11 January 2013

Wahariri watoa maoni yao kwa Tume ya Katiba


Na Mwandishi Wetu

JUKWAA la Wahariri nchini (TEF), jana liliwasilisha mapendekezo matatu yanayohusiana na tasnia ya habari kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya inaongozwa na Jaji mstaafu, Joseph Warioba.

Mapendekezo hayo yaliwasilishwa Dar es Salaam jana na Mjumbe wa TEF, Bw. Deodatus Balile kwa niaba ya jukwaa na kusisitiza kuwa, kama maoni hayo yatafanyiwa kazi, yatasaidia kupatikana Katiba Mpya yenye kiwango kinachokubalika kitaifa na kimataifa.

Alisema mapendekezo hayo yametokana na Mkutano wa Wahariri uliokaa mkoani Tanga, Desemba 2012 na kujadili kwa kina mahitaji
ya tasnia ya habari katika Mchakato wa Katiba Mpya.

“Maeneo matatu tuliyowasilisha ni Uhuru wa Vyombo vya Habari, Haki ya Kupata Habari na Uhuru wa Kutoa Mawazo, mambo mengi tuliyajadili katika kikao chetu lakini tukaamua kujielekeza katika mambo matatu ya msingi yanayohusu taaluma.

“Pamoja na umuhimu wa maeneo mengine katika Katiba Mpya, yapo makundi yenye wajibu wa kuyazungumzia,” alisema.

Aliongeza kuwa, TEF inataka Katiba Mpya iwe na ibara inayohusu uhuru wa vyombo vya habari ambayo itatamka kuwa, Bunge halitatunga sheria yenye kudhibiti au kufisisha kwa njia yoyote uhuru wa vyombo vya habari.

Ibara hiyo pia ihakikishe Wahariri, wachapishaji wa magazeti na vyombo vingine vya habari hawapaswi kudhibitiwa, kuingiliwa na Serikali, kuadhibiwa au kusumbuliwa kutokana na mawazo, maoni wanayotoa kupitia tahariri, maudhui yaliyochapishwa, kutangazwa na vyombo vyao.

Chombo chochote cha habari chenye wajibu wa kusambaza taarifa kwa jamii kuhusu au dhidi ya mtu yeyote, kinawajibika wa kutoa fursa ya kuchapisha mawazo ya upande wa pili kama yapo, kutoka kwa mtu ambaye taarifa au chapisho linamuhusu.

Pendekezo jingine ni vyombo vyote vya habari (vya Umma na Binafsi), vinapaswa kutoa fursa sawa na kuwezesha uwasilishaji  maoni na mawazo pinzani.

Akizungumzia pendekezo la Haki ya Kupata Habari, Bw. Balile alisema kila mwananchi ana haki ya kupata habari, Serikali kuchapisha na kutangaza taarifa muhimu zinazolihusu Taifa
bila kushurutishwa.

Katika pendekezo la Uhuru wa Kutoa Mawazo, alisema kila ila mtu ana haki ya uhuru wa kutoa mawazo, kutafuta, kupokea au kutoa taarifa, ubunifu wa kisanii na utafiti wa kisayansi.

Alisema haki ya uhuru huo haitahusisha propaganda kwa ajili ya vita, uchochezi wa kuanzisha vurugu, hotuba za chuki au utetezi
wa chuki inayochochea ukabila, ubaguzi kwa watu wengine, mapambano au mazingira yoyote ya ubaguzi yaliyozuiliwa
katika Katiba husika.

1 comment:

  1. TUSEME UKWELI TANZANIA KUNA VITUO VYA RADIO ZAIDI YA 86 VITUO VYA TELEVISHENI VISIVYOPUNGUA 26 VINA UHURU WA KUROPOKA HAKUNA CHOMBO CHA KUTATHMINI MAUDHUI YA VYOMBO HIVI LEO UKO MMOMONYOKO WA KUTISHA WA MAADILI YA VIJANA VYOMBO VYA HABARI NI MIONGONI MWA WAKALA WA MALEZI YA VIJANA PAMOJA NA FAMILIA,SHULE ,DINI NA MAKUNDIRIKA WALIOZEMBEA NA KUSABABISHA MMOMONYOKO WA MAADILI WA KUTISHA WA VIJANA WA LEO KWA KIVULI CHA UTANDAWAZI

    ReplyDelete