07 January 2013
Yanga hakuna kulala Uturuki *Wachezaji walioitwa Stars waendelea 'kukamua'
Na Zahoro Mlanzi
BAADA ya kulazimishwa sare na timu ya Arminia Bielefeld ya Ujerumani, vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, timu ya Yanga imeendelea na mazoezi katika viwanja vya Fame Residence na jana jioni ilitarajia kuanza mazoezi ya 'gmy'.
Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 na timu hiyo kwenye Uwanja wa Adora Belek - Antalya ambapo bao pekee la Yanga lilifungwa na Jeryson Tegete aliyetokea benchi akichukua nafasi ya Said Bahanuzi.
Kwa mujibu wa mtandao wa timu hiyo, Kocha Brandts ameendelea kukifua kikosi chake na kukifanyia marekebisho ya baadhi ya makosa yaliyojitokeza katika mchezo wa juzi ambao hata hivyo Yanga iliutawala kwa kipindi chote cha mchezo.
Bielefeld ambayo awali hawakutegemea Tanzania kuwa kunaweza kuwa na timu ambayo inaweza kuwapa upinzani, walikiri mwishoni mwa mchezo kwamba Yanga ina timu nzuri na hawakutegemea kuona kiwango kizuri kama hicho, mtandao huo ulimkariri mmoja wa maofisa wa Bielefeld.
Taariza ziliendelea kusema kwamba Bielefeld ilikuwa imetoka kuifunga Bayern Levekursen 4-2 katika mchezo wa Kombe la Ujerumani, walikutana na wakati mgumu kutokana na Yanga ilivyoonesha umahiri wake.
Brandts alisema amefarijika na matokeo ya mchezo huo, japokuwa lengo lake kubwa lilikuwa ni kupata ushindi katika mchezo huo lakini wachezaji wake waliweza kufanya kazi nzuri uwanjani kitu kilichofanya Wajerumani kushangaa.
Yanga mara baada ya mazoezi ya jana asubuhi, jioni ilitarajiwa kufanya mazoezi ya kujenga mwili na misuli katika gmy ya hotel ya Fame Residence Lara & Spa ambapo leo asubuhi itaendelea na mazoezi katika viwanja vya Fame Residence Football.
Wakati huohuo, wachezaji wa timu hiyo walioitwa katika timu ya Taifa (Taifa Stars) kujiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Ethiopia, wameendelea na mazoezi kama kawaida licha ya Stars kuingia kambini jana jioni.
Wachezaji hao ni Nadir Haroub 'Canavaro', Simon Msuva, Frank Domayo, Athuman Idd 'Chuji' na Kelvin Yondani ambapo kwa mujibu wa mtandao huo katika baadhi ya picha ilizotoa jana walionekana wakifanya mazoezi.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura kuzungumzia kuhusu muafaka wa wachezaji hao, alisema wazungumzo yalifanyika na wanachosubili ni kuona kama watajiunga au la.
"Mazungumzo si na Yanga pekee ila kwa timu zote zenye wachezaji walioitwa Taifa Stars, wanatakiwa kuanza kuripoti kuanzia leo saa 12 jioni hivyo ni suala la kusubili tuone itakuwaje au unaweza kuzungumza na Yanga katika hilo," alisema Wambura.
Alipotafutwa Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako alisema,:"Nyie waandishi kila kukicha suala ni hilo hilo la Yanga kwani hata wasipoenda itakuwaje, mimi naomba uwaulize TFF sitaki kuzungumzia hilo tena kwani nimechoka na usumbufu wenu," alikata simu kwa hasira na hata alipopigiwa tena hakupokea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment