namba 35 cha mwaka 2002, lakini aliyakana mashtaka hayo.
No comments:
Post a Comment