02 August 2012
Ngassa atua Simba
Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Azam FC imefikia makubaliano ya kumpeleka kwa mkopo mchezaji wao Mrisho Ngassa kwa klabu ya Simba na kitita cha sh milioni 25 kama ada.
Klabu hiyo imefikia hatua hiyo baada ya kumtangaza kwa siku tatu kuuzwa kwa Ngassa ambapo Yanga na Simba walipeleka ofa za kutaka kumsajili mchezaji huyo.
Kwa mujibu wa habari kutoka katika klabu hiyo, Azam wameridhia kumpeleka Ngassa Simba kutokana na klabu hiyo kuleta ofa ya sh.milioni 25 huku Yanga wao wakisema wanaishia sh. milioni 20.
Kikao cha kwanza cha kuzungumzia ofa hizo pamoja na mazungumzo kilianza juzi usiku ambapo kufukia jana mchana klabu hizo zilifikia makubaliano.
Kwa makubaliano hayo Ngassa atacheza Simba pamoja na kupokea mshahara kutoka Simba na si Azam FC kama ilivyo kwa wachezaji wengine wanaopelekwa kwa mkopo, hiyo ni kutokana na makubaliano waliofikia baina ya timu hizo mbili.
Jumatatu iliyopita Azam FC walitangaza kumuuza mchezaji huyo kwa gharama ya dola 50,000, lakini kutokana na kukosa fedha hizo wameamua kupokea sh.milioni 25 na kumpeleka Simba kwa mkopo.
Ngassa alijiunga na Azam FC misimu miwili iliyopita, katika kipindi chote alicheza misimu yote miwili huku msimu wake wa kwanza akimaliza kwa kuwa mfungaji bora wa ligi kuu.
Azam FC walifikia uamuzi wa kumuuza Ngassa kutokana na kutoonesha mapenzi yake kwa klabu, na badala yake akaonesha kuipenda klabu ya Yanga, hivyo Azam FC hawakuwa na sababu nyingine ya kuendelea kuwa naye.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment