Na Benedict Kaguo,Tanga
MKUU wa Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, Bw. Muhingo Rweyemamu, amesema chanzo cha tatizo la wanafunzi kushindwa kumaliza shule wilayani humo ni kutembea umbali wa kilomita 30 kwa miguu ili kufika shuleni.
Bw. Rweyemamu aliyasema hayo mjini Tanga jana katika Kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa (RCC) na kuongeza kuwa, hali hiyo inawafanya wanafunzi wakate tamaa ya kuendelea na masomo.
Alisema umbali wa kilimita 30 wanazotembea wanafunzi hao ni sawa na kilomita 150 kwa wiki hali ambayo inayochangia kuporomoka kwa elimu na ongezeko la mimba za utotoni.
Wajumbe wa kikao hicho walishangazwa na maelezo hayo, kuhoji kama kuna kiongozi anayeweza kutembea umbali huo kwa siku na kudai ni muhimu kuwepo utaratibu ambao utawaondolea adha ya kutembea umbali huo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize hapa nani anayeweza kutembea kwa miguu kilomita 30 kwa siku, lazima tuangalie upya namna ya kuwasaidia wanafunzi hawa ili wamalize masomo yao, hili ni tatizo kubwa kwa upande wa Handeni,” alisema Bw. Rweyemamu.
Alisema kutokana na hali hiyo, hivi karibuni wanafunzi 13 wa Shule ya Sekondari Kata Mazingira wamebainika kuwa na mimba baada ya kufanya ziara ya kushtukiza akiwa na Maofisa wa Idara ya Afya wilayani humo ambapo wanafunzi wawili walibainika kutoa mimba.
Bw. Rweyemamu aliongeza kuwa, tukio kama hilo alilikuta katika Sekondari ya Kang’ata, ambapo wanafunzi wanne walikuwa na mimba na Sekondari ya Kwamatuku, wakibaini wanafunzi watatu.
Aliongeza kuwa, njia pekee ya kupunguza tatizo hilo ni kuongeza ujenzi wa mabweni katika sekondari za kata ili wanafunzi waweze kuishi katika mazingira rafiki ya kujisomea.
“Ni muhimu kuwepo msisitizo wa kujenga mabweni ili wanafuzi wasiweze kutembea umbali mrefu ambao ndio chanzo cha kupata mimba na kukata tamaa ya kusoma,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Bi. Mboni Mgaza, alisema tatizo la utoro ni kubwa hasa katika Sekondari ya Mwakijembe.
Alisema hivi karibuni alifanya ziara shuleni hapo na kukuta wanafunzi 40 tu kuanzia kidato cha kwanza hado cha tatu.
“Wanafunzi wengi wanakuja shule katika vipindi vya michezo, nashauri michezo ipewe kipaumbele zaidi kwani inaweza kusaidia kupunguza tatizo lililopo,” alisema.
No comments:
Post a Comment