26 July 2012
Wazazi watakiwa kuziheshimu, kuzithamini shule za kawaida
Na Anneth Kagenda
WITO umetolewa kwa wazazi nchini kutozidharau shule zinazotoa elimu ya kawaida na kukimbilia shule za kimataifa badala yake wanapaswa kuziheshimu kutokana na juhudi zinazofanyika kuhakikisha zinapata vifaa vyote vya muhimu vikiwamo vitabu.
Rais wa Taasisi ya Kilimanjaro Education Outreach (KILEO) Bw. Walter Miya, Dar es Salaam jana wakati akipokea vitabu 903 vyenye thamani ya sh. milioni tano, ambavyo vimechapishwa na Kampuni ya Business Printers Limited (BPL).
Akizungumza baada ya Meneja Masoko na Mauzo wa kampuni hiyo, Idara ya Uchapishaji Vitabu Bw. Christian Gaya, kumkabidhi vitabu hivyo, Bw. Miya alisema wazazi wengi hawawapeleki watoto wao katika shule za kawaida kwa madai hazina vitendea kazi vya kutosha vikiwamo vitabu.
“Hivi sasa tumeanza kupeleka vitabu katika Shule ya Msingi Kotela iliyoko Marangu, mjini Moshi, vya masomo yote kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, hatutaishia hapa badala tukizunguka katika shule mbalimbali na kutoa misaada kadiri ya mahitaji ya shule husika,” alisema Bw. Miya.
Alisema ameamu kutoa vitabu hivyo baada ya kuzunguka na mkewe Bi. Shawn Miya na kubaini kuwa, shule nyingi za msingi zinakabiliwa na tatizo kubwa la vitabu hivyo kusababisha wazazi wengi kupeleka watoto wao katika shule za kimataifa na binafsi.
Kwa upande wake, Bi. Miya, alisema lengo lao ni kuhakikisha kiwango cha elimu kinaongezeka katika shule mbalimbali nchini tofauti na ilivyozoeleka kwa baadhi ya watu kuwa shule hizo hazifai kupeleka watoto.
Bw. Gaya alisema vitabu hivyo vitasaidia kuinua kiwango cha elimu na kuongeza katika shule za kawaida, watoto 20 hutumia kitabu kimoja jambo ambalo ni vigumu mwanafunzi kuelewa haraka tofauti na shule za kimataifa.
“Watoto kwenye shule za kawaidaa utakuta wanang'ang'ania kitabu kimoja hivyo KILEO wanastahili pongezi kwani vitabu hivi vinaenda kwa watoto ambao ni walala hoi,” alisema Bw. Gaya.
Vitabu vilivyotolewa ni vya masomo ya hisabati, history, sayansi na mengine ambapo shule hiyo ina wanafunzi 260, walimu 11 na kutoa ahadi ya kutengeneza kabati za kuhifadhia vitabu hivyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment