26 September 2012

Vijana waliomzomea Pinda wamekosa maadili - Wazee


Na Daud Magesa, Mwanza

WAZEE na viongozi wa dini mkoani Mwanza, wamesema kitendo cha baadhi ya vijana kumzomea Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, alipokuwa mkoani humo kwa ziara ya kikazi hivi karibuni, kimetokana na vijana hao kukosa nidhamu na maadili.

Shekhe wa Mkoa huo, Alhaji Salum Ferej, aliyasema hayo jana wakati wazee mkoani humo wakitoa tamko la kumuomba radhi Bw. Pinda kwa kuzomewa wakati akihutubia wananchi jukwaani.

Alisema kitendo hicho kimewasikitisha wananchi wengi na kuwataka viongozi wa dini kupitia makanisa na misikitini yao, kufanya kazi ya kutoa elimu ya maadili kwa vijana ili wabadilike.

“Chanzo cha tatizo hili ni vijana kuiga utamaduni wa kigeni ambao wao wenyewe umewashinda, utakuta mtoto anamburuta kortini baba yake mzazi kwa kuchapwa bakora pale anapokosa.

“Leo hii watoto wetu wa kike utakuta wanavaa nguo za ajabu lakini wazazi wanogopa kuwakemea ili wazingatie maadili ya kitanzania hivyo lazima tusaidiane kutoa elimu ya maadili kwa vijana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri mkoani hapa, Bw. William Kafiti, aliwataka wazee na wazazi kuacha tabia ya kutowakemea vijana na kuliacha jukumu hilo kwa Serikali.

Alimtaka Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Evarist Ndikilo, kuwaombea radhi wazee mkoani humo kwa Bw. Pinda.

Bw. Anthony Yakukumya, alidai vijana waliomzomea Bw. Pinda walipandikizwa ambapo hali hiyo inaweza kuvuruga demokrasia iliyopo nchini kwani kitendo hicho kilifanyika mbele ya viongozi
wa Serikali na vyombo vya dola lakini hakuna hatua zozote  zilizochukuliwa.

Wakati Bw. Pinda akihitimisha ziara ya siku nane mkoani humo, katika Wilaya ya Nyamagana, alizomewa na kundi la vijana wakati akihutubia wananchi jukwaani.

Akipokea tamko la wazee hao, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Bw. Baraka Konisaga, alisema walizuia polisi kutumia mabomu kwani waandaaji wa mpango huo, wangetumia nafasi hiyo kuilaani Serikali na kudai inaua watu raia wake.

“Nachukua ombo letu, nitalifikisha kwa Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya hatua zaidi ili amfikishie Bw. Pinda,” alisema.

No comments:

Post a Comment