31 July 2012
TUCTA kupinga Sheria Mpya ya Mifuko kwa maandamano
Na Darlin Said
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Mkoa wa Dar es Salaam, limetangaza maandamao ya amani ili kupinga sheria inayowazuia wanachama wanaojitoa kwenye Mifuko ya Hifadhi za Jamii, kutopata mafao hadi watakapofikisha umri wa miaka 50 au 60.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mratibu TUCTA, mkoani humo, Bw. Musa Mwakalinga, alisema maandamano hayo yatafanyika Agosti 4 mwaka huu.
Alisema maandamano hayo yataanzia Ofisi za TUCTA, Makao Makuu hadi Ofisi za Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).
“Tumeamua kuandaa maandamano ili kupeleka malalamiko yetu kwa Serikali kupitia SSRA na kufikisha kilio cha wafanyakazi, wafanyabiashara na wakulima wa nchi hii,” alisema.
Bw. Mwakalinga alisema hawakubaliani na mabadiliko ya sheria hiyo kwani ina athari kubwa kwa wanachama, kuongeza umaskini kwa wafanyakazi hasa wanapoachishwa au kuacha kazi.
Aliongeza kuwa, sheria hiyo ni kandamizi kwa wanachama kwani mfanyakazi anapoachishwa au kuacha kazi kwa hiyari yake, hawezi kupata mafao yake kwa sababu sheria haimruhusu kuyachukua kabla hajafikisha miaka iliyotajwa.
“Kimsingi aiingii akilini kama ajira ya mfanyakazi itasitishwa akiwa na umri wa miaka 30 alafu asubiri miaka 25 ndipo apate mafao yake wakati umri wa Mtanzania kuishi ni miaka 47 (mwaanaume) na mwanamke 44,” alisema Bw. Mwakalinga.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa TUCTA Bw. Nicholas Mgaya, ameitaka Serikali kufanya mabadiliko ya haraka kuhusu sheria hiyo au kuandaa utaratibu ambao utahakikisha mwanachama ambaye atajitoa na mifuko hiyo anapata haki yake kwa wakati.
Alisema TUCTA haitashindwa kuchukua hatua za kisheria kama SSRA itaendelea kushikilia msimamo wa matumizi ya sheria hiyo.
“Tumesikitishwa na kitendo cha kutangazwa mabadiliko ya sheria hii wakati mchakato wake bado haujakamilika, hii inatupa mashaka kuwa, huenda sheria hii ina mabadiliko ambayo wadau hatukuyaridhia,” alisema Bw. Mgaya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tunaomba muandae maandamano ya amani ya nchi nzima maana hili ni janga la Kitaifa.
ReplyDeleteTunashukuru sana kwa ushirikiano wenu.