11 January 2013

JK atangaza kiama waliovamia misitu, vyanzo vyote vya maji



Na Mwandishi Wetu
   
RAIS Jakaya Kikwete, amewaagiza viongozi wote nchini, kuwaondoa mara moja watu waliovamia misitu na vyanzo
vya maji hususan katika Bonde la Mto Kilombero, mkoani Morogoro.


Alisema kuanzia sasa viongozi wasiwaonee aibu watu wanaovamia misitu ya Serikali, kuharibu vyanzo vya maji na uoto wa asili.

Rais Kikwete alitoa agizo hilo jana mkoani Tabora wakati akiweka jiwe la msingi katika Mradi wa Uboreshaji, Upatikanaji wa Maji katika Mji wa Tabora, wakati akimaliza ziara ya siku tano.

“Viongozi tulisimamie hili bila woga wala aibu...wanasiasa wenzangu msiliingilie ili kupotosha watu, tuwaondoe wote
bila kuchelewa na tukifanya hivyo tunanusuru Taifa letu,” alisema.

Akizungumza na wakazi wa Bwawa la Igombe, nje ya Mji wa Tabora, Rais Kikwete, alisema viongozi wakiendelea kuruhusu uvamizi wa maeneo ya misitu na vyanzo vya maji, watakuwa wanaliangamiza Taifa.

“Hatuwezi kukubali jambo hilo, kila mtu ana sehemu aliyotoka hivyo arudi kwao badala ya kuvamia misitu na mabonde katika maeneo mengine,” alisema Rais Kikwete.

Aliongeza kuwa, uamuzi aliochukua miezi mitatu baada ya kuingia madarakani kwa kuwahamisha wafugaji waliokuwa wamevamia Bonde la Ihefu, umeanza kurudisha uhai katika Mto Ruaha.

“Watu waliingiza ng’ombe 460,000 katika eneo hili na kuharibu mfumo mzima mzima, tuliwaondoa na sasa angalau tunaanza kuona uhai kwenye Mto Ruaha ambao ulikuwa umekauka kwa sababu ya chanzo chake kuvurugwa na kuharibiwa,” alisema.

Alisema ni jambo la hatari kwa uhai wa binadamu kuharibu
vyanzo vya maji kwa sababau hakuna mbadala wa maji.

No comments:

Post a Comment