29 January 2013

Haki za binadamu waombwa kuingilia mgogoro wa mirathi



Na Mariamu Mziwanda

FAMILIA ya marehemu Juma Maulid wameiomba wanasheria za haki za binadamu iwasaidie kupata mirathi ya marehemu baba yao pamoja na Serikali kutokana na baadhi ya ndugu wa familia kuzikumbatia mali hizo kwa miaka mitatu na kusababisha watoto kuishi maisha ya shida na kushindwa kwenda shule.


Akizungumza jana Dar es Salaam kwa masikitiko kwa niaba ya watoto wa marehemu Seif Juma (18),mkazi wa Kijitonyama alisema kutokufunguliwa kwa mirathi hiyo kumesababisha mali za baba yao kutumiwa vibaya na baadhi ya ndugu na kuwaona watoto wa marehemu hawana haki ya kuishi katika nyumba aliyoacha marehemu.

"Tunaomba mirathi ifunguliwe tukabidhiwe mali zetu na sisi tukaishi na mama yetu anayeishi Mbagala kwani maisha tunayoishi hapa ni ya shida ambapo chakula tunafadhiliwa na majirani huku tukilazimishwa kuandika mkataba wa kuruhusu uuzwaji wa gari lililoachwa na baba yetu," alidai kijana huyo.

Aliongeza anawaomba wanasheria wa haki za binadamu na asasi nyingine za kiraia ziwasaidie ili waweze kupata haki zao ikiwa ni pamoja na kulipiwa ada ili waende shule kwani tangu shule zifunguliwe wiki mbili zilizopita hakuna dalili ya kurudi shule.

Juma alisema baba yao aliacha nyumba, magari na yadi ya kuhifadhia magari ambayo ipo Kijitonyama na hulipiwa kodi kiasi cha Dola za Kimarekani 1,000 kwa mwezi lakini ndugu yake na baba yake wa karibu amekuwa akizitumia fedha hizo kwa kuwasomesha watoto wake huku wao akiwaacha na kusaidiwa chakula na sabuni na majirani.

Alisema dada yake wa kwanza aitwaye Mariam amemaliza kidato cha nne mwaka jana na hivi sasa yupo chuo anasomeshwa na mama yake hivyo ni vyema mirathi ikafunguliwa na akapewa kazi ya kusimamia.

"Nimechoka namuomba Mungu na wahisani wanisaidie kutetea haki yetu kwani juzi kulitokea kutoelewana na huyo shangazi yake baada ya kudai ada na sabuni ya kufulia ambapo alianza kunishambulia pamoja na familia yake kisha kwenda kunipeleka kituo cha Polisi Kijitonyama  ambapo nilifunguliwa kesi ya kutumia lugha ya matusi yenye namba RB/ KJN/RB/649/13 na nilikaa mahabusu hadi mama yangu mzazi alipokuja kuniwekea zamana, "alidai.

Kituo cha Polisi Kijitonyama kilikiri kufunguliwa kwa jalada hilo dhidi ya mtoto huyo ambapo ilidaiwa kuwa anatuhumiwa kutumia lugha ya matusi dhidi ya watoto wa shangazi yake.

Naye mama mzazi wa watoto hao Husna Yauo aliiomba serikali imsaidie ili watoto wake waweze kupata haki zao za msingi kwani marehemu amecha mali ambazi zinaweza kuwasomesha watoto ambapo wapo watano na wote hawanufaiki na mali ya marehemu baba huyo.

Wakati huohuo, Abdul Maganga  Katibu wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) Kijitonyama alisema, wanafahamu kwa undani mali zilizoachwa na baba wa watoto hao lakini wamechoshwa na migogoro ndani ya familia hiyo kwani wamesuluhisha vya kutosha na uroho wa mali wa ndugu wa marehemu wanasababisha watoto hao kuishi maisha ya shida huku mtaa huo wakisubiri mahakama itende haki ili watoto waendelea na masomo

Naye Mjumbe wa shina Omary Bilali alisema amesuluhisha migogoro ya watoto hao kwa muda mrefu lakini kwa kifupi watoto hao wanateseka na wanatakiwa kupewa haki zao.

No comments:

Post a Comment