Na
Mwandishi Wetu
Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe , leo anatarajiwa kuwa
miongoni mwa washiriki wa mjadala mpana kuhusu njia za kumaliza tatizo la ndoa
za utotoni , ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya mtoto wa kike Duniani.
Mjadala huo
umeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu
(UNFPA), Kikundi cha Mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania yanayoshughulikia jinsia,
kwa kushirikiana na Jukwaa la Graca Machel linalopigania hadhi ya mtoto.
Maadhimisho ya
pili ya siku ya mtoto wa kike duniani nchini Tanzania yenye kauli mbiu kuwa;
"Kuwawezesha wasichana, kuhakikisha haki zao za binadamu na kushughulikia
ubaguzi na unyanyasaji wao ni muhimu kwa maendeleo ya familia nzima ya
wanadamu."
Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya ndoa za utotoni
duniani. Kwa wastani, watoto wawili kati ya watano wanaolewa kabla ya kutimiza
umri wa miaka 18.
Mjadala huu
unalenga kuchochea zaidi ushirikiano ulioundwa kwa ajili ya matokeo bora kwa
watoto ikiwa ni pamoja na wasichana na wavulana na hasa uraghibishi endelevu na
wa kina kuhusu suala la ndoa za utotoni na ajenda pana kuhusu haki za wanawake
na watoto.
Washiriki
wengine ni pamoja na Shekhe Alhad Musa Salim, Askofu Jacob ole Paul Mameo,
Mkurugenzi Mtendaji wa KIWOHEDE, Justa Mwaituka na Bi.Valerie Msoka , Mkurugenzi
Mtendaji wa Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania atakayeongoza mjadala huo na
Jama Gulaid ambaye ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini.
Mama Graca
Machel atawasalimia washiriki kwa njia ya video, washiriki wote watakuwa na
nafasi ya kuuliza maswali jopo la wazungumzaji na pia kushiriki mjadala kwa
kuchangia mada kwa kutumia utaalamu na ufahamu.
Wakati
huo huo ,Grace Ndossa,anaripoti kuwa Shirika la Kimataifa la
Plan International, leo linaadhimisha siku hiyo kwa kuelimisha jamii na kutetea
haki za mtoto wa kike.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaama jana kuhusu kampeni hiyo, Mkurugenzi Mkazi
wa Plan International, Jorgen Haldorsen, alisema kampeni hiyo itafanyika katika
viwanja vya Shule ya Benjamini Mkapa.
Alisema lengo
ni kupambana na ubaguzi wa kijinsia na kuboresha maisha ya wasichana milioni
nne duniani na zaidi ya wasichana 300,000 nchini Tanzania kwa kuwawezesha
kujiunga shuleni, kupata stadi za kiufundi na maisha pamoja na kujikimu.
Alisema pia kuwawezesha wasichana kushiriki
katika shughuli mbalimbali katika jamii na kulindwa kwa kukabiliana na vikwazo
dhidi ya maendeleo ya mtoto wa kike.
Alisema inanuia kuongeza stadi, maarifa na
uelewa wa hatari zinazowakabili watoto wa kike kutokana na ukatili wa kijinsia
katika familia, shuleni na jamii katika maeneo mbalimbali.
Aliongeza kuwa Plan inatambua kuwa ubaguzi
dhidi ya wasichana ni sababu kuu inayosababisha umaskini miongoni mwa watoto,
wasichana kwa wavulana.
Alisema wasichana wana uwezekano mkubwa wa kukosa
chakula , wanakabiliwa zaidi na ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na
wanategemewa kufanya kazi nyingi za nyumbani na hivyo kuwafanya wasifikie upeo
na uwezo wao wa kiakili.
Alisema kwa hapa Tanzania kampeni hiyo
ilizinduliwa rasmi na shirika hilo Oktoba mwaka jana kwa kushirikiana na wizara
mbalimbali za Serikali, mashirika ya haki na ustawi wa watoto, mashirika ya
Umoja wa Mataifa hapa nchini, mashirika ya kitaifa na kimataifa, watoto pamoja
na wadau wengine.
Alisema kwa mwaka huu siku
hiyo inasherehekewa kupitia shughuli na matukio mbalimbali nchi nzima ambayo
yanajumuisha watoto na jamii zao, vitengo na wizara mbalimbali na taasisi wabia
za kijamii.
No comments:
Post a Comment